UJUMBE WA BABA MTAKATIFU BENEDIKTO XVI KWA SIKU YA KIMISSIONARI DUNIANI, 2012
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa maadhimisho ya Siku ya Kimissionari
Duniani, itakayoadhimishwa hapo tarehe 21 Oktoba, 2012, unaongozwa na kauli mbiu “Mwaliko
wa kusambaza Neno la Ukweli”.Kutujuvya zaidi kutoka Studio za Radio Vatican ni Padre
Agapito Mhando.
Hili ni jukumu
la kila Mkristo. Maadhimisho ya Siku ya Kimissionari kwa mwaka huu yana umuhimu wa
pekee sana, kwani yanakwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka hamsini tangu Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipoandika hati kuhusu Uinjilishaji wa Awali,
kwa lugha ya Kilatini, “Ad Gentes”. Ni wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
kuhusu Uinjilishaji Mpya. Matukio yote haya yanapania kwa namna ya pekee, kuimaarisha
ari ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican uliokuwa na ushiriki mkubwa wa Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali
za dunia, ulikuwa ni kielelezo makini cha Kanisa la Kiulimwengu, kwani uliwakutanisha
Maaskofu wanaotekeleza utume wao katika nchi za kimissionari, Maaskofu katika Majimbo
ya Makanisa yao mahalia; wachungaji wa Jumuiya za waamini na wasiokuwa waamini. Kila
kikundi kilijitahidi kutoa mchango wake kwa kuonesha umuhimu wa azma ya Uinjilishaji
wa awali pamoja na kutambua kwamba, umissionari ni kiini na uelewa wa Kanisa.
Changamoto
hii ni kubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kwani kuna idadi kubwa
ya watu wasiomfahamu bado Kristo. Hapa wakristo hawana budi kuamsha ari na moyo wa
utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo; Lilikuwa
ni Kanisa dogo na lisiokuwa na ulinzi wa kutosha, lakini bado liliweza kusimama kidete
kutangaza Injili ya Kristo na kutolea ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo
katika ulimwengu uliokuwa unafahamika kwao.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, anasema, si jambo la kushangaza kuona kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
na baadaye viongozi mbali mbali wa Kanisa walianza kutoa kipaumbele cha kwanza kwa
ari na moyo wa kimissionari ndani ya Kanisa, kama sehemu ya mwendelezo wa amri ya
Kristo aliyoitoa kwa Mitume, ikatekelezwa na waandamizi wao na sasa huu ni wajibu
shirikishi wa Watu wa Mungu. Kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia ni wajibu
msingi wa Maaskofu, ambao wanayo dhamana nyeti ya kuuinjilisha ulimwengu.
Amri
ya kutangaza Injili ya Kristo inagusa kwa namna ya pekee, mikakati ya kichungaji na
maisha ya Kanisa mahalia. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wamelitilia wazo
hili mkazo mkubwa. Huu ni mwaliko kwa Kanisa mahalia daima kujitahidi kusoma alama
za nyakati, ili kuangalia kama mtindo wake wa maisha na mikakati yake ya kichungaji
inakwenda sanjari na agizo hili la Kristo katika ulimwengu mamboleo unaobadilika kwa
kasi ya ajabu. Kila Mkristo anapaswa kutambua kwamba, anawajibishwa na Amri ya Kristo
ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Makleri, watawa
na waamini walei, wote kwa pamoja hawana budi kufuata nyayo za Mtakatifu Paulo, Mtume
na Mwalimu wa Mataifa, aliyefanya kazi hii kwa ustadi mkubwa, akateswa na kujitaabisha
ili kuhakikisha kwamba, Injili inawafikia hata wale waliokuwa bado hawajamwamini Mungu;
kamwe hakujihurumia, kila chembe ya muda wake aliitumia kikamilifu, ili kuhakikisha
kwamba, Injili ya Kristo inafahamika na wengi.
Baba Mtakatifu Benedikto wa
kumi na sita, katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimissionari duniani anakazia kwa namna
ya pekee, ushirikiano wa kimissionari, unaojumuisha mifumo mipya si tu katika masuala
ya kiuchumi, bali wakristo wanapaswa kujimwaga barabara uwanjani ili waweze kushiriki
kikamilifu. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
kwa ajili ya Uinjilishaji mpya ni matukio muhimu ambayo Mama Kanisa anapenda kuyatumia
kuzindua ari na mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kimissionari, unaowahusisha wakristo
wengi zaidi.
Kupanuka na kuenea kwa utume wa Mama Kanisa katika ulimwengu
mamboleo, kunahitaji kuwa na njia makini zinazoweza kutumika kwa ajili ya kutangaza
Neno la Mungu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kila mwamini anaimarisha imani
yake kwa Injili ya Kristo, hasa nyakati hizi za mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza
sehemu mbali mbali za dunia.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema,
moja ya kizingiti kikubwa cha Uinjilishaji mpya ni kinzani za kiimani, si tu katika
nchi za Magharibi, bali sehemu kubwa ya ulimwengu unaoonesha kwa namna ya ajabu kiu
ya kutaka kumfahamu Mwenyezi Mungu; watu hawa hawana budi kualikwa ili waweze kupata
lishe ya chakula kilichoshuka kutoka mbinguni na kuzima kiu ya maisha yao kwa Kristo
chemchemi ya maji ya uzima.
Kuna haja ya kuwa na ari na mwamko mpya wa kutangaza
na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuendeleza azma ya Uinjilishaji
mpya kwa waamini waliokuwa na bahati ya kusikia kwa miaka mingi Injili ya Kristo ikihubiriwa
katika viunga vyao, lakini kwa bahati mbaya sasa wamekengeuka. Ni wajibu wa Mama Kanisa
kuwasaidia tena waamini kama hawa kuonja ile furaha ya kuamini.
Baba Mtakatifu
anakumbusha kwamba, hii ni dhamana kwa Wakristo wote na wala si kwa ajili ya Makleri
peke yao; kila mwamini anapaswa kufaidika na mchakato huu wa Uinjilishaji mpya sanjari
na ushiriki wake makini. Kiini cha Ujumbe wa Injili ni Upendo mkamilifu wa Mungu unaojionesha
kwa namna ya pekee, kwa Mwenyezi Mungu kumtuma Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo aliyejitwalia
hali ya umaskini wa binadamu, akawapenda na kuwakomboa kutoka katika utumwa wa dhambi
na mauti kwa kumwaga Damu yake Azizi pale juu Msalabani kama sadaka safi inayompendeza
Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema kwamba imani
ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini kushirikishana na jirani
zao hazina hii muhimu kwani kamwe hawapaswi kuibinafsisha! Kuna makundi makubwa ya
Makleri, Watawa na Waamini walei wanaotoka katika nchi zao, Jumuiya zao na kwenda
kwenye Makanisa mengine kutoa ushuhuda wa kweli za maisha ya Kikristo sanjari na kutangaza
Habari Njema ya Wokovu kwa jina la Yesu Kristo. Hiki ni kielelezo makini kabisa cha
umoja, ushirikishwaji na upendo miongoni mwa Makanisa.
Hapa mwamini anaweza
kuona jinsi ambavyo imani ilivyonyanyuliwa juu kabisa na kugeuzwa kuwa ni sehemu ya
upendo. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anachukua fursa
hii kuyashukuru Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari, ambayo kwa hakika, yamekuwa
ni vyombo vya vya ushirikiano na Kanisa la Kiulimwengu.
Kwa njia ya utume
na kazi zao mbali mbali Injili inageuzwa kuwa ni msaada kwa wengine; haki kwa maskini;
elimu kwa watoto wanaoishi vijijini; huduma ya afya kwa wote wanaohitaji, lakini kwa
namna ya pekee, wanaoishi vijijini; huu ni ukombozi unaopania kuzima kiu ya mahitaji
ya mtu; kuthaminiwa yule ambaye amesukumizwa pembezoni mwa Jamii; kuchangia maendeleo
endelevu sanjari na kuvunjilia mbali kuta za utengano wa kikabila pamoja na kuheshimu
zawadi ya maisha katika hatua zake zote.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita, anahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Kimissionari duniani, kwa
kutoa baraka zake za kichungaji kwa wadau wote wa Uinjilishaji wa awali, ili kwa njia
ya Roho Mtakatifu na neema za Mwenyezi Mungu, utume huu uweze kuwa na nguvu zaidi
katika historia ya ulimwengu.