2012-10-22 14:35:14

SALA YA KUWAOMBEA MAPADRE


Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anaendelea kuwahimiza watoto wake kuchuchumilia: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Sala ifuatayo inaweza kutumiwa na Familia ya Mungu kwa ajili ya kuwaombea Mapadre wao, ili waweze kuwa watu wema na watakatifu.

Ee Bwana Yesu Kristo. Mkombozi wetu, kwa mapendo na tamaa yako ya kutaka kulinda vema Kanisa lako, ukachagua Mapadri wawe Wachungaji na Viongozi wa roho za watu. Nakuomba sana; ubariki nia na bidii inayowapasa Mapadri wote katika kazi zao. Uwaongezee Utakatifu.

Uwatie moyo mzuri wenye mapendo makubwa kwako na roho za watu. Hivyo wakiisha kupata wenyewe Utakatifu, waweze kuwaongoza vizuri watu walio chini ya ulinzi wao, katika njia ya Utakatifu na furaha ya milele. Uwajalie neema zote za hali ya Upadri. Uwajalie ili waonyeshe kila siku ya maisha yao mfano wa kila fadhila ya mapendo na ya uaminifu katika Kanisa, kwa Baba Mtakatifu na kwa Maaskofu.

Yesu mpendelevu, uangalie kwa mapendo kazi na mateso ya Mapadri wako; ubariki na ustawishe mafundisho yao; wanapowafundisha watoto, wanapowahubiria watu, wanapowatuliza wakosefu watubu na wanapowasaidia wagonjwa na wale wanaokaribia mauti, Ee Yesu uwe pamoja nao. Uwakinge na hatari zote za roho na za mwili.

Mwokozi Yesu, ulijalie Kanisa liwe na Mapadri wengi walio Watakatifu. Uwajalie watoto na vijana wengi wasikie wito wa Upadri, uwatie furaha na Utakatifu na roho za Mapadri waliokufa uzijalie punziko la amani.

Kwa mimi mwenyewe Ee Yesu mpendelevu, naomba unijalie roho ya imani na utii mnyenyekevu ili niwaheshimu Mapadri kama Mawakili wa Mungu. Niwatii katika njia zote za wokovu wa roho yangu. Amina.








All the contents on this site are copyrighted ©.