Jitoeni kuhudumia: haki, amani, upendo, mshikamano na mafao ya wengi! Kamwe msitafute
masilahi yenu binafsi!
Tunakuleteeni Habari Njema ya furaha tunapotafakari pamoja ujumbe wa Neno aliyefanyika
mwili, Mfalme wa mbingu na nchi. Ni Dominika ya 29 ya mwaka B, Neno la Mungu latualika
kuwa watumishi badala ya kutumikiwa, kuwatanguliza wengine badala ya kutangulia sisi,
ndiyo kusema kuwa na moyo wa mapendo kwa taifa la Mungu, kuwa na mapendo ya kichungaji.
Mpendwa
msikilizaji kipindi tafakari, katika dunia hii watu hupenda kuwa na madaraka, vyeo
mbalimbali, kushinda vita, mitihani na mambo kama hayo! Lakini leo tunapotafakari
Neno la Mungu tunaona jinsi Mungu anavyotualika kuwa na mtizamo tofauti na mtizamo
wa ulimwengu. Nabii Isaya katika somo la I toka sura ya 53 anatuwekea sura ya mtumishi
aliyechubuliwa uso na kuhuzunika. Jambo hili latupa changamoto kuwa wajibu wa mkristu
ni kutumika na si kutumikiwa. Mfano kamili wa jambo hili ni Yesu Kristu mjumbe wa
Agano Jipya anayejitoa maisha yake kwa ajili ya wengine pasipo kujibakiza.
Nabii
Isaya akitafakari mateso ya Bwana na jinsi gani anavyojitoa maisha yake yote, haachi
kuona matunda ya kazi hiyo ya masiha. Nabii Isaya atasema, kwa maarifa yake mtumishi
wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki, naye atayachukua maovu yao yote.
Mpendwa mwana wa Mungu kazi ya kutokomboa imetokana na mapendo ya Bwana kwa njia
ya msalaba, na hivi mwaliko kwetu ni huo, kujitoa na kutumikia kwa ajili ya kuleta
amani na upendo katika Jumuiya zetu, hata tukidaiwa sadaka kubwa, tusomavyo katika
kituo cha njia ya msalaba.
Katika somo la pili katika Barua kwa Waebrania,
mtumishi mwaminifu tuliye msikia katikia somo la kwanza ni yule ambaye anachukua mwili
wa mtumwa ili afahamu vema shida za mwanadamu aliyeingia katika hali ya utumwa kwa
sababu ya kibuli chake na kwa jinsi hiyo mtumishi huyu mwaminifu aweze kutujalia mwili
mtukufu utakaofufuliwa siku ya mwisho. Kuchukua mwili wetu maana yake anataka kukaa
nasi na kushiriki shida zetu, ndiyo namna ya kutupenda na kutuinua toka katika dhambi
zetu. Kuhani huyu pamoja na kushiriki ubinadamu wetu jambo moja tu hakushiriki nalo
ni lile la kutenda dhambi.
Mpendwa mwana wa Kanisa katika somo la Injili Mitume
wanaonesha udhaifu mkubwa juu ya madaraka, bado hawajaelewa vema nini kazi ya Masiha,
wanafikiri kuwa Masiha ni kwa ajili ya mamlaka ya kisiasa na kwa masilahi binafsi!
na kwa namna hiyo wanadai vyeo vya kisiasa badala ya vyeo vya kitume yaani kuchunga
taifa la Mungu kwa kutumika na kutumikia. Bwana akijua udhaifu huo anawakemea kwa
nguvu na kuwambia kuwa, mwenye kutaka mamlaka lazima awe mtumishi wa wote.
Ndugu
yangu mpendwa, kemeo la Bwana na mafundisho yake si kwa ajili ya mitume tu, bali kwa
mataifa na vizazi vyote, na hivi anatuambia sisi leo kuwa uongozi ni kutekeleza mapenzi
ya Mungu, yaani kujitoa kiaminifu kama Kristu alivyojitoa msalabani kwa ajili ya wengine.
Uongozi si kudai heshima wala upendeleo ambavyo hutengeneza matabaka bali ni mshikamano
na Kristu mtumishi mwaminifu.
Mpendwa ninazidi kukualika kutafakari vema tendo
la kutumikia na hasa katika mwaka huu ambapo tunaalikwa kujikita zaidi katika kuelewa
vema Imani yetu, imani iliyotendaji, imani inayodai matendo thabiti yaliyo ya wazi
na ushuhuda wa kimisionari. Basi nikuombee baraka tele za Mungu ili uzidi kuimarika
katika imani iliyojaa utumishi alama ya mapendo makamilifu kwa Mungu na kwa jirani.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya
C.PP.S.