Katekesi za Baba Mtakatifu katika Mwaka wa Imani zinalenga kufahamu kweli za Imani
kuhusu Mungu, Binadamu, Kanisa na Ulimwengu mintarafu Kanuni ya Imani
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano tarehe 17 Oktoba, 2012 ameanza
mzunguko mpya wa katekesi unaolenga kutoa tafakari ya kina kuhusu maadhimisho ya Mwaka
wa Imani, kwa kukazia umuhimu wa shule ya sala, ili kuleta mwamko na ari mpya ya kumwamini
Kristo, Mkombozi pekee wa dunia, ili hatimaye, waamini waweze kufuata nyayo zake kwa
kutolea ushuhuda wa nguvu ya imani inayoleta mabadiliko.
Maadhimisho ya Jubilee
ya Miaka hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni fursa nyingine ya kumrudia
Mwenyezi Mungu pamoja na kujitahidi kuimwilisha imani kwa Kristo na Kanisa lake ambaye
ameendelea kuwa kweli ni mwalimu wa binadamu kwa njia ya: Utangazaji wa Neno la Mungu,
Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Matendo ya Huruma kama mwongozo wa kukutana
na hatimaye, kumfahamu Kristo: Mungu kweli na mtu kweli.
Lengo ni kumwezesha
mwamini kufanya mabadiliko ya ndani kwa kurekebisha mahusiano yake yote pamoja na
kuanza kujenga mwelekeo mpya mintarafu wito wao katika historia, maana ya maisha na
kwamba, wao daima ni mahujaji kuelekea Yerusalem ya mbinguni.
Baba Mtakatifu
anasema, Katekesi zake katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, zinapania kwa namna ya
pekee kuimarisha hija ya waamini wanaotafuta furaha katika imani, ili waweze kuifahamu
na kuimwilisha. Hii ni imani kwa Mungu ambaye ni upendo, aliyejishusha na kumkaribia
mwanadamu, kiasi cha kuyamimina maisha yake pale juu Msalabani kama njia ya kumkomboa
binadamu huyu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; hatimaye, aweze kuonja upendo
na utimilifu wa maisha.
Imani hii kuliko wakati mwingine wowote katika historia
inapaswa kutolewa ushuhuda makini, watu waonje na kuguswa na upendo wa Mungu na huduma
kwa wahitaji ili kuondokana na ubinafsi na umaskini wa binadamu kutokana na uchoyo
wake. Imani ya Kikristo inajidhihirisha kwa njia ya matendo ya huruma, ina nguvu katika
matumaini na humwezesha mwanadamu kupata utimilifu wa maisha.
Imani inafumbata
ujumbe huu na hivyo kumletea mwanadamu mabadiliko ya ndani yanayomwezesha kumfahamu
Mungu na mipango yake katika maisha ya mwanadamu. Mungu anavuka mipaka ya akili ya
binadamu, ibada na sala. Kwa njia ya Maandiko Matakatifu, waamini wanaweza kuufahamu
ukweli kwa njia ya Roho Mtakatifu. Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akateswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Huyu ndiye aliyejifunua kwa njia ya vinywa vya
manabii, lakini, kwa njia ya Neno lake amejionesha kwa wote hadi miisho ya dunia.
Kanisa
ambalo limezaliwa kutoka katika ubavu wa Kristo, pale alipochomwa mkuki mara ikatoka
damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa, ni kielelezo makini cha matumaini kwa
Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Yesu aliteswa, akafa na kufufuka, amekaa kuume kwa
Baba, ni hakimu wa wazima na wafu ndicho kiini cha imani ya Kanisa, changamoto kwa
wafuasi wa Kristo anasema Baba Mtakatifu kuwa waaminifu kwa imani hiyo.
Kanuni
ya Imani ni muhtasari ambao unaonesha kweli za kiimani zilizopokelewa kwa mara ya
kwanza na Mitume wa Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kwa namna ya pekee, kujibidisha
kufahamu mahudhui yaliyomo kwenye Kanuni ya Imani kwani hii ni dira na mwanga katika
hija ya maisha ya waamini hapa duniani, ili kuvuka vikwazo vya ukame na jangwa na
maisha ya kiroho katika ulimwengu mamboleo. Kanuni ya Imani ni chimbuko la maisha
adili miongoni mwa Wafuasi wa Kristo.
Huu ndio mchango mkubwa na endelevu
kutoka kwa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, Kanisa linapoadhimisha kumbu kumbu ya
Miaka ishirini tangu alipochapa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Kanisa lina dhamana
ya kuitangaza Imani na Injili, ili mwanga wa Injili ya Kristo uweze kuleta mabadiliko
katika maisha ya Kijamii, kwa kuwashirikisha wengine matumaini yaliyoko ndani mwao.
Waamini wajitahidi kujifunza imani yao ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza
katika Ulimwengu mamboleo. Ujumbe wa Injili uwasaidie waamini kumrudia Mungu kwa njia
ya Yesu Kristo.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, hili ndilo
lengo lake la Katekesi atakazotoa katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani; ili kufahamu
kwa kina na mapana kuhusu kweli za Imani kwa Mungu, Binadamu, Kanisa, Maisha Jamii
na Ulimwengu, mintarafu Kanuni ya Imani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, imani
hii itaweza kumwilishwa katika maisha; kwa kukazia wongofu wa ndani unaotoa mwono
mpya wa kumwamini, kumfahamu na hatimaye kukutana naye.