2012-10-24 09:13:47

Bara la Afrika ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwani mazingira yamebadilika hali inayohitaji mbinu mpya zaidi za Uinjilishaji!


Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM anasema, Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya inayoendelea hapa mjini Vatican ni jitihada mpya za Mama Kanisa katika kurithisha imani katika mazingira mapya yanayohitaji mbinu mpya na za kisasa zaidi. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Kardinali Pengo anachambua Sinodi hii kama ifuatavyo. RealAudioMP3

Kwa sasa kuna mwelekeo miongoni mwa watu wa nchi zilizoendelea kwamba, dini ni kiwazo cha maendeleo na kwamba, imani ya watu linapaswa kuwa ni jambo binafsi. Bara la Afrika ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto iliyotolewa kwa mara ya kwanza na Papa Paulo wa Sita, alipolitembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika kunako mwaka 1966, changamoto hii imeendelezwa na Papa Yohane Paulo wa Pili na kwa sasa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameivalia njuga.

Bara la Afrika halina budi kuwa tayari Kuinjilisha na Kuinjilishwa kwa kupanua wigo wa Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati ili kutoa majibu muafaka kutokana na changamoto, matatizo na fursa zinazojitokeza, kwa kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya waamini wana misimamo mikali ya kidini hali ambayo wakati mwingine, inachochea kinzani, migogoro na machafuko ya kidini.

Imani ya Kikristo Barani Afrika bado haijaota mizizi ya kutosha na matokeo yake ni waamini kupata kishawishi cha kutaka kurudi au kuchanganya na tamaduni na mapokeo yao ya asili. Kisiasa, Kanisa linaangalia matukio kadhaa ambayo yamepelekea kuvunjika kwa misingi ya haki, amani na utulivu. Kuna nchi ambamo haki msingi za binadamu zinaendelea kuvurugwa kwa mafao ya wajanja wachache kwa kutumia: ukabila, udini na rangi ya mtu.

Kardinali Pengo anasema kwamba, Uinjilishaji Mpya Barani Afrika unapania kutafuta mbinu na njia muafaka ya kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; utu na heshima ya mwanadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba, mazingira yamebadilika, hivyo mbinu zinazotumika hazina budi pia kubadilika. Ikumbukwe kwamba, Uinjilishaji Mpya bado unaendelea kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka; Alfa na Omega, Nyakati zote ni zake kwa kutumia mbinu na katika mazingira mapya.







All the contents on this site are copyrighted ©.