Yaliyojiri katika maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji mpya inayoendelea hapa mjini
Vatican
Viongozi wawakilishi kutoka katika Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki,
sehemu mbali mbali za dunia, wamepata fursa ya kuweza kutoa mchango wao kuhusu hali
ya maisha na utume wa Kanisa kutoka katika maeneo yao.
Kardinali Peter Erdò,
Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, amekazia umuhimu wa
Bara la Ulaya, kutambua na kuenzi utambulisho wao unaopata chimbuko lake katika Ukristo.
Hii ndiyo changamoto endelevu iliyojitokeza mara tu baada ya maadhimisho ya Jubilee
kuu ya Ukristo, iliyofanyika kunako mwaka 2000. Licha ya matukio mbali mbali ya kiimani
ambayo yameendelea kuadhimishwa na Mama Kanisa, lakini Bara la Ulaya linaendelea kuonesha
ukakasi katika maisha ya kiimani ya Kikristo.
Hii ni propanda inayoendeshwa
na vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Mafundisho ya dini shuleni hayana mkazo wa pekee.
Huu ni utafiti uliofanywa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya kwa
kusema kwamba, hizi ni dalili za kuporomoka kwa misingi ya imani, miongoni mwa wananchi
wa Ulaya.
Nchi nyingi zinaendelea kukazia umuhimu wa haki msingi za binadamu,
lakini zenye mwono tenge kuhusu maisha ya mwanadamu na utu wake. Kumeibuka ndoto ya
kudhani kwamba, kwa nguvu ya mawasiliano ya jamii na kiuchumi, hata wakati mwingine
kwa kubeza maadili; watu wanaweza kuitawala dunia kama wanavyopenda. Lakini, ukweli
wa mambo ni kwamba, kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya pamoja na
uwepo wa idadi kubwa ya wazee wanaohitaji hifadhi za kijamii ni kati ya viashilia
vikubwa kwa kuyumba kwa uchumi Barani Ulaya.
Kardinali Erdò anasema, matatizo
na changamoto zote hizi zinaibua kwa namna ya pekee, kiu na njaa ya tumaini jipya,
kama inavyojionesha katika maadhimisho ya Siku za Vijana Kimataifa na katika hija
za kichungaji za Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa miaka ya hivi karibuni.
Matukio haya yamekuwa ni chemchemi ya miito na matumaini mapya kwa waamini Barani
Ulaya.
Parokia nyingi zimeanza kutambua na kuthamini utume na dhamana yao ya
kushiriki katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa kuzishirikisha pia Familia za Kikristo
na Vyama vya Kitume. Uwepo wa Waamini na Wamissionari kutoka Mabara mengine umechangia
kukoleza moto wa matumaini! Matendo ya huruma kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii, ni utume unaoendelea kumwilisha utamaduni wa upendo. Licha ya kinzani, migogoro
na vita ambavyo vimejitokeza katika maeneo kadha wa kadha Barani Ulaya. Zote hizi
zimekuwa ni fursa za kujenga na kukuza moyo wa upatanisho wa kitaifa sanjari na kuendeleza
majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga Jamii inayoheshimu na kudumisha misingi
ya haki, amani na upendo.
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kwa upande wake amekazia
umuhimu wa Kanisa Barani Afrika kuwa na sura ya Kiafrika na bado likaendelea kujitambulisha
kuwa ni Katoliki. Uinjilishaji mpya Barani Afrika, kwa namna ya pekee kabisa, ulipata
chimbuko lake kutoka kwa Papa Paulo wa Sita, aliyewahamasisha Waafrika kuwa ni Wamissionari
Barani Afrika. Changamoto kubwa kwa SECAM iliyoanzishwa kunako mwaka 1969 ni kunenga
na kuendelea kuimarisha: umoja, mshikamano na ushirikiano wa dhati miongoni mwa Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki Afrika la Madagascar.
Kardinali Pengo anasema kwamba,
Jumuiya ndogo ndogo za kikristo ni chemchemi ya Uinjilishaji wa kina Barani Afrika.
Utandawazi na athari zake ni kati ya vikwazo vinavyodumaza mchakato wa Uinjilishaji
wa kina Barani Afrika, madhara yanayojioneshahata katika imani ya Kikristo. Tunu msingi
za maisha ya Kiafrika zinaendelea kuwekwa majaribuni, kiasi hata cha kuanza kubeza
thamani ya uhai wa binadamu kwa kupenda kukumbatia utamaduni wa kifo. Kuna watu wenye
misimamo mikali ya imani hali ambayo imesababisha kinzani na migogoro kati ya Waislam
na Wakristo; hali ambayo kimsingi ni kikwazo cha Uinjilishaji wa kina Barani Afrika.
Kardinali
Pengo anachambua historia ya Uinjilishaji Barani Afrika kwa kusema kwamba, uwepo wa
Wamissionari kutoka nje ya Afrika, kulionekana kuwa ni chanzo cha kutaka kukidhi zaidi
mahitaji ya malighafi kwa nchi zao asilia. Dhana kama hii pia inajitokeza kwa Wamissionari
wanaotoka Afrika kwenda Kuinjilisha Ulaya, kujikuta kwamba, wanaelemewa zaidi na uchu
wa kutafuta mali.
Ni ukweli usiopingika kwamba, Wamissionari waliopikwa na
kuiva barabara katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa wamekuwa wakichukuliwa
na kupelekwa kufanya kazi Ulaya na hivyo kuliacha Bara la Afrika likiendelea kuwa
na uhaba wa wataalam na mabingwa katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.
Kardinali
Polycarp Pengo, ametumia fursa hii, kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita, kwa kuitisha Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika pamoja na ujumbe
wake kuhusu Dhamana ya Afrika, Africae Munus. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu
Uinjilishaji Mpya ni fursa nyingine kwa Mama Kanisa Barani Afrika kuamsha imani na
hatimaye, kupata ufumbuzi wa matatizo, fursa na changamoto mbali mbali zinazoendelea
kujitokeza Barani Afrika.
Hati za Sinodi ya Maaskofu Barani Afrika, Katekisimu
Mpya ya Kanisa Katoliki, Biblia Takatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa ni nyenzi muhimu
katika Uinjilishaji wa kina Barani Afrika. Kardinali Polycarp Pengo ambaye pia ni
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, anabainisha kwamba, Familia ya Mungu Barani
Afrika, ina matumaini makubwa katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Uinjilishaji
Mpya.
Askofu mkuu Carlos Aguiar, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Amerika ya Kusini, anasema kwamba, changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni mpasuko
wa kitamaduni na Mapokeo hai. Ili kufanikisha mchakato wa Uinjilishaji mpya, kuna
haja ya Watoto wa Kanisa kujenga umoja na mshikamano wa dhati na kwamba, kuna matumaini
makubwa katika mchakato mzima wa Uinjilishaji mpya unaoendelea huko Amerika ya Kusini.
Anasema,
waamini walei ndio wadau wakuu wa Uinjilishaji mpya Amerika ya Kusini, kwani wanao
wajibu mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Wanachangamotishwa kumwilisha ndani
mwao, tunu na kweli za Kiinjili kama sehemu ya mchakato wa kuuatakatifuza malimwengu.
Waamini walei wanahitaji majiundo makini mintarafu utambulisho wao wa Kikristo unaogusa
maisha ya mtu binafsi, familia na kama Jumuiya ya waamini. Ni mwaliko wa kutolea ushuhuda
wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya uhalisia wa maisha yao.
Askofu
mkuu Carlos anasema, Uinjilishaji mpya unadai kwa namna ya pekee, umuhimu wa kukuza
na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekukemene pamoja na ulimwengu. Jitihada hizi
hazina budi kuimarishwa katika taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa.
Neno la Mungu, utu na heshima ya binadamu; familia, umuhimu wa zawadi ya maisha, elimu,
maadili na utu wema; uchumi na maendeleo endelevu ya watu; wahamiaji, watu wasiokuwa
na makazi pamoja na wakimbizi; utunzaji bora wa mazingira; haki na amani ni kati ya
kweli zinazopaswa kufundishwa na Mama Kanisa kwa umakini mkubwa miongoni mwa watoto
wake.
Waamini wanaalikwa kumtangaza Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha
yao; kwa kutumia tamaduni pamoja na njia mbali mbali za mawasiliano ya jamii. Watambue
mikakati ya kitaalimungu na shughuli za kichungaji, ili kumwilisha kikamilifu ujumbe
wa Neno la Mungu. Ili kuvuna matunda yanayokusudiwa na Mama Kanisa, kuna haja ya kuchuchumilia:
toba na wongofu wa ndani; umuhimu wa ushiriki mkamilifu na kwa njia ya uchaji Ibada
na Maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, daima kwa kuonesha umoja na mshikamano
na viongozi wa Kanisa mahalia na lile la Kiulimwengu. Familia na Vyama vya Kitume
vijitahidi kushiriki vyema katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wao
makini.
Askofu John A Dew, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Oceania, anasema kwamba, Uinjilishaji ni utume na dhamana ya Kanisa linalopaswa
kutangaza ukweli mfunuliwa, ili watu waweze kusikia, kuelewa na kuamini katika huruma
na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa namna ya pekee kwa njia ya Yesu Kristo.
Kanisa
la Oceania linazidi kukua na kupanuka; miito inazidi kuongezeka na waamini wanaendelea
kuonesha hamu na kiu ya kutaka kumfahamu Yesu Kristo Mkombozi wa dunia kwa njia za
asili pamoja na matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kisasa. Kanisa kwa
upande wake, linaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, kwa kuwawezesha waamini kujenga
uwezo na kujiamini katika masuala ya uongozi na shughuli za kichungaji. Kanisa linaendelea
kuhimiza umuhimu wa utamadunisho, ili mila na desturi njema za waamini wa Oceania
ziweze kukumbatiwa na tunu msingi za Kiinjili; kwa kutambua na kuthamini mambo matakatifu,
zawadi ya maisha bila kusahau ukarimu.
Kanisa Katoliki Oceania linapenda kuwekeza
katika majiundo awali na endelevu miongoni mwa waamini ili waweze kuchangia kwa hali
na mali katika ustawi wa maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, Kanisa halina
budi kujifunga kibwebwe kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa
ari na nguvu mpya zaidi.
Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Shirikisho la
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Asia, amekazia umuhimu wa kuendeleza na kudumisha
majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani; majadiliano na tamaduni
pamoja na watu maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ili kutoa kipaumbele cha
kwanza kabisa cha uwepo wa Mungu katika maisha yao pamoja na kudumisha mshikamano
wa kifamilia. Vyama vya kitume kwa ajili ya familia ni kati ya mafanikio makubwa ya
Kanisa Katoliki Barani Asia, hata kama bado kuna vikundi vinavyotaka kudhoofisha utume
huu ndani ya Jamii.
Familia hazina budi kujengewa uwezo wa kuthamini utakatifu
wa maisha, ili ziweze kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo na kwamba, Jumuiya
ndogo ndogo za kikristo ni nyenzo muhimu sana katika azma ya Uinjilishaji mpya, kwani
zinasaidia kujenga na kuimarisha Jumuiya za Waamini Barani Asia. Itakumbukwa kwamba,
Kanisa Barani Asia linaendelea kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa
na watu wenye misimamo mikali ya kiimani. Kutokana na ukweli huu, Majadiliano ya kidini
yanakuwa ni nguzo msingi katika harakati za ujenzi wa Jamii inayoheshimu misingi ya
haki, amani, upendo na mshikamano.
Kanisa Barani Asia linayaangalia Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani kwa matumaini makubwa, kwani, waamini wanapania kumfahamu zaidi
Kristo; kwa njia ya Neno la Mungu, Sala na Tafakari ya kina pamoja na kutambua kwamba,
Liturjia ni chemchemi ya imani ya Kanisa inayomwilishwa na waamini katika hija ya
maisha yao hapa duniani. Changamoto kubwa kwa Kanisa Barani Asia, ni kuendelea kuwajengea
vijana uwezo wa kutumia njia za mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kutangaza Habari
Njema ya Wokovu.