Ujumbe wa Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya kwenda Syria ili kuonesha mshikamano
wa Kanisa kwa wananchi wa Syria katika kipindi hiki kigumu!
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican akichangia mada kwenye maadhimisho
ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji Mpya anasema, Kanisa haliwezi kuendelea
kukaa kimya wakati ambapo kuna maafa makubwa yanayoendelea kujitokeza nchini Syria.
Tayari idadi kubwa ya Mababa wa Sinodi wamekwisha lizungumzia tatizo hili.
Kardinali
Bertone anasema kwamba, suluhu ya mgogoro wa kisiasa na kijamii unaoendelea nchini
Syria, hauwezi kupatikana tu kwa njia za kisiasa peke yake, ikizingatiwa idadi kubwa
ya wananchi wanaoendelea kuteseka na vita hii, wale wanaokimbia makazi yao kwa kuhofia
usalama wa maisha na mali zao, sanjari na kuangalia kwa umakini mkubwa mustakabali
wa Syria kwa siku za usoni.
Kutokana na changamoto hizi zote, kwa ridhaa ya
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameamua kwamba, ujumbe kutoka Mababa wa
Sinodi ya Uinjilishaji Mpya kwa siku za karibuni kwenda nchini Syria, ili kujionea
wenyewe hali halisi na kama njia ya kuwaonjesha mshikamano kutoka kwa Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita na Kanisa zima, katika kipindi hiki kigumu cha mahangaiko
yao kutokana na mgogoro wa kisiasa na kijamii nchini Syria.
Ujumbe wa Vatican
unalenga kuunga mkono juhudi za kitaifa, kimataifa na kwa wadau mbali mbali wanaoendelea
kujibidisha ili muafaka, haki, amani na utulivu viweze kutawala tena nchini Syria.