Katekesi makini na kina; ushuhuda wa Injili ya Upendo na Majadiliano na ulimwengu
mamboleo ni kati ya vipaumbele katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji mpya wanaendelea kuhimiza waamini
kufanya maandalizi ya kutosha: kiroho na kimwili wanapopania kufanya hija kwenye maeneo
matakatifu yanayobeba viashiria vya imani ya Kanisa. Nchi Takatifu ni kati ya maeneo
yanayobeba kwa kiasi kikubwa historia ya maisha na utume wa Yesu aliyeteswa, akafa
na kufufuka kutoka katika wafu. Lakini kwa bahati mbaya, maeneo haya yamekuwa pia
yakijuhujimiwa.
Uwepo wa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo
cha imani hai, kinachoweza pia kukoleza na kuimarisha imani ya wafuasi wa Kristo katika
maeneo matakatifu. Ni mwaliko wa kuendelea kuombea imani na amani inayokabiliwa na
changamoto kubwa huko Mashariki ya kati.
Waamini wanapaswa kutambua kwamba,
imani yao si jambo binafsi, wala urithi wa kijamii na kihistoria, bali ni dhamana
nyeti wanayochangamotishwa kuitolea ushuhuda amini miongoni mwa watu wanaoishi nao.
Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja ya kuendelea kuimarisha Katekesi kwa
njia ya tafakari ya kina, inayowashirikisha pia wasomi na wanasayansi wa Kanisa Katoliki
ili imani hiyo iweze pia kumwilishwa katika maisha na tamaduni za watu, kama njia
ya kuendeleza mchakato wa utamadunisho. Wakristo wanapaswa kutolea ushuhuda makini
wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, na kamwe wasijisikie wanyonge, kwani wana
haki ya kuwa jinsi walivyo. Katekesi iwe ni muhtasari makini wa kile ambacho Mama
Kanisa anaamini, anaadhimisha, anaishi katika uadilifu wake na kusali kama njia ya
majadiliano na Mwenyezi Mungu, ili kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mungu pamoja
na jirani.
Ili mchakato wa Uinjilishaji Mpya uweze kuchukua kasi inayokusudiwa
na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kuna umuhimu wa
kuwa na Wainjilishaji Wapya, wenye mwono mpana, mang'amuzi na ufahamu mpana wa imani
yao kama ilivyokuwa kwa watakatifu, wafia dini, waanzilishi wa Mashirika, Mababa wa
Kanisa, Wamissionari na wadau wengine wa Uinjilishaji kadiri ya Mapokeo ya Mama Kanisa.
Hawa ni mihimili na mfano wa kuigwa hata kwa Kanisa la nyakati hizi. Mababa
wa Sinodi wanakazia umuhimu wa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika
uhalisia wa maisha, kwa njia ya ushuhuda makini, maombezi ya watakatifu na hija katika
maeneo yenye mguso na mvuto wa kiimani. Mambo yote haya ni msaada mkubwa katika azma
ya Uinjilishaji Mpya ndani ya Kanisa.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia,
kuyumba kwa uchumi wa kimataifa pamoja na kuporomoka kwa misingi ya maadili na utu
wema, kumepelekea mahangaiko makubwa kwa watu wengi duniani, kiasi cha kujikuta watu
wanaogelea katika dimbwi la umaskini wa kipato kutokana na ukosefu wa fursa za ajira.
Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya kuendeleza majadiliano
ya kitamaduni na kiuchumi, kwa kuzingatia maadili, utu wema, haki msingi za binadamu
pamoja na kupania kutafuta na kulinda mafao ya wengi ndani ya Jamii.
Maendeleo
ya sayansi na teknolojia yasiwe ni chanzo cha kinzani za kijamii, kutokana na kuongezeka
kwa idadi kubwa ya maskini. Kanisa daima lijitahidi kuonesha mshikamano wa dhati na
waathirika wa matukio kama haya, ili hata katika ugumu wa maisha yao, waweze kuonja
huruma na upendo wa Kristo.
Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo,
Kanisa kwa namna ya pekee, linaalikwa kuutangaza na kumwilisha: haki, amani, upendo
na mshikamano wa Kristo kwa waja wake kwa njia ya maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji
ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wainjilishaji watambue na kuthamini utajiri mkubwa
unaofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kama nyenzo msingi wa Uinjilishaji
Mpya unaopania kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda makini wa imani ya Kikristo.
Mkazo utolewe kwa Majandokasisi, Watawa na Waamini walei, ili waweze kuyafahamu
Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo ni kujenga na kukuza utakatifu wa kijamii, katika
ulimwengu unaoendelea kuogelea katika dhana ya ukanimungu. Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere ni kati ya mifano bora ya kuigwa kwenye medani za siasa.
Uinjilishaji
Mpya ujikite katika kulisoma, kulifafafanua na kulimwilisha Neno la Mungu kuanzia
katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na Kanisa
katika ujumla wake, ili kuzima kiu na njaa ya uwepo wa Mungu katika maisha ya watu.
Ikumbukwe kwamba, kutangaza Habari Njema, ni dhamana ya kila Mkristo na wala si kwa
Makleri na Watawa peke yao. Waamini walei wanaalikwa kuitangaza Injili ya Kristo kwa
njia ya ushuhuda wa maisha, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.
Uinjilishaji Mpya uimarishe umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Kristo,
kwa kukuza na kuendeleza ari na mwamko wa kimissionari, daima waamini wakiwa tayari
kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza Kristo hadi miisho ya dunia. Umoja
na mshikamano ni changamoto kubwa kutoka katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Maneno
yaendane na vitendo vinavyoleta mvuto na mguso katika maisha ya watu, kwa kujikita
katika wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Ulimwengu mamboleo unatawaliwa
kwa kiasi kikubwa sana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, hii ni fursa
kubwa inayopania kuufanya ulimwengu kuwa kama kijiji. Njia hizi za mawasiliano zinaweza
pia kutumiwa na Mama Kanisa kwa ukamilifu zaidi katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya.
Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linawaandaa watu kutekeleza utume huu
nyeti kwa kuzingatia Mafundisho Tanzu na Mapokeo ya Kanisa.
Yesu ni kiini
cha Uinjilishaji na Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa hadi miisho ya dunia.
Familia za Kikristo ziwe ni vitovu vya Uinjilishaji Mpya, kwa kukazia pia majiundo
makini na endelevu kwa wanandoa watarajiwa. Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano
ya kiekumene katika maisha ya sala, huduma na mshikamano ili dunia iweze kumwamini
Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Mababa wa Sinodi wanasema,
kuna haja ya kuangalia tatizo la vijana wengi wanaokimbilia mijini wakitafuta nafuu
ya maisha, kwani hawa pia wanahitaji kuinjilishwa na wakisha injilishwa, basi wawe
pia ni vyombo vya uinjilishaji miongoni mwa vijana wenzao katika hija ya maisha yao.
Vijana wakumbuke kwamba, kwa sasa wanakabiliwa na dhana ya ubinafsi, athari za maendeleo
ya sayansi na teknolojia ya habari; athari za utandawazi, mawazo mepesi mepesi pamoja
na kukosa mifano bora ya kuigwa katika imani. Watambue kwamba, hakuna njia ya mkato
katika maisha, bali wanapaswa kwanza kabisa kujifunza kwa juhudi, bidii na maarifa.
Wachungaji na waamini kwa ujumla wao, wawasaidie vijana kukua na kukomaa katika
misingi ya imani, matumaini na mapendo kamili. Waamini watambue kwamba, Mungu ni upendo,
unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha.
Huu ndio ushuhuda wa Injili
ya Upendo uliotolewa na Mama Teresa wa Calcutta pamoja na umati mkubwa wa waamini
wanaoendelea kutoa huduma kwa wagonjwa, wakimbizi, watu wasiokuwa na makazi pamoja
na huduma mbali mbali za matendo ya huruma. Lengo ni kuwawezesha watu wote hawa kupata
utimilifu wa maisha kama Kristo mwenyewe alivyoahidi. Huu ndio utume unaoendelezwa
na Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.