2012-10-20 07:54:19

Watakatifu ni Mashahidi na Wainjilishaji wakuu; changamoto kwa kila mwamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa lenye dhamana ya kuwatangaza waamini kuwa watakatifu anasema, dhamana ya Uinjilishaji Mpya inajikita kwa namna ya pekee katika: toba, wongofu wa ndani na maisha ya utakatifu na kwamba, watakatifu ni mhimili mkuu katika Uinjilishaji Mpya . Siri kubwa inayofumbatwa katika changamoto hii ni ule mwaliko kwa kila mwamini kuwa mtakatifu.

Utakatifu wa maisha ni mada inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo inayoshuhudia matukio mbali mbali yanayolenga kuimarisha imani ya Kikristo. Watakatifu wamechangia kwa kiasi kikubwa katika maisha na utume wa Kanisa, wakajitahidi kujenga maisha yao katika msingi wa tunu na kweli za Kiinjili; wakaboresha maisha yao kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa ili kuimarisha imani, matumaini na mapendo.

Ni watu waliomwilisha kwa namna ya pekee, heri za mlimani, kioo cha uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake. Hao ndio waliokuwa fukara wa kiroho, wapole, wenye mioyo safi na wenye huruma, waliosimama kidete kutetea na kulinda amani na wakati mwingine, wakakumbana na madhulumu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani kwa Kristo. Ni watu waliofanikiwa kumwilisha Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani; kwa njia ya matendo ya huruma; wakaukumbatia ubinadamu kwa upendo, amani, mshikamano na udugu wa kweli.

Kardinali Amato anasema kama sehemu ya mchango wake wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji kwamba, ndiyo maana Kalenda ya Kanisa imepambwa kila siku na majina ya watakatifu, kutoka kila upande wa dunia; watu wenye rangi, tamaduni na mapokeo mbali mbali yanayojenga Kanisa la Kristo katika mshikamano wa upendo, unaokumbatia kwa namna ya pekee, neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Watakatifu ni mashahidi amini wa Kristo na wadau wakuu katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.