2012-10-16 08:44:19

Taalimungu inayofundishwa na kumwilishwa, iwe ni sayansi ya imani inayomsaidia mwanadamu kufahamu kweli za Kiimani


Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ni kati ya Mababa wa Sinodi waliochangia mada wakati wa maadhimisho ya kikao cha kumi na moja cha Sinodi juu ya Uinjilishaji mpya inayoendelea hapa mjini Vatican. Anabainisha kwamba, kuna ukakasi miongoni mwa watu kutaka kufahamu masuala ya dini na hasa "dini ya kweli", kwani inaonekana kwamba, watu wanatafuta kwa namna ya pekee, kufahamu mang'amuzi ya kidini na mifumo mbali mbali ya maisha ya kidini inayoridhisha njia zao za ufahamu.

Kardinali Njue anasikitika kusema kwamba, inashangaza kuona kwamba, kuna umati mkubwa hata miongoni mwa waamini wasiomfahamu Mwenyezi Mungu na hiki ndicho kielelezo cha myumbo wa imani unaojionesha sehemu mbali mbali za dunia. Umefika wakati kwa Mama Kanisa kufungua malango yake ili kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, kwa njia ya ushuhuda makini wa wafuasi wake, unaojionesha katika nia na majitoleo ya imani. Wakristo wanayo dhamana ya kuihabarisha Jamii kwa njia ya Mafundisho ya Kristo na Kweli za Kiinjili.

Taalimungu inayofundishwa na kumwilishwa na Mama Kanisa, iwe ni sayansi ya imani inayosaidia akili ya mwanadamu kufahamu kweli za kiimani. Akili na Imani ni chanda na pete, vinaopaswa kusaidiana ili kumsaidia mwamini katika maisha yake ya kiroho. Wanataalimungu wanaoishi katika Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo wanapaswa kuonesha utakatifu wa maisha na wala si tu kama majaalimu waliobobea katika taaluma ya kufundisha ukweli. Wawe ni watu waliomwongokea Kristo na watakaowasaidia waamini kumwilisha imani yao kwa njia ya upendo.

Kardinali John Njue ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi anasema kwamba, Kanuni ya imani inapaswa kuwa ni "chakula cha kila siku" kwa ajili ya waamini; kwani huu ni muhtsari wa imani ya Kanisa inayopaswa kufahamika na kumwilishwa. Waamini wanapaswa kukabiliana na changamoto za kiimani kwa njia ya ukweli na ujasiri pasi ya kukata tamaa, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kuhakikisha kwamba, imani hii inashughulikiwa kikamilifu.

Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaitolea ushuhuda makini imani yao, kwa njia ya neema iliyomiminwa ndani mwao, inayowawezesha kumwongokea Kristo kutoka katika undani wa mioyo yao. Hii ni hija ndefu inayopaswa kuendelezwa na wafuasi wa Kristo katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Waamini wanapaswa kukua na kukomaa katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.