2012-10-16 10:11:45

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, "Mwamba wa Imani" Siku ile alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki


Ilikuwa ni tarehe 16 Oktoba 1978, Kardinali Karol Wojtyla, majira ya jioni, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ulipolipuka kwa shangwe na nderemo, alipotangazwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, akichukua jina la Yohane Paulo wa Pili.

Kwa upande wa Jimbo kuu la Cracovia lilikuwa ni pigo kubwa kwani waamini hawakutaka kumwachilia kiongozi wao mkuu waliyempenda na kumthamini, lakini waliridhia mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, wakawa ni waombezi wake wakuu katika maisha na utume wake kwa Kanisa la Kiulimwengu.

Ni maneno ya Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, ambaye tangu akiwa na umri wa miaka ishirini na saba, miaka mitatu ya daraja takatifu la Upadre, alililipokea kutoka mikononi mwa Askofu mkuu Karol Wojtyla kwa wakati huo, ndiye anayesimulia tukio hili la kihistoria ambalo limeacha kumbu kumbu ya kudumu katika mioyo ya waamini na watu wenye mapenzi mema, sehemu mbali mbali za dunia. Alipoteuliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, akamteua naye pia kuwa ni Katibu wake muhtasi, utume alioutekeleza hadi mauti ilipomfika Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, baada ya kuliongoza Kanisa kwa ari na moyo mkuu.

Kardinali Stanislaw anasema kwamba, hija ya maisha ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, iliyojaa nyakati za furaha, majonzi na masikitiko makubwa, zimekuwa ni muhimu sana katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa, kiasi cha kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Injili ya Upendo wa Kristo hadi miisho ya dunia. Alikuwa ni mtu ambaye sala kilikuwa ni chakula chake cha kila siku. Alipenda kunoa akili yake kwa kujisomea na kuandika mara kwa mara, yote haya yakiwa ni matokeo ya tafakari ya kina kwa Yesu wa Ekaristi.

Ni Kiongozi ambaye kwa kipindi cha muda mfupi, aliweza kufahamika, kupendwa na kuheshimiwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kamwe hakusahau utamaduni na mapokeo ya nchi yake ya Poland yaliyomwezesha kuwa na majiundo makini: kiroho, kimwili, kiakili pamoja na uwezo wa kuwafahamu lugha mbali mbali. Aliutambua ulimwengu, changamoto na matumaini yake, akawa daima tayari kutoa majibu muafaka kwa kusoma alama za nyakati.

Ni mtu ambaye alipenda kuwajengea waamini na watu wenye mapenzi mema, ujasiri wa kufungua malango ya maisha na mioyo yao kwa Kristo bila woga, dira na mwelekeo ambao ameutekeleza katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kipindi cha miaka ishirini na saba. Ulimwengu unachangamotishwa hata leo hii kuruhusu tunu msingi za Kiinjili ziweze kupenya katika sekta mbali mbali za maisha, ili Mwenyezi Mungu aweze kupewa heshima, sifa na utukufu; mwanadamu athaminiwe utu na heshima yake; maadili na utu wema, viweze kutawala; daima: ukweli na uhuru wa mwanadamu vikipewa msukumo wa pekee.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, alipenda kuhakikisha kwamba, watu wanatambua uwepo wa Mungu katika maisha yao na kwamba, ndani na kwa njia ya Yesu Kristo, wanaweza kupata maana na utimilifu wa maisha yao. Yohane Paulo wa Pili ni kati ya viongozi wajiojitosa kimasomaso katika dhamana ya Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, changamoto na mfano wa kuigwa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani. Wafuasi wa Kristo, waendelee kujitaabisha ili kweli za Kiinjili ziweze kueleweka miongoni mwa watu!

Kardinali Stanislaw Dziwisz anasema, kwa hakika amejifunza na kujiunda kwa umakini mkubwa katika shule ya Yohane Paulo wa Pili, kwa ajili ya upendo kwa Kristo na Kanisa lake; maisha ya kiroho, kwa kujitoa bila kujiachilia kwa ajili ya Mungu na jirani. Kwa hakika, utajiri wa maisha na utume wake ni mchango mkubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.