Watoa rushwa wachukieni na washitakini ili wakione kilicho mnyoa Kanga manyoya!
Hotuba ya Rais Kikwete wakati wa hafla ya kufunga mkutano mkuu wa nane wa Umoja wa
Wanawake Tanzania, Mkoani Dodoma, tarehe 21 Oktoba 2012.
Nakushukuru sana Ndugu
Mwenyekiti kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika sherehe za kufunga Mkutano Mkuu
wa Nane wa UWT. Nawapongeza wajumbe wote wa Mkutano huo kwa kukamilisha vizuri shughuli
ya uchaguzi wa watu watakaoongoza Jumuiya yetu kwa miaka mitano ijayo.
Nakupongeza
wewe Ndugu Mwenyekiti na Makamu wako kwa kuchaguliwa tena kushika nafasi hizo za juu
kabisa za Jumuiya ya Wanawake. Pia nawapongeza wale wote waliobabatika kuchaguliwa
katika nyadhifa mbalimbali ndani ya Jumuiya yetu. Nawapongeza wale wote waliojitokeza
kugombea ambao hawakujaaliwa kuchaguliwa. Nyote nawapa pole kwa misukosuko iliyowakuta
kwani kugombea si kazi rahisi hasa siku hizi ambapo kuna mchanganyiko wa mambo mengi.
Yapo mengine yasiyopendeza hata kuyasema, kusimulia ambavyo lazima Chama chetu kiendelee
kuyapiga vita.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Uchaguzi umekamilika kilichoko mbele
yenu ninyi viongozi ni kuchukua nafasi zenu na kutimiza wajibu wenu wa kuongoza Jumuiya
ya Wanawake na wanachama wake kutekeleza wajibu na malengo yaliyofanya CCM iunde Jumuiya
hii.
Shabaha ya CCM katika kuunda Jumuiya hii ni kukiwezesha Chama kutekeleza
madhumuni yaliyotamkwa katika Ibara ya 5 ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi: Nanukuu:
“…………. kwa hiyo malengo na madhumuni ya CCM yatakuwa yafuatayo: Kushinda katika uchaguzi
wa Serikali Kuu na Mitaa, Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali
Kuu na Mitaa katika Jamhuri ya Muungano kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande wa
pili“… Kwa mujibu wa Ibara hiyo, madhumuni ya msingi ya Chama cha Mapinduzi ni kushinda
uchaguzi katika ngazi zote tangu kitongoji mpaka taifa.
Tunataka Mwenyekiti
wa Kitongoji awe wa CCM, Mwenyekiti wa Mtaa au Kijiji awe wa CCM, Serikali ya Mtaa
au Kijiji iwe ya CCM, Diwani awe wa CCM, Halmashauri iwe ya CCM, Mbunge au Mwakilishi
awe wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar wawe wa CCM, Serikali
zetu mbili ziwe za CCM. Hiyo ndiyo sababu na maana ya kuundwa na kuwepo kwa Chama
cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Hiyo pia ndiyo sababu ya kuundwa na kuwepo
kwa Jumuiya ya Wanawake, Jumuiya ya Vijana na Jumuiya ya Wazazi. Kwa vile nchi yetu
ni ya demokrasia na kwamba ushindi unapatikana kwa njia ya kupigiwa kura na wananchi.
Tunapozungumzia ushindi wa chaguzi za dola tunazungumzia kupigiwa kura na wananchi.
Tena katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ushindi huo unapatikana kwa kushindana
na vyama vingine vya siasa ambavyo idadi yake imefikia 20 pamoja na CCM.
Hivyo
tunashindania kukubaliwa na wananchi wengi zaidi kuliko wenzetu. Jumuiya za Chama
zimeundwa kuisaidia CCM kukubalika na kuungwa mkono na wananchi. Kila Jumuiya imepewa
kazi maalum ya kufanya katika jamii na Jumuiya ya wanawake imekabidhiwa kufanya kazi
hiyo miongoni mwa wanawake hapa nchini.
Ndugu Wananchi;Kwa vile sasa mmemaliza
uchaguzi jipangeni kisawasawa kutimiza wajibu wenu huo. Kazi yenu ya awali ni kujenga
Jumuiya yenu. Anzeni kwanza kabisa na kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi,
miongoni mwa viongozi na wanachama na miongoni mwa wanachama kwa wanachama. Demokrasia
ya uchaguzi ndiyo njia bora kuliko zote za kupata viongozi. Lakini, ina hatari zake
na hasa kusababisha mgawanyiko au hata mpasuko miongoni mwa viongozi na miongoni mwa
wanachama.
Kazi kubwa ya awali ya kufanya katika kujenga Jumuiya baada ya uchaguzi
ni kuziba nyufa za uchaguzi, migawanyiko na nongwa za uchaguzi. Ukomavu na ustahamilivu
unahitajika sana. Kwanza lazima mtambue kuwa kugombea ni haki ya kila mwanachama
wa Jumuiya, tena ipo kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Jumuiya kila baada ya miaka
mitano. Hivyo, hakuna sababu ya kumchukia mwanachama aliyejitokeza kugombea. Pia
si dhambi kwa mwanachama kumuunga mkono au kumpigania mgombea yeyote anayemuona yeye
anafaa.
Ukimchukia au kumuona adui mtu aliyeamua kugombea nafasi unayogombea
au kutokukuunga mkono wewe katika uchaguzi na akamuunga mkono mgombea mwenzako, wewe
utakuwa unaonyesha udhaifu wa hali ya juu wa kiuongozi. Si mwana demokrasia. Utakuwa
hutoshi, ni kiongozi usiyejiamini au unayejikweza na kupenda makuu na kuabudiwa.
Na, daima utakuwa kiongozi wa makundi na mwenye visasi. Daima Chama au Jumuiya itakuwa
na misuguano isiyoisha chini ya uongozi wako au wewe usipopata uongozi.
Ninaposema
maaneno haya nayasema kwako dada yangu Sofia na kwako dada yangu Anna. Uchaguzi umeisha
sasa mshirikiane kujenga Jumuiya. Na nyie mlioshinda ndiyo muongoze njia kuwajumuisha
wenzenu. Na, nyie mlioshindwa muwe mfano wa kuwa tayari kufanya kazi na wenzenu.
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Nisieleweke kuwa hata watenda maovu
muwapende. La hasha! Watoa rushwa wachukieni na washtakini.
Ndugu Mwenyekiti;Hatua
hizo zitasaidia sana kuleta utulivu katika Jumuiya na hivyo kuwapa nafasi ya kufanya
kazi ya msingi ya kuijenga na kuiimarisha. Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na kuingiza
wanachama wapya, kuwandaa wanachama hao wapya na wa zamani kutimiza ipasavyo majukumu
ya msingi ya Jumuiya hiyo. Pia, lipo jukumu la kuwajengea uwezo viongozi wa Jumuiya
waweze kutekeleza majukumu yao ya uongozi, kuhakikisha kuwa vikao vinafanyika, vinazungumza
mambo ya msingi na vinaendeshwa vizuri. Pia, kuijengea Jumuiya uwezo wa rasilimali
fedha na vitendea kazi.
Inatia faraja sana kuwa katika miaka mitano iliyopita,
Jumuiya yetu imetimiza vyema majukumu yake ya kujenga na kuimarisha Jumuiya hii.
Taarifa ya kazi za Jumuiya zinaonyesha kuwa wanachama wameongezeka kwa wingi wakiwemo
wasomi na vijana.
Ila hapa lazima nisema kuwa, wakati tunapitia majina ya wagombea,
wanawake wasomi hatukuwaona kwa wingi kujitokeza kugombea. Dada Sophia nilimuuliza,
naomba na nyie lazima mjiulize kwa nini? Jumuiya yetu hii muhimu ikikosa wanawake
wasomi kuchukua nafasi za uongozi miaka ijayo itakuwa vigumu sana kwa Jumuiya yetu
kufanikisha majukumu yake ya kutafuta ushindi na kufanya kazi ndani ya umma na kuipatia
CCM ushindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti; Nimefurahi pia kuona Jumuiya inafanya
jitihada kubwa kutekeleza Azimio la Halmashauri Kuu ya CCM ambalo limekiagiza Chama
na Jumuiya zake kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kuongeza kipato kwa lengo la kujitegemea.
Nafurahi kuona juhudi za uongozi unaomaliza muda wake zimeanza kuzaa matunda kwani
mapato ya Jumuiya hii sasa yameanza kuwa na mwelekeo wa matumaini. Naomba juhudi
ziongezwe maradufu ili muda si mrefu ujao Jumuiya ijitegemee na kutoa ruzuku kwa chama.
Kwa
bahati nzuri, Jumuiya ina rasilimali za kutosha, hususan majengo na viwanja kwenye
maeneo mazuri. Naomba tuzitumie rasilimali hizi vizuri kwa faida ya Jumuiya. Najua
peke yenu hamuwezi kuendeleza kila kitu mlichonacho. Simamieni vizuri utaratibu
mlioanzisha wa kuingia ubia na wawekezaji mbalimbali. Hakikisheni mnafaidika na ubia
mnaouingia. Isiwe ubia ambao anayefaidika ni mwekezaji na kiongozi au viongozi wachache
wa Jumuiya. Uwe ni ubia unaofaidisha Jumuiya na kuiwezesha kufikia malengo yake.
Ndugu
Mwenyekiti; Kukamilika kwa uchaguzi wa taifa kunahitimisha mchakato wa uchaguzi
kuanzia ngazi ya Tawi mpaka taifa. Viongozi wapya waliochaguliwa, kwa muhtasari, wamekabidhiwa
dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa yale mazuri yaliyofanywa na viongozi waliopita yanadumishwa
na mafanikio yaliyopatikana yanaendelezwa. Wasibweteke na hali ilivyo sasa, lazima
wawe wabunifu na wenye kuona mbali - visionary leaders. Wabuni mipango mipya itakayoendelea
kuimarisha Jumuiya na Chama kwa ujumla ili tuweze kuzikabili kikamilifu changamoto
zilizopo
Katika kufanya kazi ndani ya umma naomba Jumuiya yetu ijipange vizuri
kutimiza wajibu huo. Hakikisheni mna wanachama walio hai, wenye kulipia ada zao kwa
wakati, wenye kujitolea michango yao ya hali na mali kwa ajili ya kuendeleza Jumuiya.
Tembeleeni wanachama wenu mara kwa mara, muwaongoze na kuwahamasisha kukisemea
na kukitetea Chama cha Mapinduzi. Watembeleeni wanawake, kwa jumla zungumzeni nao,
fafanueni sera za Chama cha Mapinduzi. Jihusisheni na shida zao na mahitaji yao.
Jitambulisheni nao ili waone Jumuiya yetu hii ndiyo mtetezi wao na mkombozi wao.
Kwa kufanya hivyo mtaimarisha imani yao kwa UWT na kwa yule mwenye Jumuiya yake ambae
ni CCM.
Ndugu Mwenyekiti; Viongozi wapya wa UWT hawana budi kuwa na mawazo
mapya na mbinu mpya za namna ya kujenga Jumuiya kwa kuzikonga nyoyo za wanachama na
akina mama nchini. Jumuiya ikiweza kusimamia ipasavyo haki zao, itaheshimiwa na wengi;
ikitetea maslahi ya wanawake ya kijamii na kiuchumi, itakuwa kimbilio la wengi. Lazima
UWT muonekane mkiwasemea akina mama pale ambapo wengi wao hawana msemaji, itasikilizwa
na kuungwa mkono na wengi. Kwa ujumla itatumainiwa na kupendwa na wengi. Vile vile,
viongozi wanatakiwa kuwa wabunifu zaidi ili Jumuiya iendelee kuwa kiungo muhimu cha
wanawake wote wa mijini na vijijini. Iwe ni Jumuiya yenye manufaa kwa vijana na wazee,
wasiokuwa wasomi, wenye elimu ya kati na wasomi.
Kwangu mimi, hiyo ndio namna
nzuri na endelevu ya kuongeza wanachama wengi zaidi kwenye Jumuiya yenu. Mimi binafsi
nikiangalia asasi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya wanawake, hakuna kama
UWT. Hakuna taasisi yenye mtandao mpana, yenye wanachama wengi nchi nzima na uzoefu
kama UWT. Iweje leo zisikike taasisi hizo, tena baadhi yao zinaishia Dar es Salaam
badala ya UWT iliyopo nchi nzima? Hii ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa ipasavyo
na uongozi mpya.
Ndugu Mwenyekiti; Kabla sijamaliza hotuba yangu napenda
kutoa rai moja kwenu. Nawaomba mhimize viongozi na wanachama wenu wajitokeze kwa wingi
kutoa maoni yao kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba watakapotembelea maeneo
yao. Hii ni fursa adhimu kwa wanawake. Wahamasisheni wajitokeze kwa wingi kutoa maoni
yao. Huu ndio wakati wake.
Ndugu Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano
Mkuu, Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana;
Mwisho, nawashukuru tena kwa
kunialika na kunikaribisha vizuri. Nawapongeza kwa kumaliza vizuri uchaguzi na kupata
viongozi wapya wa UWT. Kupitia kwenu, nawashukuru wanawake wote wa Watanzania kwa
kuendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi na Serikali zake mbili, yaani Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Tunaahidi tutaendelea kuongeza
jitihada za kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania. Azma yetu
ipo pale pale “maisha bora kwa kila Mtanzania”
Nawatakia viongozi wote waliochaguliwa
mafanikio katika utendaji wa majukumu yao mapya. Rai yangu kwenu ni muwe na umoja,
ushirikiano na upendo. Mkifanya hivyo Jumuiya yenu itapata mafanikio na kujiletea
maendeleo ya haraka. Na, kwa wanachama na wanawake wote kwa ujumla tafadhali wapeni
viongozi wenu mliowachagua ushirikiano unaostahili. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. Kidumu
Chama Cha Mapinduzi!