Dini zina wajibu wa kukumbusha sheria maadili katika kukuza na kudumisha misingi ya
haki ndani ya Jamii
Mheshimiwa Padre Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano
ya Kidini, akishiriki katika mkutano wa majadiliano ya kidini, uliofanyika hivi karibuni
huko Istanbul, Uturuki, uliokuwa unaongozwa na mada "haki na ujenzi wa mfumo mpya
wa ulimwengu" alikazia umuhimu wa Jamii kuendelea kujikita katika mchakato wa kumwilisha
haki jamii sanjari na uhuru wa kidini kama njia ya kujenga na kuimarisha misingi ya
haki, amani na utulivu na kwamba, dini mbali mbali duniani zinayo dhamana kubwa ya
kusimamia ujenzi wa haki na amani.
Padre Miguel anabainisha kwamba, dini zinao
mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha majadiliano katika Jamii ya watu, ili kwa
pamoja, waweze kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu
wa sayansi na teknolojia. Dhana ya amani na jamii ni tema zinazofumbatwa katika maisha
ya kiroho ndani ya dini mbali mbali. Kanisa Katoliki kwa kadiri ya Mapokeo yake, linatambua
na kuthamini umuhimu wa haki kama sehemu ya mchakato wa mwanadamu kufikiri, kwa waamini,
wasioamini na watu wote wenye mapenzi mema.
Hii ni dhana inayoenzi na kudumisha
msingi wa utu wa mwanadamu na kwamba, uwezo wake wa kufikiri ni haki msingi ambayo
inapaswa kutetewa na kuheshimiwa na wote, ili kweli haki iweze kutendeka. Serikali
zina wajibu wa kutoa haki kwa raia wake na kwamba, kiwango hiki kinapimwa kwa umakini
mkubwa kwa njia ya utendaji wake. Serikali zinaposhindwa kutoa haki kwa raia wake,
hapo zinapoteza dhamana yake ya kimaadili.
Dhana hii inaonesha kwamba, Serikali,
kimsingi zinaweza pia kuwajibishwa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake ndani ya Jamii
mintarafu sheria maadili na wala huu si uchaguzi wa kisiasa. Ni changamoto kwa Serikali
na Jamii kuhakikisha kwamba, zinatekeleza wajibu wake msingi pamoja na kutoa fursa
kwa dini na viongozi wake kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watu wao. Dini zina
dhamana ya kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wanyonge na wote wasiokuwa na sauti
wala uwezo wa kujitetea na wote wanaodhulumiwa katika hali mbali mbali za maisha.
Hii ni sauti ya kinabii, inayohamasisha suluhu ya amani ili haki iweze kupatikana.
Ni changamoto pevu kwa Jamii kutafuta daima mafao ya wengi. Kutokana na mantiki hii,
dini zinao mchango mkubwa hata katika masuala ya kisiasa, kwa kukazia umuhimu wa sheria
maadili kama njia kudumisha haki ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki.