Msiendekeze "nyumba ndogo" na "vidumu" kumbukeni kwamba, Familia ina dhamana ya Kujiinjilisha
na Kuinjilishwa!
Askofu mkuu Peter Kairo wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya ni kati ya Mababa wa Sinodi ya
Maaskofu juu ya Uinjilishaji aliyeonesha kuguswa kwa namna ya pekee na matatizo na
changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii
katika ujumla wake.
Familia kwa sasa zinakabiliwa na kinzani katika tunu msingi
za maadili na utu wema. Matokeo yake ni familia nyingi zinajikuta zinasambaratika
hata katika uchanga wake; baadhi ya wanafamia wamejikuta wanaendekeza uchumba sugu
kiasi kwamba, wazo la kufunga ndoa kwao ni msamiati mgumu.
Baadhi ya ndoa
zinalega lega kutokana na kukosekana kwa uaminifu na utamaduni wa mapendo ya dhati
kiasi kwamba, upendo huu unachangiwa kwa kukumbatia dhana ya wake wengi; ukosefu wa
uaminifu kwa kuendekeza "nyumba ndogo" au "vidumu". Kutokana na uwepo wa ndoa tenge,
baadhi ya wazazi na hasa wanawake wamejikuta wakibeba jukumu kubwa la malezi pamoja
na kuziwezesha familia zao.
Askofu mkuu Kairo anasema, ingawa wanandoa ni watu
wanaopaswa kuishi kwa pamoja katika maisha yao yote hadi kifo kinapowatengenanisha,
lakini wamejikuta mara nyingi hawana maandalizi ya kutosha wala kupata majiundo endelevu
mara baada ya kufunga ndoa. Huu ni udhaifu mkubwa unaopaswa kurekebishwa mapema kama
sehemu ya Uinjilishaji Mpya, ili Familia ziweze kutekeleza wajibu na dhamana yake
kama mhimili mkuu wa Uinjilishaji ndani ya Kanisa kwa kupania kuyatakatifuza malimwengu.
Masuala
ya kiuchumi pamoja na ajira ni mambo yanayoitendea familia katika kujenga na kuimarisha
mshikamano wake wa upendo, kwani kuna baadhi ya wanandoa wanajikuta wakiishi mbali
na wenzi wao kutokana na sababu za kiuchumi au kikazi, hapa kuna hatari kwa wanandoa
"kuteleza na kuanguka majaribuni". Familia za Kikristo wakati mwingine zimeendelea
kukumbatia pia mila na desturi za makabila yao kiasi cha kupoteza utambulisho wake
wa Kikristo.
Uinjilishaji Mpya uziwezeshe Familia kujenga na kuimarisha utamaduni
wa upendo, sanaa ya kusikilizana na kushirikishana, kwa kutambua kwamba, wao ni sehemu
nyeti ya maisha na utume wa Kanisa, inayopaswa kupendwa, kuthaminiwa na kuendelezwa.
Wakristo wafahamu maana ya ndoa ya Kikristo kadiri ya mpango wa Mungu, Mafundisho
ya Kanisa; Utu na Maadili mema.
Familia ni Kanisa dogo la nyumbani lenye dhamana
ya kujiinjilisha ili liweze kuiinjilisha pia. Ili utume huu uweze kukolea katika maisha
ya waamini, kuna haja ya kutubu, kuongoka na kuchuchumilia utakatifu wa maisha.