2012-10-24 14:06:15

Barua ya kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa nchi yao!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda katika barua yake ya kichungaji kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka hamsini tangu Uganda ilipojipatia uhuru wake, imekuwa ni fursa ya kuadhimisha urithi wao, kufanya tathmini ya kina kwa kuangalia mafanikio na mapungufu yaliyojitokeza ili kujiwekea mikakati ya maboresho kwa siku zijazo, wakiongozwa na kauli mbiu “kwa ajili ya Mungu na Nchi yangu”.

Sehemu ya kwanza ya barua hii ya kichungaji inaangalia kwa namna ya pekee, kukua na kupanuka kwa Kanisa Katoliki nchini Uganda katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, matunda na kazi ya Roho Mtakatifu katika Uinjilishaji, ulioshuhudia Wamissionari wakijitoa kimaso maso kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kiasi hata cha kumwaga damu yao ambayo kwa sasa imekuwa ni mbegu ya Ukristo nchini Uganda.

Kanisa Katoliki Uganda katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, limebahatika kupata Makardinali wawili, Maaskofu wakuu watano na Maaskofu ishirini na nne na kati yao wanne tayari wametangulia katika usingizi wa amani wakiwa na tumaini la maisha ya uzima wa milele. Kuna zaidi ya watawa elfu tatu na mia mbili wanaotekeleza utume wao ndani na nje ya Uganda katika Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa.

Idadi ya Makatekista ni zaidi ya elfu kumi na tatu na kwamba, idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki kwa sasa ni sawa na asilimia arobaini ya idadi ya wananchi wa Uganda hadi kufikia mwaka 2011. Licha ya mafanikio yote haya bado kuna kazi kubwa inayolikabili Kanisa Katoliki nchini Uganda, hasa zaidi kwa kutaka kuamsha ari na moyo wa kimissionari, changamoto iliyotolewa na Papa Paulo wa Sita alipoitembelea Uganda kunako mwaka 1969.

Kanisa Katoliki Uganda lina jumla ya Majimbo makuu manne yanayoundwa na Majimbo kumi na tisa na kwamba, kuna jitihada za makusudi kabisa za kutaka kulitegemeza Kanisa kwa rasilimali watu na fedha. Vyama vya kitume ni fursa kubwa kwa Kanisa katika azma yake ya Uinjilishaji Mpya nchini Uganda. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, Familia ya Mungu katika ujumla wake, inajitahidi kuyafahamu kwa kina Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuyamwilisha malimwengu pamoja na kuboresha mahusiano kati ya Serikali na Kanisa.

Juhudi hizi zinakwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili waVatican. Lengo ni kusimama kidete kwa pamoja kulinda na kutetea haki msingi za kijamii, mafao ya wengi pamoja na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Mshikamano huu pia unajionesha katika utoaji wa huduma za kijamii hasa kwa kuwasaidia waathirika wa UKIMWI.

Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Uganda, hata kama bado wanakabiliana na mfumo dume unaowanyanyasa na kuwadharau. Chama cha Wanawake Wakatoliki Uganda kilichosambaa katika Majimbo mbali mbali nchini Uganda, kimekuwa ni msaada mkubwa sana katika kuwajengea wanawake uwezo pamoja na kuwapatia majiundo endelevu ili waweze kutekeleza wito na dhamana yao ndani ya Kanisa kwa ufanisi mkubwa zaidi. Wanawake wamekuwa na mchango mkubwa, lakini hasa zaidi ni katika sekta ya elimu na afya.

Kanisa Katoliki nchini Uganda limeendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu zenye viwango na ubora unaotakiwa na Serikali na Jumuiya ya Kimataifa. Kanisa linamiliki na kuendesha Shule za Awali zipatazo 139, Shule za Msingi ni 4,775, Shule za Sekondari ni 594. Taasisi za elimu ya juu pamoja na Seminari ziko tano kwa sasa. Shule, taasisi za Elimu ya juu na Vyuo vikuu vimechangia katika majiundo na malezi ya maelfu ya wananchi wa Uganda. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, watu hawa watakuwa ni chumvi na mwanga katika kuyatakatifuza malimwengu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linasema, katika kipindi cha Miaka hamsini ya uhuru wa Uganda, linajivunia kwa namna ya pekee, mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mawasiliano ya jamii, kwa kutambua kwamba, Kanisa lina dhamana ya kutangaza Ukweli Mfunuliwa kuhusu Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu. Kanisa Katoliki nchini Uganda hadi sasa lina miliki na kuendesha Vituo kumi na vitatu vya Radio, Kituo kimoja cha Televisheni bila kusahau mtandao mkubwa wa magazeti na majarida yanayochapishwa na Majimbo kadhaa.

Maaskofu wanawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii kwa kuliwezesha Kanisa kutoa sauti yake ya kinabii pamoja na mchango wake katika maendeleo endelevu ya wananchi wa Uganda. Wanasema, hata njia za mawasiliano ya jamii zinazomilikiwa na kuendeshwa na watu binafsi zinaweza kukumbatia tunu msingi na kweli za Kiinjili kama vile: Injili ya Upendo, Haki, Amani, Mshikamano; Utu na Heshima ya binadamu; mada ambazo zinaweza kuwa ni nyenzo ya Uinjilishaji Mpya, ili kuleta mabadiliko katika fikra na maisha ya watu kutoka katika undani wao.

Huduma inayotolewa na Mama Kanisa katika sekta ya afya ni mwendelezo wa utume wa uponyaji ulioanzishwa na Kristo mwenyewe, unaolenga kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Baraza la Maaskofu Katoliki linasema, Kanisa nchini Uganda linachangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya ya jamii kwa kumiliki Hospitali 30, Vituo vya Afya 252, Vyuo vya Afya na Tiba ni 13 na kwamba kuna zaidi ya wafanyakazi katika sekta ya afya elfu saba na mia tano wameajiriwa na Kanisa.

Kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Kanisa katika huduma ya afya, ingawa bado kuna haja kwa taasisi hizi mbili kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa Mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Ugonjwa wa UKIMWI umekwisha sababisha watu zaidi ya millioni mbili nukta mbili kupoteza maisha na wengine zaidi ya Watu Millioni moja nukta mbili wameathirika. Ugonjwa wa UKIMWI unaendelea kusababisha madhara makubwa katika maendeleo ya nchi kwa kupoteza nguvu kazi. Maaskofu wanakazia kwa mara nyingine tena, umuhimu wa kuzingatia na kudumisha misingi bora ya maisha ya kifamilia, maadili na utu wema kama njia ya kuepukana na maambukizi mapya ya UKIMWI.

Ni changamoto kwa wananchi wote wa Uganda katika ujumla wao kuondokana na unyanyapaa kwa wagonjwa na waathirika wa UKIMWI, wawe daima tayari kuwaonjesha upendo.

Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa UKIMWI sehemu mbali mbali nchini Uganda. Kuna Hospitali ishirini na nane na Vituo vya Afya saba vinavyotoa huduma ya dawa za kurefusha maisha. Kanisa litaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika kuwahudumia waathirika wa UKIMWI pamoja na kuweka mikakati ya kichungaji kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huu.

Maaskofu wanasema, wamekuwa mstari wa mbele kuchochea maendeleo endelevu nchini Uganda kwa kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata maboresho ya maisha yao kwa kuongeza kipato, kuwa na uhakika na usalama wa chakula kwa kukazia kilimo bora pamoja na kuwahudumia watu mbali mbali waliokumbwa na maafa asilia. Kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika kanuni bora za utunzaji wa mazingira kwa kuondokana na tabia ya uharibifu wa misitu na matumizi mabaya ya rasilimali ya nchi ambayo kimsingi ni urithi wa wananchi wote wa Uganda.

Kanisa Katoliki nchini Uganda, limeendelea kuchangia harakati za kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. Inasikitika kusema kwamba, Uganda kwa kipindi kirefu imejikuta ikitumbukia katika misigano na kinzani za kisiasa, kikabila na kidini, bila kusahau madhara makubwa yaliyosababishwa na Jeshi la Waasi la LRA. Kuna umuhimu wa kuendeleza majadiliano yanayopania kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa, sanjari na kukuza somo la uraia, jukumu ambalo linawahusu wananchi wote wa Uganda.

Baraza la Maaskofu Katoliki limekwisha anzisha Tume za Haki na Amani katika majimbo kumi na tisa, ili kuhakikisha kwamba, Familia kama Kanisa dogo la nyumbani linashiriki katika mchakato mzima wa upatanisho, haki na amani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda katika barua yao ya kichungaji, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka Hamsini tangu walipojipatia uhuru, katika sehemu ya pili, wanayaangalia pia mapungufu yaliyojitokeza nchini Uganda katika kipindi cha miaka hii. Ukosefu wa amani na utulivu pamoja na athari zake ni jambo ambalo limeacha majonzi makubwa miongoni mwa wananchi wa Uganda. Kumbe, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kisiasa kwa ajili ya mafao ya wengi nchini Uganda

Wanawake wameendelea kuathirika na mfumo dume. Licha ya mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika sekta ya elimu kuna haja wa kuendeleza maboresho, ili taifa liweze kujipatia wataalam na wagunduzi watakaosaidia kuzalisha fursa za kazi, kuliko mfumo wa sasa unaozalisha watu wanaotafuta ajira, kiasi kwamba, kuna jeshi kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira.

Vyombo vya mawasiliano ya jamii, vinapaswa kulinda na kuheshimu utu wa mwanadamu, maadili na tamaduni njema za kiafrika badala ya kuendekeza mambo yanayokwenda kinyume na maadili na utamaduni wa Kiafrika. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapaswa kuzingatiwa hata katika matumi ya njia za mawasiliano ya kijamii. Uhuru wa kujieleza uzingatie pia sheria na mafao ya wengi. Maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya Jamii yalenge mafao ya wengi na kwamba, yatumiwe pia na Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya.

Changamoto hizi kwa vyombo vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, zishughulikiwe kwa kujenga mshikamano utakao imarisha mtandao wa mawasiliano Kikanisa, kukuza vipaji, kuongeza ugunduzi, ujasiri, nidhamu pamoja na kuwa na mang’amuzi mapya.

Maaskofu wanasema, kuna haja kwa Uganda kujikita katika sera ya kuzuia na kutibu magonjwa; kuboresha huduma za afya; kupunguza gharama za matibabu ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki pamoja na kuboresha masilahi ya wafanyakazi wa sekta ya afya kadiri ya uwezo wa Serikali. Kanisa linapinga sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo. Linawahimiza wananchi wa Uganda kuchuchumilia maadili, uaminifu na kujizuia kama njia za kudhibiti maambukizi mapya ya Ugonjwa wa UKIMWI.

Kuna pengo kubwa kati ya matajiri na maskini, kielelezo cha kutokuwepo na uwiano sawa katika mgawanyo na matumizi ya rasilimali ya nchi. Umefika wakati kwa wadau mbali mbali kuunganisha nguvu zao katika mapambano dhidi ya umaskini, kama sehemu ya mchakato wa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia. Rasilimali na utajiri wa nchi uwe ni kwa mafao ya wengi. Upatanisho, haki na amani ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mikakati ya maendeleo, vinginevyo ni vigumu sana kusonga mbele kimaendeleo wakati mtutu wa bunduki unaunguruma mtaani.

Mapambano ya kisiasa yalenge kuboresha huduma na wala si kichaka cha watu kutaka kujilimbikizia utajiri. Tofauti za kijamii zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu. Watu wasipende kutawaliwa mno na mali, bali wawe tayari kushirikishana na wengine mali waliyo nayo. Ukabila rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma vimekuwa ni saratani ya kitaifa, kuna haja ya kuongoka na kuwa na maelekeo na mawazo mapya kuhusu mali na matumizi yake kama kikolezo cha haki jamii na amani.

Sehemu ya tatu ya Barua ya Kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda inabainisha changamoto kubwa iliyoko mbele yao ya kutaka kufanya mabadiliko ya ndani kuanzia katika ngazi ya mtu binafsi na Jamii kwa ujumla wake, dhamana wanayopaswa kuitekeleza katika misingi ya ukweli, uwazi na unyenyekevu, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, daima wakitafuta mafao ya wengi. Viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii wajenge ndani mwao ari na mwamko wa kupenda kuhudumia, kwa kuonesha dira na utekelezaji wake.

Maaskofu wanapaswa kuendelea kuongoza, kutakatifuza na kuwafundisha Watu wa Mungu; wakitangaza ukweli hasa zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Mapadre na Watawa watambue kwamba, wanashiriki kwa namna ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa, dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa moyo mkuu na unyenyekevu, wakitambua kwamba, wanawajibika kwa Mungu na kwa jirani zao. Viongozi wa kisiasa watekeleze wajibu wao vyema.

Familia zinakumbushwa kwamba, ni Kanisa dogo la nyumbani linaloendelea kukumbana na changamoto mbali mbali katika Ulimwengu wa Utandawazi, Maendeleo ya sayansi na teknolojia; mmong’onyoko wa maadili na utu wema bila kusahau ukanimungu na mawazo mepesi mepesi. Imani potofu, uchawi na ushirikina pamoja na tamaduni tenge ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa umakini, ili kweli familia ziendelee kutekeleza wajibu wake kwa Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Vijana wajengewe utamaduni utakaomwilisha Injili ya Upendo, haki, amani, msamaha, ukarimu, upatanisho pamoja na kuguswa na matatizo ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Vijana wapate majiundo makini: kiroho na kimwili, ili kuwaandaa kutekeleza wajibu wao na kamwe wasitumiwe kwa ajili ya kubomoa nchi.

Maaskofu katika sehemu ya nne ya barua yao ya Kichungaji wanaonesha matumaini yaliyomo kwenye sakafu ya mioyo yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Uganda. Wanapenda kuwaona Waganda wakiwa ni wachamungu; watu wanaojikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; wakiheshimu na kuthamini uhuru wa kuabudu; wakijitahidi kuchuchumilia: demokrasia, utawala bora, sheria, ukweli na uwazi; ili haki, amani na utulivu viweze kutawala na kushamiri.

Wananchi wawezeshwe ili kushiriki kikamilifu katika uongozi wa nchi, kwa njia ya maboresho ya sekta ya afya na elimu inayowajengea uwezo wa kupambana na changamoto za maisha. Wananchi waoneshe umoja wa kitaifa kwa kukumbatia tunu msingi za kitaifa. Taifa liwe na miundo mbinu ya uhakika, watu wapate huduma ya maji safi na salama, daima watambue kwamba, kupanga ni kuchagua.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linahitimisha Barua yake ya Kichungaji katika Maadhimisho ya Jubilee ya miaka hamsini tangu Uganda ilipojipatia uhuru wake kupambana na changamoto mbali mbali kwa ujasiri na moyo mkuu, daima kila mwananchi akipania kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, misingi ya haki na amani. Wajifunze kutokana na makosa yaliyopita na kuganga yale yajayo kwa kukazia mafao ya wengi.

Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, wataweza kutekeleza kwa uaminifu: mawazo na changamoto zinazotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika pamoja na Waraka wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Dhamana ya Afrika, Africae Munus: Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ya Uinjilishaji Mpya; changamoto za Maadhimisho ya Jubilee ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Mwaka wa Imani.

Matukio yote haya si bure, bali ni neema ya Mungu inayopania kuleta upya katika maisha ya wananchi wa Uganda, basi yatumike kikamilifu. Waamini kwa namna ya pekee, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa, kwa kutambua kwamba, dhamana na utume wao unajikita katika huduma ya upatanisho, haki na amani. Wanaalikwa kuendelea kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji Mpya.








All the contents on this site are copyrighted ©.