Mama Kanisa bado anachangamotishwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya
dunia! Hakuna kulala hadi kieleweke!
Maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani yanakwenda sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee
ya Miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mwaka wa Imani uliotangazwa na
kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita hivi karibuni, Miaka ishirini
ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
juu ya Uinjilishaji Mpya.
Mama Kanisa bado anaendelea kuhimiza umuhimu wa Uinjilishaji
wa awali miongoni mwa waamini wasiomfahamu bado Mungu, kama Mababa wa Mtaguso Mkuu
wa Pili wa Vatican walivyosema, "Ad Gentes". Mtaaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ilikuwa
ni Pentekosti mpya kwa Kanisa, iliyowakusanya Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za
dunia, ili kutoa dira na mwongozo kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya
tatu ya Ukristo.
Huu ulikuwa ni Mtaguso wa Kiekukemene, uliowashirikisha pia
wawakilishi kutoka dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Zaidi ya Maaskofu mia
sita kutoka katika nchi za kimissionari walihudhuria. Leo hii Kanisa katika nchi hizo
lina zaidi ya Majimbo elfu moja na mia moja, kwa hakika, Kanisa limekuwa na kupanuka
katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita.
Haya ni maneno yaliyomo kwenye
ujumbe wa Mheshimiwa Padre Timothy Lehane Barret, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa
la Uinjilishaji wa Watu, katika maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani, inayoadhimishwa
tarehe 21 Oktoba 2012. Anasema, ari na moyo wa kimissionari unapaswa kukuza na kudumishwa
hususan katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani; kwa njia ya kutangaza Injili ya Kristo,
kwa kutambua kwamba, hii kimsingi ni dhamana ya Wakristo wote, lakini Maaskofu ni
wadau wa kwanza kabisa.
Uinjilishaji ni utume muhimu sana unaopaswa kugusa
medani mbali mbali za maisha ya Kanisa pamoja na kuwashirikisha waamini kwa ukamilifu
zaidi, kwani kwa njia ya Ubatizo waamini wamekuwa pia ni wadau wakuu wa Uinjilishaji,
hasa zaidi kwa njia ya maisha yao adili.
Mwaka wa Imani uwawezeshe waamini
katika Jumuiya zao za Kikristo kuwasha moto na ari ya kutangaza na kushuhudia imani
yao katika uhalisia wa maisha. Mtikisiko wa imani, usiwe ni kikwazo cha Uinjilishaji
Mpya, changamoto kwa Waamissionari wapya kujitokeza ili kuweza kumtangaza Kristo hadi
miisho ya dunia, kwa kutumia karama na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Kila
mwamini ajibidishe kukutana na Kristo Mfufuka, ili aweze kuimarisha imani yake na
hatimaye, kuishuhudia.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawashukuru
na kuwapongeza Wamissionari na Mashirika yote ya Kimissionari yanayojitosa kimasomaso
kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Anawahimiza kuendelea kuonesha ushirikiano
na mshikamano ili kufanikisha dhamana hii nyeti katika mapambazuko ya Millenia ya
tatu katika Ukristo.
Huduma mbali mbali zinazotolewa na Wamissionari na Mashirika
haya katika sekta ya elimu, afya, maendeleo endelevu; haki na amani ni kielelezo makini
cha umwilishaji mbegu ya Injili katika hali halisi ya maisha ya watu. Maadhimisho
ya Siku ya Kimissionari Duniani, yalete mwamko mpya katika Mwaka wa Imani.