2012-10-17 07:43:25

Uchumi, sayansi, teknolojia na siasa jamii ni maeneo mapya yanayohitaji kuinjilishwa tena!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, nakukaribisha kwa moyo mkunjufu kabisa katika mwendelezo wa vipindi vyetu vya uinjilishaji wa kina. Juma lililopita tulizungumzia juu ya maeneo muhimu yanayoguswa na uinjilishaji mpya kama yanavyoletwa kwetu na Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Mwongozo wa Sinodi ”Lineamenta” ya Maaskofu mwaka huu juu ya Uinjilishaji mpya. RealAudioMP3

Leo tuendelee tena kuzungumzia maeneo hayo muhimu yanayoguswa na uinjilishaji mpya baada ya kusikia juu ya utamaduni, sekta ya jamii na mawasiliano.

Uchumi ni eneo muhimu katika uinjilishaji mpya. Hapa Kanisa linakazia zaidi katika ujenzi wa uchumi utakaonufaisha mataifa yote. Hali iliyopo inatishia maisha katika jamii nyingi na kutishia tena mazingira anayoishi binadamu. Kuongezeka kwa umaskini kusini mwa dunia kumepelekea mitafaruku mingi kati ya mataifa na kuzua matatizo ambayo ni changamoto kubwa kwa serikali nyingi. Uharibifu wa mazingira sit u umehatarisha maisha ya watu bali usalama wa dunia kwa ujumla. Leo hii kuna ongezeko kubwa la joto, uhaba wa mvua, matetemeko ya ardhi na mlipuko wa magonjwa ambukizi ambayo yote kimsingi yanatokana na kuharibika kwa mazingira.

Sayansi na teknolojia ni eneo jingine linalhitaji uinjilishaji mpya. Tafiti mpya za kisayansi zimepelekea ugunduzi wa mambo mazuri na ya manufaa kwa binadamu. Ukweli huu usitufanye tupumbae na kushindwa kuelewa kuwa iko hatari sasa ya kuifanya sayansi kuwa mungu na kuacha Mungu wa kweli. Watu wengi kutokana na kukua kwa sayansi wanafikiri kuwa sasa sayansi ina majibu yote ya maisha. Lazima ikumbukwe kuwa sayansi inaboresha tu maisha ya binadamu na sio kuyaumba au kuyaokoa, vinginevyo basi umilele wa maisha ya mwanadamu ulio dhahiri kabisa utakuwa hauna maana.

Siasa ya jamii ni eneo muhimu pia kwa uinjilishaji mpya. Hadi leo tangu Mtaguso wa Pili wa Vatikano kumetokea mabadiliko makubwa sana katika siasa za jamii. Kuanguka kwa ukomunisti kulikomesha malumbano kati ya mashariki na magharibi na kufungua milango ya imani mashariki sambamba na kukuza uhuru wa kuabudu. Lakini hivi sasa kumezuka kwa mifumo mipya ya uchumi na siasa inayojijenga katika misingi ya nguvu na udini huko Asia na Mashariki ya Kati. Hali hii inaleta changamoto mpya ambapo Kanisa lazima lijikite katika kutetea haki, maendeleo ya mtu mzima kiroho na kimwili, kujenga siasa bora zinazojenga usawa na haki kwa watu wote, haki msingi za binadamu na utunzaji wa mazingira kwa mafao ya binadamu na viumbe.

Mpendwa msikilizaji mpaka hapa unaweza kuona kazi nzito inayolikabili Kanisa katika kujenga na kulinda utu na hadhi ya mwanadamu na ulimwengu kwa ujumla kama ilivyokusudiwa na muumba tangu mwanzo. Katika Sinodi ya Maaskofu mwaka huu, Maaskofu wanalo jukumu la kubuni mbinu mkakati na kutoa mwongozo kwetu sote ya jinsi ya kuiishi imani yetu katika mazingira, mila na desturi za kileo bila kuyumbisha mafundisho msingi ya Injili na Kanisa.

Kutoka Studio za Radio Vatican, nakutakia Baraka tele toka kwa Mwenyezi Mungu na usikilizaji mwema wa vipindi vingine vya idhaa ya Kiswahili. Tukutane tena juma lijalo. Ni mimi mtayarishaji na msimulizi wako Fr George wa Bodyo.










All the contents on this site are copyrighted ©.