2012-10-19 08:38:30

Familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na Vyama vya Kitume ni nyenzo msingi katika Uinjilishaji mpya na ule wa kina Barani Afrika!


Bwana Joakim Kipyego Koech ni mwamini mlei kutoka Chama cha Kitume cha Comunal and liberation, kinachotekeleza utume wake nchini Kenya. Ni kati ya Mababa wanaoishi katika Sinodi ya Uinjilishaji Mpya inayoendelea hapa mjini Vatican. RealAudioMP3

Akihojiwa na Radio Vatican anabainisha kwamba, ameguswa kwa namna ya pekee, kwa jinsi ambavyo Mababa wa Sinodi wanavyojadili kwa kina na mapana kuhusu mustakabali wa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni kwa kuonesha matumaini makubwa licha ya matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza.

Anasema, mkazo wa Mababa wa Sinodi kuhusu Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Vyama vya Kitume pamoja na Familia unaonesha dhamana kubwa ambayo waamini wanatakiwa kuitekeleza katika maisha na utume wa Kanisa, wakati wa mchakato mzima wa Uinjilishaji mpya na ule wa kina kwa Familia ya Mungu Barani Afrika.

Waamini walei kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa na Jamii kwa ujumla wake, wajibidishe kukuza, kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili hata watoto na vijana ndani ya Familia zao waonje kweli uwepo wa Mungu ambaye ni upendo. Ni mwaliko na changamoto ya kukazia malezi ya awali na endelevu kwa waamini walei, ili watambue dhamana na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.