2012-10-19 11:30:34

Sanaa na Utamaduni ni chanda na pete: Tume ya Kipapa na Utamaduni pamoja na Mambo ya Kale kuunganishwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kunako tarehe 30 Julai 2012 ametia sahihi kwenye hati ijulikanayo kwa lugha ya Kilatini Pulchritudinis Fidei inayounganisha Tume ya Kipapa ya Utamaduni na Mambo ya Kale pamoja na Baraza la Kipapa la Utamaduni ambalo kwa sasa liko chini ya uongozi wa Kardinali Gianfarnco Ravasi. Uamuzi huu utaanza kutekelezwa hapo tarehe 3 Novemba 2012.

Kuundwa kwa Tume hii yalikuwa ni matunda na changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika ile Hati ya Kichungaji inayozungumzia Kanisa Ulimwenguni, Gaudiu et Spes. Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili wakati wa uongozi wake, aliunda Taasisi mbili ambazo kimsingi zilipewa jukumu la kuendeleza majadiliano ya kina na tamaduni pamoja na sanaa zinazofumbata utajiri wa imani na maisha ya Kikristo.

Baraza la Kipapa la Utamaduni, likaundwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 20 Mei 1982 na hivyo kulitenganisha na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini lililopewa dhamana ya kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini na wale wasioamini.

Tume ya Kipapa kwa ajili ya Utamaduni na Mambo ya kale iliundwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 25 Marchi 1993. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1952 Papa Pio wa Saba alikuwa ameunda Tume kuu ya Sanaa Takatifu.

Baadaye, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, akaifanyia mabadiliko kunako tarehe 28 Juni 1988 kwa kuipatia jukumu la kuwa ni Tume ya utunzaji wa urithi wa sanaa na historia ya Kanisa na kuiweka chini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri. Baba Mtakatifu akahimiza uhusiano wa dhati kati ya Mabaraza haya kwa ajili ya mafao ya Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.