Wasomi waliojikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene wapewa Tuzo la Ratzinger!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amewashukuru na kuwapongeza viongozi mbali
mbali waliofanikisha maandalizi ya Tuzo la Ratzinger, ambalo limeingia katika awamu
ya pili, linalopania kuwazawadi wasomi wanaofanya tafiti za kisayansi kuhusu kazi
mbali mbali zilizowahi kutungwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Kwa
namna ya pekee, amewashukuru Padre Daley na Professa Brague walionesha umahiri mkubwa
katika tafiti na ufundishaji, kiasi cha kushiriki maisha na utume wa Kanisa kama Padre
na Mlei, katika ulimwengu mamboleo. Wasomi hawa wawili wanaendelea kutoa mchango mkubwa
katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini, kwa njia ya tafiti za kina
kuhusu Mababa wa Kanisa, ili kuwajengea watu ari na moyo wa kulipenda Kanisa, sanjari
na kukuza moyo wa upendo na mshikamano na waamini wa Kanisa la Kiorthodox.
Baba
Mtakatifu anasema Profesa Brague ni msomi na mtaalam katika masuala ya filosofia za
dini, hususan dini ya Kiyahudi na Kiislam Nyakati za Kati. Katika maadhimisho ya Jubilee
ya miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Baba Mtakatifu anapenda kushiriki
pamoja nao Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu umuhimu wa majadiliano
ya kidini na kiekumene, utu wa mwanadamu na uhuru wa kuabudu vikipewa kipaumbele cha
kwanza.
Baba Mtakatifu anawahimiza Wasomi hawa waliobahatika kujinyakulia Tuzo
la Ratzinger kuendelea kushirikisha mang'amuzi yao katika nyanja hizi, ili kukuza
na kuendeleza majadiliano kati ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo. Anawashukuru kwa majitoleo
yao yanayojionesha katika kutafuta ukweli wa mambo kwenye lugha mbali mbali, changamoto
kwa Mama Kanisa kuendeleza ari na moyo wa kufanya tafiti za kina katika sekta ya elimu
na utamaduni.
Baba Mtakatifu anawaalika wanafunzi na wasomi mbali mbali kujihusisha
na tafiti hizi, kama ilivyojionesha nchini Poland na semina maalum itakayofanyika
hivi karibuni huko Rio de Janeiro, nchini Brazil. Washindi wa tuzo hii wameonesha
umahiri wa kuunganisha sayansi na hekima, daima mwanadamu akipewa msukumo wa pekee,
ili aweze kugundua sanaa ya kuishi vyema, kwa njia ya imani angavu inayotolewa ushuhuda
wa kweli kwa kuonesha uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Ni vyema
ikiwa kama watu watatambua kwamba Yesu ni njia ya maisha na kwamba kwa njia ya mwanga
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wasomi wanapata fursa ya kugusa akili na nyoyo za watu,
changamoto kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na dhamana ya Uinjilishaji
Mpya.