Askofu Chengula asema: tumethubutu, tumeweza kukusanya kiasi cha sh. mill. 89, sasa
tusonge mbele kulitegemeza Kanisa!
Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania limefanikiwa kuchangisha zaidi ya Sh.Mil.89 katika
harambee iliyoendeshwa na kuongozwa na Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki
Mbeya, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kulitegemeza Jimbo, katika miradi mbalimbali
ya maendeleo badala ya kutegemea sadaka.
Akizungumza katika ibada ya misa takatifu
ya harambee iliyofanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Parokia
ya Mbeya mjini, Askofu Chengula amewashukuru wote waliojitoa kulichangia kanisa ili
liweze kusimama lenye we bila kutegemea misaada,michango na sadaka.
Akizungumza
katika hafla fupi ya chakula cha mchana iliyoandaliwa baada ya misa katika ukumbi
wa Parokia ya Mbeya mjini hivi karibuni, Askofu Chengula alisema hiyo ni mikakati
ya awali ambayo wameiweka na kutokana na mafanikio hayo inaonesha dhahiri kwamba,
Kanisa limethubutu na limeweza hivyo kinachotakiwa ni kuendelea kuweka utaratibu huo
kwa mwakani, ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linajitegemea, ili kuendeleza utume na
mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Askofu
Chengula alisema ni vema kamati hiyo ikaweka utaratibu mzuri wa kuzitumia fedha hizo
kwa ajili ya miradi mbalimbali itakayojenga na kuliimarisha Jimbo. Kamati inapaswa
pia kutoa taarifa za mapato na matumizi mwakani ili waamini na watu wenye mapenzi
mema waweze kupata moyo wa kuchangia zaidi.
"Kumbe tunaweza kama tumethubutu
na huu ni utaratibu ambao tumeuanza sasa,kwa hiyo tunaweza kuendelea na tukasonga
mbele bila kutegemea mahali popote nje ya kanisa,tulipanga kupata zaidi ya Sh.mil.89
lakini, tunaweza kupata zaidi,"alisema.
Akizungumza kwa niaba ya kamati ya
harambee Padre Gabriel Mwakasita alisema kuwa michango hiyo iligawanyika katika ngazi
tofauti na kwamba wamefanikiwa kukusanya fedha taslimu kiasi cha Sh.Mil.66.3 na ahadi
ambazo zitakamilishwa kuwasilishwa ni kiasi cha Sh.Mil.22.9.
Ametaja kundi
lililopo katika daraja la A ni Parokia za Mbeya mjini ambazo zilipangiwa kutoa kila
moja kiasi cha Sh.mil.3 na hivyo kupata jumla ya Sh.Mil.18, daraja B ni Parokia za
Tukuyu, Vwawa, Kyela, Chunya, Itaka na Chunya waliopangiwa kutoa Mil.2 na hivyo kukusanya
jumla ya Sh.mil.10.
Padre Mwakasita ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mwanjelwa
alisema zaidi ya Sh.Mil.13.5 zilipangwa kukusanywa katika Parokia za Mwamabani, Igoma,
Itumba, Mlowo, Pinda, Inyala, Igurus, Simike na Kisa ambazo zilipangiwa kutoa kila
mmoja zaidi ya Sh.Mil.1.5 na kundi D lilitarajiwa kukusanya zaidi ya Sh.Mil.11.2 kwa
kutoa kila mmoja Sh.laki nane.
Mwenyekiti huyo alikuwa akisaidiwa na Katibu
wake Edgar Mangasila alisema, Kundi E lilitarajiwa kukusanya zaidi ya Sh.Mil.2.4 kwa
kila mmoja kutoa shilingi Laki nne ambalo ni Parokia za Ngawala, Kapalala, Gua Sange,
Ipoka, Kambikatoto pamoja na Parokia mpya ya Idiwili.
Aidha alisema Taasisi
za elimu na sekondari zilipangiwa kila mmoja kutoa Sh.Mil.5 na hivyo kukamilisha Sh.Mil.14.5,Mashirika
ya kitawa yalipangiwa kutoa laki tano kila moja na hivyo kukamilisha kiasi cha Sh.Mil.3.8,vituo
vya afya Sh.mil.2.6, mashamba ya jimbo Shilingi laki mbili, Vyama vya Kitume na Jumuiya
za Jimbo vilitoa Shilingi laki tano na kukamilisha Sh.mil.9.3.
Hata hivyo,
Mwenyekiti huyo alisema kamati iligawa jumla ya kadi 40 kwa waamini na watu maarufu
kuomba kuchangia na hivyo wanatarajia wanaweza kuvuka lengo endapo wote watajitoa
kulichangia juhudi za Jimbo Katoliki Mbeya kujitegema ili kuwaletea watu wake maendeleo
ya kweli.
Baadhi ya waamini walionesha kufurahishwa na mafanikio ya harambee
hiyo iliyohusisha Jimbo pekee na kudai kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupata mamilioni
ya fedha endapo lingeshirikisha watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama na serikali
na jamii wakiwemo watu maarufu na mashuihuri, wafanyabiashara na taasisi za dini na
binafsi.