2012-10-15 09:59:03

Vikwazo katika upendo na maisha ya ndoa na familia


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, nakualika tena tuendelee na tafakari zetu za ndoa na familia na sasa tuangalie kuhusu msamaha na uaminifu ambazo ni nguzo muhimu katika maisha ya ndoa na familia. Ila leo katika kipindi chetu cha kwanza tuseme kidogo kuhusu vikwazo katika safari hii ya ndoa. RealAudioMP3
Ndugu msikilizaji, maisha ya ndoa na familia kama ilivyo kwa maisha mengine yana misimu mbalimbali, yana masika na kiangazi, vuli na hari. Kuna nyakati za furaha kweli lakini kuna nyakati za magumu na machungu. Hapa ni mwaliko kwa wanandoa hasa kwenye miaka ya kwanza ya ndoa kutambua changamoto hizo na kuzitumia vizuri katika kujenga mazingira ya upendo wa kudumu.
Baadhi ya changamoto wanazoweza kukutana nazo wanandoa ni kupoteza mivuto ya kimwili iliyo muhimu sana kwa umoja wao. Wakati mwingine upendo wao hupoteza vionjo vipya na kuwa kitu cha kawaida (monotonous) na katika maana hii kila mmoja kati ya wana-ndoa humwona mwenzake kama kipingamizi kinachomzuia kupumua na kufurahia uhuru binafsi.
Ni vizuri hapa turejee tena katika simulizi la uumbaji. Adamu alipojitambua katika muungano wao na Eva furaha iliwajaa. “Huu ni mfupa na nyama katika nyama yangu, ataitwa mwanamke” (Mwanzo 2:18-24). Lakini muda si muda baada ya kuvunja amri za Mungu wananyosheana sasa vidole, “si huyu mwanamke uliyenipa” nawe mwanamume ulikuwa wapi wakati yote haya yanatokea? Hapa tunagundua umimi, ukosefu wa uvumilivu, uamuzi wa haraka, dharau na hata wivu wa kupindukia, hata wakati mwingine tabia ya kutaka kulipiza kisasi.
Hapa wanandoa huanza kupoteza ule uzawadi uliotawala maisha yao. Upendo huanza kuwa baridi, matendo ya upendo huanza kufa na kila mmoja humwona mwenzake kama kizuizi, hatari na mzigo kwake. Hatua kwa hatua hufikia mahali pa kukosa uaminifu katika tendo la ndoa (betrayal of the intimacy). Wanandoa hufikia mahali pa kutafuta kitulizo cha upendo na umoja nje ya muungano sahihi wa ndoa ambao kwa uhakika haufikiwi ila matatizo huongezeka kama wengi tunavyoshuhudia. Hapa tunayo mifano mbalimbali ambayo kama yote tungeitaja muda wetu kwa uhakika usingetutosha.
Ndugu msikilizaji, ndoa hujengwa na upendo na matendo ya mapendo. Huu ni mwaliko kwa kila mmoja kati ya wana-ndoa kujitahidi kujenga mazingira mazuri yanayomvutia mwenzake katika umoja kamili tusiishie kusema huyu mwenzangu ana matatizo. Je, mimi nimechangia kiasi gani kumfanya mwenzangu adumu katika uaminifu wa kindoa? Huu ni mwaliko wa kufanya vizuri zaidi pale ambapo ubaridi umetawala.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.