Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania
MUHTASARI WA TAARIFA YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YA UCHUNGUZI WA TUKIO
LILILOPELEKEA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI KILICHOTOKEA SEPTEMBA 2, 2012 KIJIJINI NYOLOLO,
WILAYA YA MUFINDI, MKOANI IRINGA.
UTANGULIZI
Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya serikali iliyoundwa kwa mujibu
wa Kifungu cha 129(1)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977
na Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka 2001. Jukumu
kubwa la Tume ni kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binadamu nchini. Katika kutekeleza
jukumu hilo Tume imepewa mamlaka ya kupokea malalamiko (kwa njia mbalimbali) kutoka
kwa mtu yeyote au kuanzisha uchunguzi wake yenyewe endapo itaona kuna uvunjifu wa
haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Kwa kuzingatia majukumu
hayo, Tume ilianzisha uchunguzi wake yenyewe baada ya vyombo vya habari kutoa taarifa
ya tukio la kifo cha Daudi Mwangosi. Tume iliunda timu ya watu watatu iliyoongozwa
na Mhe. Kamishna Bernadeta Gambishi akisaidiwa na maafisa wawili, Bwana Gabriel Lubyagila
na Bwana Yohana Mcharo. Timu hiyo ilifanya uchunguzi wake kuanzia tarehe 13-19 Septemba,
2012.
Katika uchunguzi uliofanywa, Tume ilizingatia zaidi masuala ya uvunjwaji
wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hivyo basi, Tume ilitilia
maanani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria mbalimbali za nchi na mikataba
ya kimataifa na ya kikanda inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.
Kwa
kuzingatia matakwa ya sheria ya Tume Na. 7 ya mwaka 2001, baada ya uchunguzi huo kukamilika,
Tume imeandaa taarifa yake na kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Taarifa
ya uchunguzi wa Tume imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambazo ni: Maelezo ya viongozi, watendaji na wananchi waliohojiwa Uchambuzi wa taarifa/vielelezo
vilivyopokelewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazohusiana
na masuala ya haki za binadamu Matokeo ya uchunguzi Maoni na mapendekezo.
Kwa kuwa tukio la kifo cha Daudi Mwangosi liligusa hisia
za jamii, Tume imeona ni vyema kukutana na wawakilishi wa vyombo vya habari ili kutoa
taarifa yake.
2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI Katika uchunguzi wake Tume imebaini
kuwa: Tarehe 02/09/2012 Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi (OCD) kufanya mikutano
ya ndani na kuzindua matawi mapya. Lakini jioni ya tarehe 01/09/2012 Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Iringa (RPC), alizuia CHADEMA kufanya mikutano iliyoruhusiwa na OCD ambaye
ni “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka.
Viongozi wa CHADEMA walikuwa na mazungumzo
na Mkuu wa Polisi Mkoa Upelelezi (RCO) na kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa
na mikutano ya hadhara.
Msajili
wa vyama vya siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha
shughuli zao kwa sababu ya sensa.
Wakati
shughuli za uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, RPC alifika katika eneo hilo na
kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe; na kuwa wafuasi wa CHADEMA walipinga kukamatwa
kwa viongozi wao.
RPC
aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika
ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
Baada
ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo; na kuwa marehemu
Daudi Mwangosi alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa bomu
na kufa hapo hapo.
Daudi
Mwangosi aliuwawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la
Nyololo.
Katika
tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo Mwandishi wa Habari wa
Nipashe, Bwana Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya
Mufindi, Bibi Winnie Sanga na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi, Asseli Mwampamba aliyekuwa
akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.
Kutokana
na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi
limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
2.1
Uvunjwaji wa Haki za Binadamu Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
1977, sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu
(Universal Declaration of Human Rights of 1948), Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki
za kiraia na kisiasa (International Covenant on Civil and Political Rights of 1966)
na Mkataba wa mataifa ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu (African Charter on
Human and Peoples Rights of 1981), Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja
haki zifuatazo:
Haki ya kuishi, Haki ya
kutoteswa na kupigwa, Haki ya usawa mbele ya sheria na Haki ya kukusanyika
na kutoa maoni.
CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina
usajili wa kudumu. Chini ya sheria ya vyama vya siasa (Cap. 258 RE. 2002), vyama
vya siasa vyenye usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza
baada ya kutoa taarifa kwa “Afisa wa Polisi” wa eneo husika. Baada ya taarifa kutolewa
chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na “security agencies” (mawakala wa usalama).
2.2
Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora Ili pawepo utawala bora mamlaka zote za serikali
ni lazima zifuate utawala wa sheria. Uchunguzi umebaini kuwa kamanda wa Polisi Mkoa
wa Iringa, Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa majukumu yake
alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a) na (b) na
sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri
ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa “Officer In-charge” wa polisi wa
eneo husika. Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu
ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka,
hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Aidha, hatua ya Msajili wa vyama
vya siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka
kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani
maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1
ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa pia
ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) Kifungu cha 11(a) na (b)
inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya kuingiliwa.
Ibara
ya 8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelezea kwamba Tanzania ni
nchi inayofuata misingi ya demokrasia na Haki ya Kijamii, aidha ibara 18(b) na (c)
ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano (kutoa maoni/habari)
na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake. Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa
na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo Mufindi kwa kuwa waandishi wa habari na
wafuasi wa CHADEMA walizuiwa na Polisi kufanya shughuli zao za kupata habari na za
kisiasa. Huu ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha
au inafifisha uhuru wa habari.
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO Kwa kuzingatia Sheria
ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka 2001 Kifungu cha 15(2)(c)
na 28 Tume inapendekeza yafuatayo: Kamati za ulinzi na usalama
za Mkoa na Wilaya ziwe makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji
wa misingi ya utalawa bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.
Aidha, kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili
masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.
Viongozi wa CHADEMA
na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa
na vyombo hivyo bila shuruti. Pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni
vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Jeshi la Polisi na Msajili wa
Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au
upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Mfano,
Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huo Chama
cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa Kampeni huko Zanzibar. Aidha,
rai ya Msajili wa vyama vya siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA
walishurutishwa na Polisi kutii rai hiyo.
Demokrasia
ya mfumo vya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.
Elimu
ya vyama vya siasa na sheria ya Polisi kuhusu vyama vya siasa itolewe kwa askari polisi
ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.
4.0 HITIMISHO Jukumu
la kulinda amani na utulivu ni wajibu wa kila mtanzania, mkulima na mfanyakazi, viongozi
wa serikali na watumishi wa umma wote wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli wakati wanapotekeleza
majukumu yao ya kila siku. Tume inatoa wito kwa watanzania wote kuheshimu haki za
binadamu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya utalawa bora. Kwa kufanya hivi Taifa
letu litaendelea kuwa na amani na utulivu. Tume inatoa rai kwa jeshi la polisi kutekeleza
wajibu wake mkuu wa ulinzi na usalama wa raia bila kutumia jazba.
Kuwepo kwa
vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukuwa kwa demokrasia na sio kuwa ni upinzani kwa
chama tawala.
Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri R. Manento
MWENYEKITI TUME
YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA