2012-10-23 14:09:05

Mwongozo wa uhamasishaji wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania


Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, imekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanashiriki katika kutoa maoni yao, jambo ambalo linaungwa mkono na Maaskofu mbali mbali. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha Mwongozo huu kama changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Maaskofu walipokutana na Jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki Roma.
MCHAKATO WA MABADILIKO YA KATIBA
Mwongozo wa uhamasishaji
UTANGULIZI
Ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania wananchi kushirikishwa katika kuandika Katiba ya nchi. Ni fursa ya pekee, kwa hiyo inatupasa kuitumia vizuri ili kupata Katiba nzuri itakayoweza kuongoza Taifa letu kwa kadiri ya mpango wa Mwenyezi Mungu. Ni wajibu wetu sote, na ikiwa hatutautimiza, tuelewe tunawaachia wengine ambao kwa nia mbaya ama kwa kutoelewa watatumia nafasi hiyo kusukuma mambo ambayo yanaweza kuathiri vikali misingi mikuu ya taifa letu ambayo ni umoja, mshikamano, maelewano, utulivu, udugu na amani. Kila siku tunamwomba Mungu adumishe amani katika Taifa letu. Hii ni nafasi ya kipekee ya kutekeleza kwa matendo wajibu wetu kushiriki kupatikana kwa mwongozo au “muundombinu” thabiti wa jinsi Taifa letu litakavyoongozwa na kutawaliwa ili kuhakikisha viashiria vya uvunjifu wa amani, kama kero kuu za wananchi, vinathibitiwa kwa ufanisi zaidi. Kwa hiyo kila mmoja ajione ana wajibu huo, aupokee na kuutimiza bila kusitasita.
I. KANUNI MSINGI
    Kujitambua sisi ni nani katika Tanzania

Sisi ni raia na pia Wakristo Wakatoliki. Ukristo wetu utuongoze tuweze kuwa raia wema ikiwa ni pamoja na kushiriki mchakato huu wa kuandika Katiba. Ushiriki wetu uwekee mkazo kanuni za Mafundisho ya Kanisa kuhusu Jamii. Kanuni hizo ni kujali utu wa kila mtu, upendo, kushughulikia manufaa na ustawi wa wote hasa wanyonge na Mshikamano.

    Maana ya Katiba

Ni makubaliano ya wananchi kwa pamoja juu ya namna ya kuongoza maisha yao kama Taifa na hasa jinsi wanavyotaka kutawaliwa. Katiba huainisha haki na wajibu kwa kila mmoja – raia na viongozi na kuweka vyombo vya kusimamia utekelezaji. Ni chombo kitakatifu kinachotusaidia kuishi vizuri tukiongozwa na maadili mema na hivyo kuthihirisha maisha yenye kuonyesha upendo kwa Mungu na kwa jirani.

    Kwa nini tunahitaji mabadiliko ya Katiba?

Wananchi wameonyesha wazi kutaka mabadiliko ambayo yataweza kujibu kero na changamoto zinazowakabili katika maisha yao na kama Taifa. Hasa changamoto ambazo zimeonekana hazina ufumbuzi katika mfumo wa utawala uliopo na zinaelekea kukatisha tamaa wananchi walio wengi. Alama za nyakati zinaonyesha hasira ya jamii kwa sababu wanaona mambo mengi hayaendi vizuri. Ni kwa hiyo tunataka Katiba itakayoweza kuleta mabadiliko hayo, kwa kujibu kero na changamoto ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya watanzania wengi na pia kuathiri tunu ya amani katika nchi yetu.
    Katiba inaainisha mamlaka ya wananchi, na kwa hiyo haitoshi tu kuwa na Katiba nzuri. Ni lazima pia iwe Katiba inayotekelezwa katika maisha ya kila siku ya raia na Taifa. Ikiwa inatokea ukiukwaji, basi mfumo uwepo wa kulazimisha Katiba kutekelezeka.


II. MAONI YA KUONGOZA MCHANGO WETU KATIKA KUANDIKA KATIBA
Nia ya maoni haya ni kusaidia waumini wetu kutafakari na kupata uelewa na hivyo kuweza kutoa maoni makini kwa faida ya jamii yetu na Taifa letu. Moni haya yamejikita hasa katika changamoto zifuatayo:
    Rushwa na ufisadi

Tukumbuke Rushwa nia adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa. Hadi sasa miaka hamsini ya uhuru wetu tunaona rushwa inazidi kukua na kuenea. Na imejikita pia hadi kwenye vyombo vikuu vya utawala (polisi, mahakama, serikali na bunge) na inaelekea vigumu kuidhibiti. Tatizo hili kongwe linahusu jamii nzima – kushiriki kwa kutoa au kupokea ama kufumbia macho. Matokeo yake rushwa na ufisadi imetuathiri sote kama wananchi na kama Taifa. Tutoe maoni yetu kuonyesha ni namna gani tatizo hili linaweza kutatuliwa kisheria na kijamii. Tutazame upya jinsi ya kuimarisha vipengele vya kudhibiti ukiukwaji wa maadili kwa viongozi na pia kuona kama TAKUKURU kama ni chombo huru na chenye meno kisheria.

    Mgawanyo wa mali na rasilimali za nchi

Hizi ni pamoja na ardhi, madini, mafuta/gesi, misitu, mbuga za wanyama, bahari, maziwa na mito, bila kusahau mfuko wa taifa (hazina). Utajiri huu ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi wa Watanzania wote kwa vizazi na vizazi. Hali ilivyo sasa ni tofauti na azma hiyo. Wachache wamejilimbikizia na wengi wanaendelea kuishi maisha duni, kumekuwa na mgawanyo wa matabaka ya wenye nacho na wasio nacho. Kijumla wanyonge wametupwa pembeni katika maendeleo ya kiuchumi. Wawekezaji kutoka nje wanapewa kipaumbele dhidi ya wananchi kwa njia ya mikataba kusainiwa katika usiri mkubwa. Mwelekeo huu unahatarisha amani na hadi sasa kumekuwa na matukio mengi ya uvunjifu wa amani katika jitihada za wananchi kujaribu kutetea maslahi yao. Katiba iweke namna ya kuhakikisha wananchi wote wanashiriki katika kutumia rasilimali zetu kwa maendeleo ya wote na kuzitunza kwa ajili ya vizazi vijavyo.

    Uwajibikaji : raia na viongozi kwa ngazi na makundi yote

Kadiri siku zinavyokwenda moyo wa uwajibikaji unaendelea kufifia tangu ngazi ya familia. Jamii inakosa kushikamana katika kujiletea maendeleo na ustawi na hata huharibu miundombinu iliyowekwa kwa ajili yao. Viongozi wanakiuka maadili na kuliingizia Taifa hasara kubwa na bado hakuna kuwajibika ama kuwajibishwa. Kwa hiyo tunaona mfumo wa uwajibikaji kijumla sio mzuri. Katiba iweke taratibu wa kung’olewa madarakani kwa sababu ya kutowajibika, iimarishe njia za kudhibiti madaraka (checks and balance), bunge liwe kweli mwakilishi wa wananchi na mijadala yake iongozwe katika hali ya kuruhusu maoni mbadala na kuyaheshimu. Raia wasibaki katika kulalamika tu, bali waonyeshe mamlaka yao na nguvu yao katika suala zima la uwajibilkaji.

    Vyombo vya kusimamia na kutoa haki

Hapa tulenge mahakama na polisi. Vyombo hivi vimeshindwa kufikia matarajio ya wananchi. Zaidi vimekuwa upande wa wenye fedha na madaraka na kwa wananchi wa kawaida na hasa wanyonge imekuwa ni vigumu mno kupata haki zao. Kwa upande mwingine wananchi nao wanashiriki kuvifanya vyombo hivi vishindwe kutimiza majukumu ya uwepo wake mfano kwa njia ya kushiriki rushwa, wakati mwingine ikiambatana na kubambikiza kesi, polisi kutesa na kudhalilisha, kuchelewesha mno kesi na pengine hukumu ikitoka kuonyesha kuwa mhabusu hakuwa na kosa nk. Katiba iwezeshe vyombo hivi kuwa huru na hivyo kutenda haki sawa kwa wote badala ya kuegemea upande fulani.

    Uteuzi wa viongozi

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa Rais ana madaraka makubwa mno. Vigezo vinavyotumika haviko wazi na mara kadhaa imeonekana wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa sababu wamepewa kazi ambayo hawana uwezo nayo. Hata inapodhihirika hivyo bado imekuwa vigumu mno kuwaondoa madarakani. Vigezo vya kidini na kinasaba pia vimekuwa vikilalamikiwa kuwa vinatumika. Kwa mteuliwa husukumwa kutumikia matakwa ya aliyemteua badala ya kuwa mtumishi wa wananchi. Katiba ijibu changamoto hii kwa kuweka sifa na vigezo kadiri ya mahitaji ya nafasi husika na pia njia ya kuwajibisha. Uteuzi usibaki kwa mtu mmoja bali ufanyike kwa njia shirikishi kupitia Tume huru.

    Huduma bora za jamii na haki za binadamu

Haki hizi ni pamoja na huduma za afya, elimu, maji, miundombinu nk. Haki hizi zaweza kulenga mtu mmoja mmoja , makundi maalum kama vile walemavu, wazee na maskini ama jamii nzima. Kutimiza haki hizi serikali na wananchi wote wanawajibika kila mmoja kwa nafasi na kiwango chake. Haki hizi ziainishwe katika Katiba na Katiba ihakikishe zinatekelezeka kisheria.

    Ukubwa wa serikali

Tunaweza kuwa na serikali ndogo ambayo inafanya kazi kwa ufanisi. Hapa tuangalie idadi ya wizara na mawaziri, na hata mgawanyo wa mikoa na wilaya. Tunaweza kupunguza gharama za uendeshaji kwa kupunguza maeneo haya na hivyo kuweza kuongeza fungu katika bajeti ya maendeleo na mahitaji mengine muhimu ambayo tunakwama kuyagharamia. Katiba iainishe hayo isiwe ni matakwa ya kila awamu ya uongozi.

    Ukubwa wa bunge

Kwa nia hiyo hiyo ya kupunguza gharama inafaa kuangalia upya nafasi za ubunge wa kuteuliwa na wa viti maalum. Kimsingi mbunge ni mwakilishi wa wananchi ambao wanaweza kumwajibisha, na aelewe anabeba dhamana kubwa na anapaswa kuchapa kazi kwa umahiri na weledi.

    Mgawanyo wa madaraka

Hii ni kanuni msingi ya demokrasia na utawala bora. Kibinadamu ni jambo msingi kwa sababu inatoa nafasi ya kusahihishana na hivyo kukabiliana na madhaifu ya kimaumbile. Mihimili mikuu ya dola – bunge, mahakama na serikali yapasa vifanye kazi kwa uwajibikaji na kuwajibishana na sio katika mwingiliano. Kwa hali ilivyo sasa tunaona kuna mwingiliano mkubwa na hata tunaona serikali hukimbilia mahakama (isiyo huru) kama kichaka kuficha udhaifu katika utendaji wa majukumu yake, hasa kukwepa kutimiza haki za watu. Kwa namna hii utawala wa sheria unakuwa mgumu kudhihirika. Katiba iimarishe kanuni hii kwa kutoruhusu wabunge kuwa mawaziri, majaji kutoteuliwa na Rais nk. Wananchi wapewe uwezo wa kudhibiti mihimili ya dola kwa kuweka Mahakama ya Katiba kupeleka mashauri yao pale wanapoona kuna ukiukwaji wa Katiba katika utekelezaji wa majukumu yao.

    Madaraka ya Rais

Madaraka ya uteuzi wa viongozi wa juu yana wigo mpana mno unaoingilia mihimili mingine ya dola - jaji mkuu na majaji na wabunge wa kuteuliwa. Vile vile huteua mkuu wa Jeshi la polisi, wakuu wa mikoa na wilaya nk. Pia ana mamlaka ya kusamehe wafungwa, kuvunja bunge na baraza la mawaziri nk. Madaraka haya yanaweza kutumiwa vibaya, na pia uwajibikaji kwa wateuliwa hao kwa wananchi unakuwa mdogo. Madaraka haya yapunguzwe na/ama yadhibitiwe. Vigezo viwe wazi na uamuzi ufikiwe kwa njia shirikishi.

    Tume huru ya uchaguzi na Tume nyinginezo

Kwa sababu inaundwa kwa njia ya uteuzi bila vigezo kuwekwa wazi, wananchi wengi wamekosa imani nayo, na malalamiko yamekuwa mengi. Uundwaji wa Tume zetu ufanyike kwa uwazi na iliyo shirikishi.

    Dhana ya kuwa Serikali haina dini (Secularity of the State)

Msingi huu ndio nguzo ya umoja na amani katika nchi yetu. Ifafanuliwe na kusimamiwa kikatiba ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka katika uhuru wa kuabudu kwa kuwa tumeshaona unatumika vibaya kama vile kuleta mgawanyiko na mtikisiko katika familia, kufanya mihadhara ya kukashifu dini nyingine, kuharibu mali za wengine na kusababisha uvunjifu wa amani. Vile vile msukumo wa kuanzisha mahakama ya kadhi ndani ya mfumo wa mahakama za nchi siyo haki kwa hiyo isiwemo katika Katiba kwa kuwa ni mambo ya kidini na huenda ni njia ya kuifikisha nchi yetu katika kukiuka dhana ya kuwa serikali yetu haina dini.


    Muungano

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Katiba ya Muungano imevunjwa, wakati huo huo msukumo wa watu kutaka Muungano uangaliwe upya una hoja zenye nguvu. Tutoe maoni yetu tukizingatia sababu za waasisi wa muungano, na pia faida na hasara za muungano kwa wakati huu. Mapendekezo ya kutambua Tanganyika kama nchi yametambuliwa na Katiba ya sasa ya Zanzibar, kwa hiyo wazo la kuwa na Muungano wenye Serikali tatu ni hoja ambayo tunaweza kutolea maoni yetu.

    Haki ya kuishi

Kwetu sisi Wakatoliki ni jambo la kupigania kwa nguvu zote Katiba iweze kulinda uhai tangu kutungwa mimba. Vile vile tunaweza kutoa maoni yetu juu ya adhabu ya kifo. Hapa tuna wajibu wa pekee kabisa kutoka imani yetu inayotufundisha kwamba mwenye mamlaka ya kutoa uhai na kuutwaa ni Mungu Mwenyewe.

    Umiliki ardhi

Haki ya watu wa Tanzania Visiwani kumiliki ardhi ya Bara ifutwe kama ilivyo kwa watu kutoka Tanzania Bara kutoweza kumiliki ardhi huko Visiwani.

    Kubadilisha Katiba

Iwe wazi kutoruhusu Bunge kurekebisha Katiba kadiri ya matakwa yao. Mabadiliko yafanyike kwa ridhaa ya wananchi. Hapa tunaweza kubainisha na kuainisha mambo ambayo hayawezi kuguswa kabisa na Bunge. Vipengele hivyo msingi katika Katiba vibadilishwe tu na wananchi kwa kura ya maoni. Vipengele vingine ambavyo siyo vya msingi viruhusiwe kubadilishwa na bunge kwa kura si chini ya theluthi mbili. (Ila hii itawezekana tu kama Katiba itawapa wananchi uwezo wa kuwawajibisha wabunge wao kwa kuwaondosha au “recall” wasiporidhika na uwakilishi wao).

    Mgombea huru/ binafsi

Ni vema kuruhusu ili kuwezesha wale ambao hawapendi kujiunga na vyama waweze kuwa na haki ya kugombea nafasi za urais, ubunge na udiwani. Hii itasaidia pia viongozi hawa kuwajibika zaidi na kwa wananchi badala ya kujali zaidi maslahi ya chama kama ambavyo imeonekana. Itazuia chuki na uhasama ndani ya vyama kumwondoa mbunge ambaye ni chaguo la wananchi na wanampenda.

    Vyama vya siasa

Ni muhimu sheria ya kuanzisha na kuendesha vyama vya siasa ishinikize vyama vyenye kukubalika na kuwakilisha wananchi kwa kuzingatia umoja wa Taifa na kupiga vita ubaguzi wa ukabila, dini au makundi mangine yoyote. Vilevile kuwe na vigezo vya vyama kukubalika na wananchi kwa kiasi cha upeo utakaokubalika. Na pia kuwe na mwongozo kuhusu matumizi na vyanzo vya mapato ya vyama vya siasa kwa ajili ya kudhibiti rushwa na kutekwa na matajiri.



    Muundo wa maeneo ya uwakilishi

Maeneo haya – mikoa, wilaya na majimbo yagawanywe kwa kuzingatia vigezo wazi – idadi ya watu, ukubwa wa eneo na hata rasilimali zilizopo. Ugawaji wa bajeti uwe wa kuwezesha pia kuleta maendeleo kiuwiano kwa maeneo mbalimbali ya nchi ili kusiwe na tofauti kubwa ya maendeleo baina ya kanda au maeneo mbalimbali ya nchi. Wazo hili linakuwa wazi zaidi tunapoangalia mgawanyo baina ya Bara na Visiwani.

    Kumwondoa mbunge madarakani kabla ya muda kuisha

Ili kuhimiza uwajibikaji kwa wananchi, Katiba iwape wananchi uwezo na utaratibu wa kumwondoa mbunge wao madarakani ikiwa wamethibitisha kuwa hawafai (kwa mfano kulingana na michango yake na kura zake bungeni kama zina tija kwa wananchi anaowawakilisha).

    Elimu na ukomo wa ubunge

Kipindi cha ubunge kiwe na ukomo wa vipindi viwili, na pia nafasi hiyo igombewe na wenye elimu isiyopungua kidato cha sita. Kazi hiyo ina majukumu makubwa yanayohitaji upeo na uelewa na uwezo wa kusoma na kutafiti masuala mengi.

    Kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais, kinga ya Rais kushtakiwa

Fursa hii iwekwe ili kumsaidia mtu kujibidisha katika uadilifu na uwajibikaji tangu aingiapo madarakani hadi anapotoka. Kuhoji matokeo inasaidia kuondoa manung’uniko ya wale walioshindwa na kurejeshea wananchi imani kwa aliyeshinda.

    Baraza la Wazee

Kuwe na Baraza la Wazee lenye uwakilishi wa Kanda za kimila (cultural zones) na Taasisi mbali mbali zinazosimamia maadili (kama za dini). Baraza liwe pia na uwakilishi wa sehemu za jamii kama wanaume na wanawake na liwe la kushauri na kuamua au kuafiki kuhusu mambo muhimu yanayohusu maadili, mila na uhai wa Taifa. (Vilevile ikiwa nchi imeingia vitani liweze kuafiki kama iendelee na vita au la).

III. NAMNA YA KUSHIRIKI MCHAKATO
Lazima kujiandaa vizuri kwa kusoma nyaraka muhimu, kuzitafakari kwa muktadha wa maisha yetu kama Watanzania ili tuweze kutoa maoni yenye hoja nzito. Tuongeze mwamko wetu na tujitokeze kwa wingi na kutoa maoni yetu. Mpango Tume una hatua hizi:
    Kuundwa Tume
    Utoaji wa elimu kwa umma
    Kukusanya maoni

Kazi hii imekwishaanza. Katika kila mkoa vinawekwa vituo vya mikutano hiyo. Tunaweza kutoa maoni kwa kujieleza ama kwa kuandika. Ikiwa unashindwa kufika mkutanoni, basi andika na kupeleka Tume au kutuma kwa njia ya posta au barua pepe. Maoni yanaweza kuwa ya mtu mmoja ama ya kikundi.
    Kufanya majumuisho na uchambuzi

Tume itaweka maoni ya watu pamoja. Maoni yaliyotajwa na kuelezewa vizuri na wengi yatapewa uzito
    Uandikaji wa Rasimu ya Katiba
    Rasimu kujadiliwa katika Mabaraza ya Katiba. Kurudisha majumulisho kwa watu kupitia Mabaraza ya Katiba
    Urutubishaji / uboreshaji wa Rasimu baada ya michango ya Mabaraza ya Katiba


    Bunge la Katiba kuijadili Rasimu
    Kura ya maoni
    Kuanza kutumika kwa Katiba mpya


Mwisho : Ikiwa itakosa kupitishwa kwa 50% mara ya kwanza kura itarudiwa. 50% ikikosekana tena, basi tutaendelea kutumia Katiba ya sasa hadi mchakato mwingine utakapoandaliwa.









All the contents on this site are copyrighted ©.