2012-10-20 18:31:46

Imani inapaswa kuwa ni kielelezo cha uaminifu kwa Mungu pamoja na Kristo na Kanisa lake


Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, huku Kanisa likisherehekea Mwaka wa Imani, Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya pamoja na Siku ya Kimissionari Duniani. RealAudioMP3

Akihojiwa na Radio Vatican, Padre Francis Bartolon, C.PP.S., Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu duniani anasema kwamba, Mtakatifu Gaspar alibahatika kuishi katika mazingira akashirikiana na baadhi ya Mapadre waliomuunga mkono katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu waliokuwa wanalega lega katika imani.

Katika Mapinduzi ya Kifaransa, alikazia umuhimu wa matumizi ya kipaji cha akili inayopaswa kupata mwanga wa Injili, ili iweze kutumika kwa ajili ya mafao ya wengi. Alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti, ambayo ilikuwa ni chakula chake cha kila siku, ikawa ni dira na mwongozo wa maisha yake ya kimissionari na kipadre. Imani kwa Mtakatifu Gaspar ilikuwa ni kielelezo cha uaminifu kwa Mungu, Kristo na Kanisa lake, kiasi kwamba, ikamjalia uwezo na utayari wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo mjini Roma na Italia katika ujumla wake.

Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar, waamini wanachangamotishwa kutambua kwamba, akili ni paji kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kuangazwa na mwanga wa Injili, ambayo kimsingi ni muhtasari wa maisha ya Yesu Kristo Mkombozi wa dunia; ujumbe wa upendo; kielelezo cha uaminifu wa Mungu ambaye anampenda na kumjali mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake. Injili ni kielelezo makini cha upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu na kati ya mwanadamu na jirani yake.







All the contents on this site are copyrighted ©.