Askofu Beatus Kinyaiya anabainisha baadhi ya mambo yanayotiliwa mkazo na Mababa wa
Sinodi ya Uinjilishaji Mpya hapa Vatican
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ilibahatika kukutana na Askofu Beatus Kinyaiya,
Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Sinodi ya
Uinjilishaji Mpya inayoendelea hapa mjini Vatican.
Pamoja na
mambo mengine anabainisha: Mababa wanaohudhuria, lengo, changamoto kutoka Barani Afrika
kuhusiana na dhana ya Uinjilishaji Mpya; mbinu zinazotarajiwa na Mama Kanisa katika
azma ya Uinjilishaji Mpya; umuhimu wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo pamoja na wito
wake kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.
Sinodi hii ambayo Baba Mt. Benedikto
XVI amependa ifanyike wakati huu inahudhuriwa na maaskofu 263 kutoa nchi mbali mbali
duniani. Pia inahudhuriwa na wawakilishi wa wakuu wa mashirika mbali mbali na baadhi
ya wakuu wa vyuo vikuu vya kitaalimungu hapa italia. Vile vile inahudhuriwa na wawakilisha
wa makundi mbali mali kama vile waanzilishi wa vyama vya kitume kama Neo katekumenato
na wawakilisha wa wa na familia na vijana.
Q 2. Lengo la Sinodi hii ni
nini?
Jina la sinodi hii ni Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani
ya Kikristo Lengo ni kutafuta mbinu mpya ya kufundisha imani ile le aliyotufundisha
Bwana wetu Yesu Krsitu, kwa namna ambayo itakubalika na watu wa kizazi hiki. Pia
Sinodi inalenga kuasha upya na kukazia zaidi umuhimu wa kuishi imani.
Ukitazama
historia ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican kwa mfano, ambao tumeadhimisha Jubilee
yake ya miaka 50 hivi majuzi, utaona kuwa nayo ililenga kuwasaidia watu kiroho ili
wamrudie tena Mwenyezi Mungu hasa baada ya kuporomoka kwa maadili na utu wema, kufuatia
Vita kuu ya pili ya dunia pamoja na kuenea kwa ukomunisti n.k
Kanisa la
sasa limejikuta katika hali kama hiyo; Kanisa la Ulaya na Marekani kwa mfano
Imani imefifia sana. Nyuma ya yote hayo ni watu kupenda mno malimwengu. Na hali
hii imechochewa sana na vyombo vya labari – TV, Internet, Radio, nk. Vyombo hivi vinafundisha
kuwa kila kitu ni ruksa.
Matokeo yake ni kwamba watu wanaishi na falsafa ya
kusema “ upe mwili kitu unapenda” Matokeo yake ni watu kujiingiza katika ulevi,
kutumia madama ya kulevya, kujamiiana bila kuishi katika misingi ya maisha ya ndoa
na familia. Na yote haya yanakubalika na kuonekana ni sawa. Na asiyefanya hivyo anaonekana
mshamba. Huu ni uhuru usiokuwa na mipaka wala nidhamu na utu wema.
Kwa kuwa
Kanisa linapinga mambo hayo, hawa watu ambao baadhi yao walikuwa wakristu, wanalikwepa
kanisa, hawasali tena, hawapokei tena Sakramenti, na wengine wanafikia hatua ya kukana
dini yao.
Q 3. Kwa upande wa Afrika hali ikoje?
Kwa
upande wa Afrika hali sio mbaya kama kwa wenzetu. Kanisa barani Afrika linakuwa
vizuri na lina nguvu. Watu wanahudhuria ibada na wanashiriki kwa furaha. Lakini yale
yaliyopo ulaya nayo pole pole yanakuja Afrika kwa njia ya mtandao pamoja na matumizi
ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Vijana wetu wanaona na wanaiga haraka sana kwani
wanaamini kuwa kila kinachofanyika Ulaya na Marekani ndio maendeleo. Kwa hii falsafa
ya kusema “ upe mwili kitu unapenda” inaonekana pia kwa baadhi ya viaja wetu, hasa
wanaoishi mijini.
Siku hizi tunaona jinsi tatizo la ulevi wa kupindukia likiharibu
familia nyingi. Pia madawa ya kulevya yanatumiwa na baadhi ya vijana wetu. Na kuna
watu wamejiingiza kabisa kwenye hiyo biashara kwa sababu soko lipo. Swala ya kujamiiana
nje ya ndoa nalo ni tatizo. Ndiyo maana janga la Ukimwi linazidi siku hadi siku.
Zaidi ya hayo, tuna tatizo la kuchanganya Ukristu na Upagani: dhana ya uwili
katika maisha. Kwa mfano, kama kuna tatizo la ugonjwa au kifo, baadhi ya wakristu
wanakimbilia wa waganga wa kienyeji kupiga bao ili wajue ni nani amesababisha hilo
tatizo. Au wakati wa uchaguzi baadhi ya watu wakiwemo wakrsitu huenda kwa waganga
wa kienyeji ili wasaidie kushinda. Ni mambo ya kipuuzi lakini watu, tena wasomi wanafanya.
Halafu kuna woga wa uchawi. Pia woga wa mizimu kwamba wanaweza kuwadhuru,
n.k. Kwa hiyo, kuna wakristu ambao wanaamini katika dunia mbili- dunia ya Ukristu
na dunia ya upagani. Vile vile kuna uonevu mwingi katika jamii zetu. Tunaona jinsi
akina mama, vikongwe, watoto, na walemavu wanavyonyimwa haki zao za mingi. Hamu
ya Sinodi hii ni kuona haya matatizo yanapungua na hata kuisha kabisa ili watu wote
waonje uhuru wa kuwa Waana wa Mungu na njia pekee ya kupambana nayo ni kumleta Mungu
kati yao.
Q 4. Mbinu gani mnategema kutumia katika Uinjilish Mpya ?
Mbinu
ya kwanza ni kumtegemea zaidi Roho Mtakatifu. Yeye amelitunza kanisa karne zote,
na tunaamini ataendelea kufanya hivyo. Viongozi kujitazama kwa upya. Sinodi inatuasa
sisi viongozi (Maaskofu na Mapadre) kujitahidi kuishi kile tunachowafundisha watu
ili kwa maisha yetu ya utakatifu tuwavute wengi kwa Kristu. Maisha huongea zaidi
kuliko maneno matupu
Pia lazima tujitahidi kuwa karibu zaidi na watu. Wale
mapadre ambao wanawatembelea Wakristu wao nyumba kwa nyumba wanafanikiwa zaidi katika
kueneza Neno la Mungu. Sinodi pia inawakumbusha wahubiri wote kuandaa vizuri mahubiri
yao. Wako Wakristu wanaoacha kufika Kanisani kusali kwa sababu ya baadhi ya mahubiri
yetu kutokuwa na ujumbe wa kuwafaa. Ili tuweze kuhubiri vizuri tunahitaji kusoma
na kujiandaa vya kutosha.
Sinodi pia inawakumbusha Walezi wa Seminari umuhimu
wa kuwaandaa vizuri Waseminaristi wakubwa na wadogo. Sio tu kuwajaza elimu kuhusu
taalimungu, bali wawasaidie pia kukutana na Yesu ( personal encounter) katika
maisha yao.
Kwa upande wa watawa, Sinodi hii inawakumbusha watawa kuishi wito
kwa uaminifu mkubwa kwani utakatifu wa maisha yao ndio utakaowavuta wengi kutaka
kumjua Mungu.
Kwa upande wa Waamini Walei, Sinodi inawaambia walei kuwa kwa
njia ya Ubatizo sisi sote tumeitwa kumtangaza Kristo. Kwa hiyo, wawe tayari kumtangaza
Kristo po pote wanapokuwa bila aibu. Wazazi nao wajue wana wajibu wa kuwarithisha
watoto wao imani. Wasiache kuwabatiza watoto kwa kisingizio kuwa wataamua wenyewe
mbele ya safari. Hii si sawa. Wawe tayari hata kufa mashahidi kwa ajili ya imani
yao kwa Kristo. Tangu sasa walei wajue kuwa ile namna yao ya kufikiri kuwa kazi ya
kuhubiri ni ya ma padre na makatekista kuwa si sawa.
Kwa vijana, Sinodi inawashauri
viongozi wote kuwa na utaratibu mathubuti wa kuwalea vizuri vijana katika maswala
ya imani. Vijana wote po pote pale walipo wapewe malezi ya Kikristo, iwe shuleni vyuoni
n.k. Na wale wanaoishi katika mazingira magumu, Mapadre waanzishe clubs – vikundi-
vya kuwakusanya siku za Jumapili na kuwafundisha imani, kujibu maswali yao kuhusu
maishana matarajio yao kwa siku za usoni.
Kwetu sisi sote, tunakumbushwa tena
na Sinodi ya Uinjilishaji Mpya kuwa Sala na Sakramenti na hasa Sakramenti ya Ekaristi
na Upatanisho ni muhimu sana kwa maisha yetu ya kiroho. Tupende kuzipata mara kwa
mara na kwa njia ya uchaji.
Q. 5. Sinodi imezungumza lo lote kuhusu Jumuiya
ndogo ndogo?
Sinodi ya Uinjilishaji Mpya pia imezungumzia juu ya Jumuiya
Ndogo nndogo za Kikristo. Kwa kuwa Jumuiya ndogo ndogo zimefakiwa sana Barani Afrika
katika kuwaleta watu wachache na kusali pamoja na kutafakazi Neno la Mungu kama Familia
ya Mungu inayowajibika tumesifiwa sana kwa hilo na wenzetu kutoka sehemu mbali mbali
za dunia.
Nasi tumewashauri waanze jumuiya ndogo ndogo ulaya na marekani. Baaadhi
ya sehemu wameshaanza kuiga na wanaonja sasa faida yake kama chombo muhimu cha Uinjilishaji
mpya unaopania kufufua imani.
Q 6. Mwisho, una wito gani kwa watu wote ?
Napenda
kuwakumbusha watu wote kuwa ikiwa sisi sote tutaishi maisha ya kimungu, maisha ya
uadilifu, maisha yenye kuongozwa na tunu za kikristu, maisha ya hapa duniani yatakuwa
ya haki, ya amani, utulivu na furaha kubwa.
Pili siku tutakapoondoka katika
dunia hii, kama tutakuwa tumishi kama tunavyoaswa na viongozi wetu wa dini, na kama
Sinodi hii inavyotuasa, hakika tutapata maisha ya furaha kuu yasiyo na mwisho mbinguni
kwa Baba.
Lakini kama tutaendelea na ukaidi wetu na kukumbatia yale ya kidunia
ambayo hayampi Mungu nafasi, basi siku ya mwisho tutatupwa kwenye mahangaiko makuu
yasiyo na mwisho pamoja na yule mwovu shetani.
Kwa kuishi maisha yanayotawaliwa
na Imani ya Yesu Kristu, hatupungukiwi na chochote na badala yake, tunafanya dunia
yetu iwe mahali pazuri zaidi pa kuishi na wakati huo huo, tunajiandalia mema mengi
ya kiroho mbinguni.