2012-10-16 09:09:14

Waamini walei wanalo jukumu la kuyatakatifuza malimwengu kwa moyo na tunu msingi za Kiinjili


Askofu Beatus Kinyaiya mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji mpya, amekazia juu ya dhamana ya waamini walei katika azma ya Uinjilishaji. Mama Kanisa ana rasilimali kubwa ya watu ambayo ni waamini walei, inayoweza kutumika katika mchakato wa Uinjilishaji. Waamini hawa kwa njia ya nguvu na imani yao wanaweza kutoa msukumo mpya katika maisha ya Kikanisa.

Askofu Kinyaiya anasema, Barani Afrika kuna kampeni ya chini chini inayopania kuhakikisha kwamba, Kanisa na Viongozi wake hawajishughulishi kabisa na maisha ya Kijamii, kwa maneno mengine, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuhubiri Makanisani na kamwe wasijishughulishe na masuala ya kijamii.

Kuna mikakati na sera zinazotolewa na baadhi ya Nchi Barani Afrika, zinazotaka kulinyima Kanisa fursa za kushiriki na kuchangia kikamilifu katika sekta ya elimu, afya, huduma za kijamii, vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja na kutaka kuzima sauti ya kinabii inayokazia umuhimu wa maadili na utu wema mintarafu tunu msingi za Kiinjili.

Katika mazingira kama haya anasema Askofu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Katoliki la Mbulu, Tanzania kwamba, wito na dhamana ya waamini walei ni kuyatakatifuza malimwengu kwa kujikita zaidi na zaidi katika wito na dhamana waliyojitwalia wakati walipopokea Ubatizo. Ni jukumu lao kuhakikisha kwamba, maadili, mafao ya wengi, haki na amani vinadumishwa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, kisayansi, kisanaa na katika vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Waamini walei wanadhamana ya Kuinjilisha: upendo wa kibinadamu, maisha ya kifamilia, kwa kujikita katika malezi na majiundo ya watoto na vijana; kwa kushirikisha taaluma na ujuzi wao kwa ajili ya mafao ya wengi sanjari na kuwahudumia wagonjwa na wote wanaoteseka; yote haya yafanyike kwa lengo la kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Viongozi wa Kanisa kwa upande wao, wanayo dhamana na jukumu la kuhakikisha kwamba, waamini walei wananolewa barabara, kwa kujenga na kuimarisha vituo na taasisi za majiundo ya walei bila kusahau kutumia pia taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa.

Ni changamoto kwa Mabaraza ya Maaskofu na Majimbo mbali mbali kuanzisha mchakato wa kuadhimisha Sinodi katika maeneo yao, ili kuwashirikisha waamini katika hatua mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei wanapaswa kusaidiwa katika maisha yao ya kiroho kwa njia ya mafungo na semina mbali mbali bila kusahau kuwajengea moyo na ari ya kimissionari ndani mwao.

Askofu Beatus Kinyaiya anakamilisha mchango wake katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji mpya kwa kusema kwamba, Yesu Kristo ndiye Mkulima wa kweli, anayewaita wanadamu kushiriki katika kazi ndani ya shamba lake, ili liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Ni wajibu wa waamini walei kuyatakatifuza malimwengu, changamoto inayoweza kujionesha kwa namna ya pekee katika: mila, sheria na miundo ya jamii wanamoishi. Ni jukumu la waamini walei kuyatakatifuza malimwengu kwa moyo na tunu msingi za Kiinjili.







All the contents on this site are copyrighted ©.