2012-10-11 15:25:51

Maelfu ya waamini na watu wenye mapenzi mema wamiminika kumzika Padre Theodorus Slaats, Maktaba ya Kanisa la Tanzania!






Hatimaye, safari ya mwisho ya aliyekuwa Katibu wa Askofu na mshauri wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Padre Theodorus Johannes Maria Slaats wa Shirika la Roho Mtakatifu imefikia kikomo, tarehe 9 Oktoba, 2012; majira ya saa 8.39 baada ya kumhifadhi katika nyumba yake ya milele ndani ya Kikanisa cha Pango la Bikira Maria.



Padre Slaats ambaye wengi wa waumini na mapadre walizoea kumuita Babu, wengine Padre Silas ama Sailas alikuwa Paroko wa Kanisa la Roho Mtakatifu, Parokia ya Ruanda, Jimbo Katoliki la Mbeya amefariki akiwa na umri wa miaka 82 ambapo ibada ya Misa Takatifu ilianza majira ya saa 4.00 asubuhi na kuongozwa na Mhashamu Baba Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya.



Katika Misa wawakilishi mbalimbali walihudhuria akiwemo Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Anthony Makunde, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu Kanda ya Tanzania, Padre Amandus Kepele, Mwakilishi wa Shirika hilo kutoka nchini Uholanzi, Padre Harry Tullemans Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bwana Abbas Kandoro, Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi "Sugu", wawakilishi kutoka Majimbo ya Iringa, Njombe, Dodoma na Sumbawanga pamoja na na wakuu wa Mashirika ya kitawa ya kike na kiume.



Askofu Chengula katika mahubiri yake alisema, hakuna cha kumpatia Padre Slaats isipokuwa ni kuyaenzi mapendo yake, kuyaendeleza matendo mema aliyowaachia sanjari na kuendelea kumuombea na anaamini kwa imani na matumini ndiyo yaliyowafikisha watu wote kumsindikiza katika safari yake ya mwisho hapa duniani.



Amewashukuru wawakilishi kutoka majimbo ya Iringa, Njombe, Dodoma na Sumbawanga na kwamba wawakilishi kutoka Jimbo la Songea na Mbinga wameshindwa kufika kutokana na ajali mbaya ya gari iliyotokea tarehe 8 Oktoba 2012 kati ya Njombe na Songea na hivyo kugharimu maisha ya Sr. Gabriel wa Mbinga ambaye kitaaluma alikuwa ni daktari.



"Padre Slaats amelala usingizi wa milele sasa hatembei, haongei, viungo vyake vimekauka na baadaye tutamrudisha katika udongo…hili ni fumbo lisilohitajika ambalo binadamu halifahamu kwa undani wake kwani kifo siyo tabia wala hulka,"alisema.



Alisema wakati akiugua na baadaye kuanza kutembelea kiti cha matairi baada ya kupooza, Padre Slaats aliwahi kumtania Askofu Chengula kuwa walikuwa na miili mikubwa lakini sasa hatembei tena na kumtaka yeye (Askofu) naye ajiandae katika safari yake ya mwisho.



Alisema mapato yake na matendo yake mema yatabaki na kuweza kuunda tabia ya watu kwani itabakia kumbukumbu muhimu katika maisha ya wote kwasababu imani,amani na kusameheana na kudumu katika kristo ndiyo mwanzo wa maisha ya mbinguni na jambo la furaha uanza na magumu na hofu ya maisha huku akielekeza kusoma kitabu cha Mwinjili Mathayo 25:34.



Askofu Chengula alisema anamfahamu Padre Slaats akiwa Morogoro na baadaye kumteua kuwa Katibu wake kutokana na matendo yake mema kwani aliishi kama Yesu Kristo kwa kuwasaidia watu wenye ulemavu, ukoma, wasiojiweza na kila mhitaji aliyemwendea!



"Ametufundisha vya kutosha, lakini, tunalishukuru Shirika kwa kutupatia heshima Jimbo letu kukubali kumzika hapa, kwani kadiri ya katiba yenu mngeweza kutukatalia lakini tulikubaliana na mawazo yake ya kuomba arudi jimboni baada ya kutibiwa na mkuu wake wa Uholanzi alimruhusu.



"Pili kabla hajafa ndugu zake walikuja na kuzungumza naye walikubaliana na ombi lake la kuzikwa Tanzania, Jimboni Mbeya ni heshima kubwa na shukrani kwa walio mlea nchini Uholanzi…Padre Slaats Mkaribie mungu na usisahau wenzako tupo nyuma yako tunakuja usije ukafunga komeo la mlango huko mbinguni,"alihitimisha Askofu Chengula kwa majonzi makubwa.



UJUMBE BARAZA LA MAASKOFU TANZANIA (TEC).



Akitoa salamu za pole kwa Askofu Chengula, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Anthony Makunde alisema kwa niaba ya Rais wa Baraza la Maaskofu, Askofu Ngalekumtwa na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Songea, Norbert Mtega wamempa pole sana na kwamba kutokana na majukumu ya kuzika masalia ya mwadhama Kardinali Lugambwa Bukoba wameshindwa kufika vivyo hivyo kwa Askofu Mtega kutokana na ajali iliyochukuwa maisha ya Mkuu wa Shirika la watawa wa kike Jimbo la Mbinga.



Padre Makunde alisema Padre Slaats alikuwa hazina kubwa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kwani angeweza kusema alikuwa ni maktaba ya TEC na hasa pale zilipokuwa zikihitajika kumbukumbu za Kanisa Katoliki za miaka ya 1912 hadi 1972 aliweza kuzipata katika maktaba yake.



"Katika kukamilisha historia na kuadhimisha miaka 40 ya AMECEA sisi kama Baraza hatukufaulu kupata historia yake lakini Baba Slaats alikamilisha kila kitu na sasa tunapoelekea miaka 100 ya Baraza historia yote tangu mwaka 1912 hadi 1972 ni kazi ya mikono yake…tuliipata toka kwake na sasa ametuachia kazi ya kuanzia mwaka 1972 hadi sasa tunaendelea kukamilisha,’alisema.



UJUMBE KUTOKA UHOLANZI



Padre Harry Tullemans kutoka Shirika la Roho Mtakatifu parokia ya Oeffelt nchini uholanzi alisema alikuja nchini Tanzania katika Jimbo la Mbeya ikiwa ni miezi minne imepita tangu amlete Padre Slaats aliyekataa kubakia ulaya na kuamua kuja kufia Afrika, Tanzania, Jimboni Mbeya.



"Daktari wake alimshauri akiwa Ulaya kuwa hasirudi Afrika hataweza kufika na badala yake atafia ndani ya ndege lakini ‘ujeuri’ wake alikataa akasema nitaenda kwa sababu hapa (Uholanzi)ni nyumbani nilipozaliwa lakini hata huko ni nyumbani kuna ndugu, wazazi, watoto na marafiki pia kwa hiyo aliamua kurudi nami nilitumwa kumsindikiza na leo nimerudi akiwa ameshakufa,’alisema Padre Harry.



Alisema ametumwa kuwakilisha Shirika kutokana na mapadre walio wengi kuwa wazee kama alivyokuwa marehemu lakini wanamsubiri siku ya jumamosi ijayo katika ibada ya misaa takatifu maalum kwa ajili ya kumuombea Padre Slaats ambayo itakuwa ni misa ya kipekee.



"Wananisubiri mimi na porojo zangu na jicho kubwa (akimuelekeza video shooter),tutakwenda kuonyesha kila kitu kilichotokea hapa leo na wiki ya kesho wataona mambo makubwa na watashangaa imani yenu kubwa na mlivyojitokeza kumsindikiza mpendwa wenu."



UJUMBE KUTOKA SHIRIKA LA ROHO MTAKATIFU KANDA YA TANZANIA



Mkuu wa shirika la roho mtakatifu Tanzania Padre Amandus Kapele alisema marehemu padre Slaats aliishi kwa upendo na mapadre wenzake na watawa na hivyo hakuweza kufahamika kuwa ni wa kutoka shirika gani na atakumbwa kwa mambo yake mema mengi ikiwemo mwaka 1958 ni miongoni mwa mapadre vijana waliounga mkono jitihada za ukombozi wa Taifa zilizofanywa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kupigania uhuru wa Tanzania enzi za chama kimoja cha TANU.



Alisema Padre Slaats pia alikuwa miongoni mwa mapadre waliounga mkono ‘Africanization’ kuwataka mapadre waafrika kupewa nafasi ya kuongoza, hivyo atakumbukwa kwa mengi aliyoyafanya kwa taifa la Tanzania,watanzania,waumini na watawa wenzake ikiwemo na kutunza kumbukumbu na vifaa vya makumbusho.



UJUMBE WA SERIKALI



Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas kandoro amemuelezea Padre Slaats kuwa alikuwa ni kiongozi mwenzao aliyekuwa na sifa nyingi za uongozi kwani aliipenda injili na watu wote waliwaongoza kwa kulitumikia kanisa kwa moyo wake wote. Alisema watamkumbuka padre huyo kwa mchango wake mkubwa katika kuiongoza jamii ya mkoa wa Mbeya kwani hakuwaunganisha waumini pekee bali wananchi wote kwa sababu alijuwa kanisa ni jamii iliyo pana na hivyo kila mmoja kwa nafasi yake amtendee haki kwa kuwayaendeleza aliyoitendea jamii.



Alisema kama serikali anatoa pole kwa Askofu,mapadre,watawa wa kike na kiume,waumini na wanambeya kwa ujumla kwa kuondokewa na kiongozi,hodari,shupavu,mpenda watu.



MBUNGE WA JIMBO LA MBEYA MJINI



Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini kupitia tiketi ya Chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye pia ni mwanamuziki wa miziki ya kizazi kipya yeye kama mtoto aliyekulia Parokia ya Ruanda walizoea kumuita Padre Slaats: babu na rafiki.



Mimi nimempoteza rafiki yangu kwa sababu nilikuwa ninampotembelea hata nilipopata ubunge alikuwa akinikosoa na kuniambia hapa Chama chenu kimekosea na hapa mmefanya vyema na hakuwa akiniita mbunge bali aliniita ‘MCHADEMA’…Jumapili ya tarehe 16 Septemba 2012 nilimtembelea kumtakia hali na tulizungumza naye kwa kweli ni pigo kwa Jimbo ni pigo kwa watanzania wote,"alisema.



Mbunge sugu ambaye pia alishiriki katika mkesha wa kumuombea Padre Slaats uliofanyika katika Kanisa la Roho Mtakatifu, Parokia ya Ruanda, alitoa rambi rambi mifuko 20 ya Saruji kwa ajili ya kujengea kaburi la Padre Slaats.



Katika safari hiyo ya mwisho maelfu ya watu walijitokeza kumzika kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya huku kwaya zikiimba nyimbo za kabila la kiswafwa ambazo inadaiwa alipenda sana kuzisikiliza na kuziimba huku wao wakimwita mwene(chifu).



Hivyo ndivyo nyota ya Padre Slaats ilivyozima ghafla katika uso wa dunia bali tunaamini kiroho yupo nasi daima.raha ya milele umpe ee! bwana na mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani padre Slaats amina.



HITIMISHO LA ASKOFU CHENGULA



Hata hivyo Askofu Chengula amehitimisha kwa kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas kandoro na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ambaye ni mwamini wa Kanisa la Ruanda kwa kushiriki katika maziko hayo na amewataka viongozi wa chama na serikali kushirikiana na kanisa siyo katika shida tu bali hata katika mazuri.



"Ninawashukuru Mkuu wa Mkoa na Mbunge na viongozi wa madhehebumbali mbali, ninakumbuka Mkuu wa Mkoa ulinisaidia sana katika kuhakikisha shule ya sekondari ya St.Francis haifungwi wakati wa mgogoro na leo umefika katika kifo, tushikamane mikono hata wakati wa raha pia, Mbunge tuombeane muongoze vizuri,msitusahau wapiga kura wenu mtukumbuke katika kutuletea maendeleo,"alisema.



Askofu Chengula alisema Mapadre na Masista ni jukumu lao kuongea na viongozi wa vyama na serikali katika kuwasaidia na kuwaunganisha na wananchi bila kujali imani za kidini wala itikadi za kisiasa,rangi wala kabila,"nanyi wa madhehebu asante sana,msiwe na wasi wasi Padre Slaats amekwenda kwa mungu."











All the contents on this site are copyrighted ©.