Chuo Kikuu cha Wasalesiani kufungua Mwaka wa Masomo 2012- 2013: kwa kutafakari juu
ya ushirikiano wa kimataifa!
Mheshimiwa Professa Andrea Riccard, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa nchini Italia,
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya ufunguzi wa Mwaka wa Masomo, kwa
mwaka 2012- 2013, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani, kilichoko mjini Roma, hapo
tarehe 16 Oktoba 2012 majira ya asubuhi. Tukio hili pia litahudhuriwa na Mheshimiwa
Padre Pascual Chaves Villanueva, Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco.
Professa
Andrea Riccard anatarajiwa pia kutoa hotuba ya kufungua mwaka wa masomo pamoja na
medali kwa majaalimu na wanafunzi waliopeta katika nyanja mbali mbali za masomo na
taaluma katika mwaka wa masomo uliopita. Itakumbukwa kwamba, Professa Riccard, kunako
mwaka 1968 alianzisha Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambayo kwa sasa imeenea katika
nchi sabini duniani. Ni Jumuiya inayopania kudumisha na kuendeleza ushirikiano wa
kimataifa hasa zaidi katika mchakato unaopania kudumisha misingi ya haki, amani na
upatanisho wa kitaifa.
Professa Andrea Riccard amechangia kwa namna ya pekee
katika harakati za kupatanisha mataifa mbali mbali yaliyojikuta yakiingia katika kinzani
na migogoro yakivita. Anakumbukwa sana kutokana na mchango wake uliosaidia kufanikisha
utiaji wa sahihi wa mkataba wa amani nchini Msumbiji, ambao kwa sasa unasherehekea
miaka ishirini, changamoto ya kukuza na kudumisha misingi ya uhuru na demokrasia kama
wanavyohimiza Maaskofu Katoliki kutoka Msumbiji. Amesaidia harakati za amani huko
Guatemala, Pwani ya Pembe na Guinea.
Ni mwandishi maarufu wa vitabu na kati
ya vitabu vyake ni kile cha Wasifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, kilichochapishwa
katika lugha nane za kimataifa nchini Italia, kunako mwaka 2011.