Papa anawaalika Wananchi Mashariki ya Kati kujikita katika kutafuta, kulinda na kudumisha
misingi ya amani kwa ajili ya mafao ya wengi!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameonesha masikitiko makubwa kutokana na
shambulio la kigaidi lililotokea mjini Beirut, Lebanon, Ijumaa tarehe 19 Oktoba 2012
na kupelekea watu nane kupoteza maisha yao na wengine wengi kupata majeraha.
Baba
Mtakatifu ameonesha masikitiko hayo katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali
Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Patriaki Bechara Boutros Rai wa
Kanisa la Kimaroniti. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kutoa mwaliko kwa
watu wanaoishi huko Mashariki ya Kati kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda
na kudumisha amani kwa ajili ya mafao ya wengi.