2012-10-23 09:01:51

Tangazeni Injili ya Upendo, Umoja na Mshikamano wa dhati ili Kristo: afahamike, apendwe na kufuatwa!


Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya ni fursa makini ya kuyaangalia malimwengu kwa jicho la Kiinjili, hasa kutokana na ukweli kwamba, mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, utandawazi umeendelea kushika kasi ya ajabu sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kiasi kwamba, utamaduni wa watu kutafuta faida kubwa unatawala hata wakati mwingine kwa kufisha maadili, utu na heshima ya mwanadamu.

Watu wengi wanaendelea kuathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na myumbo wa uchumi kimataifa. Tunu msingi za maadili na utu wema zimeendelea kumong’onyoka siku hadi siku. Zote hizi ni changamoto ambazo Mama Kanisa anapaswa kuzifanyia kazi katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, ili Mwanga na Tunu za Kiinjili ziweze kuyakoleza malimwengu.

Mwaliko wa Mama Kanisa kwa wakati huu ni: kutubu na kuiamini Injili ili kukumbatia utakatifu wa maisha, tayari kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Waamini wanapaswa kujitahidi kuhakikisha kwamba, wanakutana na Yesu kwa njia ya: Tafakari ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma, kielelezo makini cha Umwilishaji wa Injili kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Waamini wanapaswa kutangaza Injili ya Ukweli mfunuliwa na upendo, inayojikita katika maisha ya Kisakramenti na kwamba, Waamini wanapaswa kuthamini na kukoleza umoja na mshikamano wa Familia ya Mungu inayowajibika. Jumapili iwe ni siku maalum kabisa kwa waamini kuonesha imani yao kwani hii: ni Siku ya Mungu; Siku ya Kristo, Siku ya Kanisa, Siku ya Mwanadamu na Siku ya Mambo ya Nyakati.

Umoja na ushuhuda ni mambo ambayo yanapaswa kupewa msukumu wa pekee hasa katika ulimwengu mamboleo wanasema Mababa wa Sinodi uliogubikwa na ubinafsi, uchoyo na tamaa ya kupenda sifa kupindukia. Uhusiano huu unapaswa pia kujionesha kwa namna ya pekee kati ya Watawa wanaoshiriki katika utume na maisha ya Makanisa mahalia; wote wajisikie kwamba, wanayo dhamana ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa kushirikisha karama na utume wa Mashirika husika.

Mababa wa Sinodi wanasema, inasikitisha kuona kwamba, idadi ya miito ya kitawa inaendelea kupungua Ulaya na Marekani, ingawa kuna ongezeko kubwa la miito hii Afrika na Asia. Lakini, wanakumbusha pia kwamba, kuna wimbi kubwa la watawa wanaoacha wito wao kutokana na sababu mbali mbali, lakini kubwa kabisa ni kwamba, kuna baadhi yao wanajisikia wakavu katika maisha yao ya kiroho na mahusiano katika Jumuiya zao.

Huu ni mwaliko kwa Jumuiya za Kitawa kujenga na kuimarisha utamaduni wa kusikilizana na kushirikishana, yale yaliyofichika katika undani wa mtawa mwenyewe, ili watawa ambao kwa miaka mingi wamekuwa ni sauti ya kinabii, waendelee kutekeleza dhamana, wajibu na wito wao ndani ya Kanisa na Jamii pasi ya kukata tamaa au kujutia uamuzi wao kuhusiana na maisha ya kitawa.

Ikumbukwe kwamba, watawa ni rasilimali watu kubwa, ambayo ikitumiwa kwa umakini mkubwa itasaidia sehemu kubwa ya Uinjilishaji Mpya kwa kumwilisha Injili ya Upendo kwa kushirikisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu. Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa linahitaji ushuhuda wa Watawa sehemu mbali mbali za dunia.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanaendelea kuwahimiza Waamini walei kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mwanga na chumvi ya ulimwengu kwa kushiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; changamoto inayokwenda sambamba na majiundo makini na endelevu kwa waamini walei. Makleri na Waamini walei washirikiane kwa dhati kabisa ili Habari Njema ya Wokovu iweze kuwafikia watu wengi zaidi, utume ambao unapaswa kutekelezwa kwa namna ya pekee katika maisha ya Kiparokia.

Hapa ni mahali ambapo Kanisa mahalia linapaswa kuonesha ushuhuda wa maisha na utume wake. Ni mahali ambapo waamini wanapaswa kuonja ile furaha ya Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini wajisikie kuwa ni wadau wakuu katika Uinjilishaji Mpya, wanapotekeleza mikakati mbali mbali ya maisha na utume wa Kanisa mahalia.

Hapa ndipo watoto, vijana na watu wazima wanapaswa kujichotea utajiri wa Imani inayoungamwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya Nyakati; Imani inayoadhimishwa katika Sakramenti mbali mbali za Kanisa, chemchemi ya neema na wokovu; Imani inayomwilishwa kwa njia ya matendo na utu wema unaobubujika kutoka katika Amri za Mungu na hatimaye, ni Imani inayojionesha katika maisha ya Sala.

Familia ya Mungu inachangamotishwa na Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, wanajikita katika azma hii bila ya kujibakiza hata kidogo. Hii pia ni changamoto endelevu kwa Vyama vya Kitume kuhakikisha kwamba, vinashirikisha malengo ya vyama vyao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Haya ni matunda ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa.

Katika Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, Kanisa linaendelea kusherehekea matukio mbali mbali ya hija ya Imani ya Kanisa katika ujumla wake. Tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Waamini sehemu mbali mbali za dunia wameendelea kukabiliana na nyanyaso na madhulumu yanayojikita katika Imani, kama inavyojionesha huko Mashariki ya Kati, Asia na Barani Afrika.

Hii inaonesha kwamba, bado kuna haja ya kukuza na kukoleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ili kujenga msingi unaoheshimu na kuthamini tofauti za kidini zinazojitokeza ambao kimsingi ni utajiri wa Watu wa Mungu.

Mababa wa Sinodi wanawachangamotisha waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahdi kumwilisha Injili ya Ukweli na Upendo katika hija ya maisha yao ya kila siku ili watu waonje kwa mara nyingine tena, upendo na huruma ya Kristo. Watakatifu saba waliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wawe ni vielelezo makini vya umwilishaji wa Injili ya Ukweli na Upendo kati ya watu.

Ushuhuda wa maisha ni jambo msingi sana katika azma ya Uinjilishaji Mpya inayohitaji Waamini walioandaliwa barabara. Kazi hii inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kuanzia ndani ya Familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, Parokia na kwa namna ya pekee, kwenye Seminari na Nyumba za Malezi. Watu wajifunze kutafakari nakujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini kwa njia ya Ukimya ili kugundua Mwenyezi Mungu anataka nini kutoka katika undani wa maisha yao.

Mshikamano na umoja wa Kikanisa umefanikisha mipango mingi ya shughuli za Kimissionari sehemu mbali mbali za dunia. Vijana waendeleee kujengewa uwezo pamoja na kuhamasishwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Walijitahidi kulifahamu Neno la Mungu, Mafundisho Jamii ya Kanisa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.

Mababa wa Sinodi wanaalika Waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusoma alama za nyakati, kwa kutorudia makosa yaliyofanywa na Wainjilishaji kwa nyakati mbali mbali hali ambayo imepelekea ukakasi katika maisha na utume wa Kanisa; kinzani na migongano na hata wakati mwingine Kanisa likashindwa kueleweka. Kamwe dini isichanganywe na mambo ya kisiasa.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yawajengee waamini uwezo wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima yake; wajitahidi kutafuta mafao ya wengi ndani ya Jamii sanjari na kujenga umoja na mshikamano wa dhati miongoni mwa Familia ya Mungu. Katiba za nchi ziandaliwe kwa umakini mkubwa kwani hii ni Sheria Mama. Kwa pamoja wajitahidi kuyatakatifuza malimwengu kwa kuondokana na vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhilifu wa mali ya umma. Kwa njia hii, Serikali na Kanisa vinaweza kushirikiana kwa ajili ya mafao ya wananchi wao.

Kamwe, Kanisa lisinyamaze kutetea haki msingi za binadamu, utu, heshima na maadili mema. Lakini ikumbukwe kwamba, Kanisa litaweza kufanikiwa katika azma hii, ikiwa kama litaendelea kuwa aminifu kwa Kristo mwenyewe, daima likitafuta utakatifu wa maisha, likisimamia misingi ya ukweli na uwazi katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Kanisa lijitahidi kuwaongoza watu wanaotafuta ukweli wa Kiinjili, ili hatimaye, waweze kukutana na Kristo Mfufuka.








All the contents on this site are copyrighted ©.