Fadhila ya Uaminifu, Upatanisho na Msamaha ni vigezo muhimu vinavyodumisha maisha
ya ndoa na familia
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena tuendelee na tafakari yetu ya maisha
ya Ndoa na Familia leo tukazie zaidi umuhimu wa uaminifu na msamaha kama nguvu za
lazima kati ya wanandoa. Mojawapo ya ahadi
wanazopeana wana-ndoa ni ahadi ya uaminifu na upendo katika hali zote za maisha, katika
raha na taabu siku zote za maisha yao. Ahadi hizo huwapa nguvu wana-ndoa kuanza safari
yao hata kama baadaye haiko wazi lakini kwasababu wako kwenye umoja basi hupeana matumaini
wakati wote wa safari yao. Uaminifu huenda sambamba na fadhila za matumaini, ujasiri
na upendo. Uaminifu ni lazima utawaliwe pia na kujikatalia pale ambapo yanajitokeza
mazingira yanayopingana na uaminifu. Ndugu msikilizaji kama tulivyotaja hapo mwanzoni
uaminifu wa wanandoa ni ule wanaojifunza kwa Kristo. Aliyebaki mwaminifu mpaka juu
ya msalaba na hivyo akatulea wokovu. Ndugu msikilizaji Waswahili husema: “Chupa
zinapokaa pamoja hugongana, lakini pia ili miti inyoke vizuri msituni ni lazima ikwaruzane.”
Hali kadhalika wana-ndoa wanapokaa pamoja katika utofauti wa tabia zao hutofautiana
na utofauti huu ni muhimu katika ujumuiya wao. Lakini pia mapungufu hutokea na yanapotokea
dawa pekee katika mapungufu haya ni ni msamaha. Mwenyeheri Yohane Paulo II katika
mafundisho yake kwa wanandoa mwaka 1996 aliwaambia “Upendo wa kindoa ni lazima utawaliwe
na msamaha. Hakuna mapendo yasiyojua msamaha. Kila anayesamehe anafungua mlango wa
kusamehewa. Na kwa Wakristo hujifunza msamaha toka kwa Kristo aliyewasamehe sio tu
marafiki zake ila hata maadui wake pia. Tujifunze kusamehe na kusahau, kwani kukosa
na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu
wa maisha. Ndugu msikilizaji kila mmoja wetu anajua jinsi ambavyo familia nyingi
kila mahali zipo kwenye magomvi ya kudumu. Msamaha na uaminifu huhitaji sadaka kubwa
lakini faida zake ni nyingi kwa faida ya wanandoa na familia zao,kwa faida ya jamii
zima. Kwa uhakika ni dawa nzuri katika maisha ya ndoa na familia. Kutoka Studio
za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya
Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano- Roma.