2012-10-23 09:48:08

Jimbo Katoliki Mbeya katika harakati za maboresho ya huduma ya Afya Wilayani Igongwe


Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya, hivi karibuni amehoji sababu inayokwamisha Serikali ya Mkoa wa Mbeya kutoa ardhi kwa ajili ya kujenga Chuo cha Wauguzi katika Hospitali ya Igogwe mchakato ambao umeanza tangu mwaka 1992 bila mafanikio.

Askofu Chengula alisema katika miaka ya hivi karibuni wafadhili walio wengi wamesitisha misaada kwa asilimia kubwa kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa. Kumbe, ni bahati ya pekee kupata wafadhili wenye nia ya kutaka kuwajengea Chuo ambacho kitaisaidia Serikali ya Tanzania na wananchi kwa ujumla kwa kuongeza wataalamu wa kutoa huduma katika Zahanati na vituo vya afya kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya wananchi wa Tanzania

Akizungumza katika Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kufunguliwa kwa Hospitali ya Teule ya Wilaya ya Igogwe inayomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya mwaka 1962, Askofu Chengula alisema, kilio chake kikubwa kwa mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Abbas Kandoro ni kupata uwanja wa ekari nne unaohitajika kwa ajili ya kujenga Chuo cha Uuguzi.

Alisema leo hii wafadhili wamekata mawasiliano ya kutoa misaada na waliobakia wanaendelea kutoa kidogo walicho nacho kutokana na mioyo yao mizuri, hivyo ni nafasi ya pekee kuwaombea wafadhili hao waliobakia kutoka barani Ulaya ili mwenyezi mungu aendelee kuwapa afya na uzima.
"Lakini tunashangaa tumezuiliwa na watu wenye mioyo iliyoganda wasio kuwa na mapendo na wenzao wanaoumia, kwa nini tusiwe na mshikamano wa kuwasaidia watoto wa Nchi hii. Jubilei hii iwatie moyo tumtegemee Mungu. Serikali kwa nini tusishirikiane kuunganisha nguvu katika huduma tunayotaka kupatiwa na watu wa mbali?,"alihoji Askofu.

Askofu Chengula alisema Kanisa limeomba tangu muda mrefu ardhi ya kufanyia kazi kwa ajili ya kuwasaidia watanzania wote bila kujali: imani, itikadi wala kabila kwa kuwajengea shule itakayoziba pengo la uhaba wa wauguzi na haiombi fedha, lakini bado kumekuwa na ubabaishaji na kuzungushwa hali ambayo inaweza kuwafanya wafadhili waliotaka kutoa misaada kukataa tamaa.

"Neema inapita wala haisubiri, ugumu unatoka wapi? Barabara ndiyo hiyo watu hadi wavunje miguu, kama hamtaki semeni kuliko kutuambia mara mchakato, tutaangalia…mnaumba dunia?,"aliendelea kuhoji.

Hata hivyo Askofu Chengula aliwasihi Wauguzi na Madaktari wasikate tamaa bali waendelee kufanyakazi kwa bidii, juhudi na maarifa, wakitambua kwamba, wanashiriki katika utume wa Mama Kanisa unaopania kumponya mwanadamu: kiroho na kimwili.

Ameupongeza Uongozi na Wafanyakazi wa Hospitali hiyo kwa kutimiza Agizo la Sinodi ya pili ya Afrika ambapo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake “Africae Munus” Dhamana ya Afrika, anakazia umuhimu wa amani, utulivu pamoja na huduma makini kwa wagonjwa. Waguswe na mahangaiko na mateso ya wagonjwa wanaowahudumia wakitambua kwamba, kwa kufanya hivyo, wanamhudumia Kristo anayejionesha miongoni mwa maskini na wanyonge.

Katika Maadhimisho ya Jubilee hii, Wakristo mia mbili waliimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, wakiwemo: watoto, vijana na wazee na amewataka kuendelea kudumu katika imani na kufuata maadili ya Kanisa badala ya kutanga tanga toka dhehebu moja hadi jingine, dalili za myumbo wa imani.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kandoro amemwambia Askofu Chengula kulala usingizi na kuwa na amani katika suala la eneo la ukubwa wa ekari nne za uwanja kwani kuanzia jumatatu tarehe 22 Oktoba 2012 linaanza kushughulikiwa na kulikamilishwa muda siyo mrefu. Meela alisema utafiti unaonesha kuna kundi la watu katika Kijiji hicho wanaotaka kuleta siasa katika masuala ya maendeleo, lakini “washindwe na walegee” kwani Serikali haitalivumilia suala hilo linalotaka kukwamisha maendeleo ya wengi.

"Kwa mujibu wa sheria za ardhi, ardhi yote ipo chini ya Rais na kwa wilaya msimamizi ni Mkurugenzi wa wilaya na kama ardhi ya umma inatumika kwa manufaa ya umma kwa nini kuwe na kigugumizi? Serikali ina mpango wa kuweka Zahanati kila Kijiji na Vituo vya afya kila Kata, Wauguzi watatoka wapi kama siyo katika Vyuo hivyo vinavyotakwa kujengwa?," alihoji.

Amelishukuru Kanisa Katoliki kwa juhudi zake kwa kushirikiana na Serikali bega kwa bega na kwamba, hawawezi kupoteza msaada huo kwa ajili ya watu wachache wasiopenda maendeleo, na kuwa suala la barabara litaingizwa katika mpango. Tayari zaidi ya Sh.mil.60 zimetengwa kwa Wilaya ya Rungwe kwa ajili ya kuzishughulikia barabara.

"Pia nimesikia kuna tatizo la uhaba wa maji lakini niwahakikishie Serikali imeshatenga Sh.Mil.120 kwa ajili ya Mradi wa Maji Rungwe, lakini tutaendelea kuwaleta wauguzi na madaktari kuboresha huduma za Hospitali na kwa mwaka wa fedha awamu ya tatu dawa hazitapitia MSD zitakuja moja kwa moja Wilayani tutapata mgao wa dawa,"alisema.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amewaonya watu wanaochoma moto ovyo misitu na hatimaye, kuharibu mazingira na vyanzo vya maji kuwa waache mara moja kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria. Alitoa kiasi cha sh.500,000 katika mchango wa kukisaidia Kituo cha Watoto Yatima cha Igogwe ili kiweze kuendelea kutoa huduma nzuri.

Wafadhili kutoka nchini Uholanzi wanaoendelea kuisadia Hospitali hiyo na kutaka kujenga Chuo cha Wauguzi Yan Veltmann na Hans Berendsen kutoka katika Hospitali ya Medisch Spectrum Twente enshede wataendelea kutoa misaada ya vifaa na madawa. Walisema wanaelewa kwamba kuna uhitaji mkubwa wa msaada kwa ajili ya kuwasaiidia ndugu zao wa afrika kutokana na uhitaji kuongezeka siku hadi siku na wao watazidi kuongeza pale inapowezekana.









All the contents on this site are copyrighted ©.