Wenye heri wa kwanza katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani watangazwa na Kanisa kwa
kuthubutu kuishuhudia imani yao kwa njia ya kifodini!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana,
Jumapili iliyopita, 14 Oktoba 2012, alimzungumzia Mtumishi wa Mungu Federic Bachstein
pamoja na Wanashirika wenzake, kumi na watatu wa Shirika la Ndugu Wadogo, waliouwawa
kikatiliki kutokana na msimamo wa imani yao kunako mwaka 1611, waliotangazwa kuwa
ni Wafiadini, walioshuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hata wakathubutu
kuyamimina maisha yao. Tukio hili limefanyika huko Prag, Jamhuri ya Watu wa Czech.
Baba
Mtakatifu anasema, hawa ni Mashahidi wa Kwanza kutangazwa katika Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani. Ni wafiadini wanaowakumbusha Wafuasi wengine wa Kristo kwamba, kumwamini
Kristo maana yake ni kujiachilia mikononi mwake, kiasi hata cha kuyamimina maisha
pamoja na kwa ajili ya Yesu.
Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu anaendelea
kuwaalika waamini katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kuwa na ujasiri wa kujadiliana
na Yesu, ili aweze kuwaonesha yale anayotaka wafanye zaidi, ili wapate uzima wa milele.
Hii ni changamoto kwa watu walio pweke, maskini na wagonjwa, ili katika hija ya maisha
yao hapa duniani waweze kuwa ni warithi wa maisha ya uzima wa milele na ahadi kutoka
kwa Mwenyezi Mungu.
Amewapongeza kwa namna ya pekee, Waamini na Watu wenye
mapenzi mema kutoka Poland waliomiminika kwa wingi kabisa kwa ajili ya kumbu kumbu
ya maadhimisho ya Siku ya Yohane Paulo wa Pili, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu
"Mtumishi wa Mungu Yohane Paulo wa Pili ni Papa wa Familia". Amewapongeza kwa moyo
wao wa mshikamano na umoja ndani ya Kanisa. Anawaalika waamini na watu wote wenye
mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yanakoleza imani,
Injili ya Upendo na kutafuta daima mapenzi ya Mungu katika hija ya maisha yao hapa
duniani.