2012-10-10 10:07:07

Muadhama Kardinali Pengo ahutubia Sinodi


Mababa wa Sinodi kwa ajili ya Uinjlishaji Mpya, wanaendelea kushirikishana hali halisi, na uzoefu na ushauri kutoka maeneo yao, kwa mujibu wa utaratibu uliotolewa. Jumatatu kati ya waliohutubia sinodi ni muadhama, Askofu Mkuu Polycarp Kardinali Pengo wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar,SECAM, alizungumza kwa niaba ya mabaraza hayo.
Kardinali aliitoa muhtasari wa historia ya Uinjilishaji Afrika akisema , historia inathibitisha Uinjilishaji barani Afrika ni tangu mwanzo wa Kanisa, "Matendo ya Mitume ; 8,26, 39, mnatajwa uinjilishaji uliofanywa na Philipo nchini Ethiopia.
Ingawa Ukristu uliingia mapema Kaskazini mwa Afrika, juhudi hizo hazikujipenyeza kwa haraka katika eneo la Kusini mwa Afrika. Na hivo kwa wakazi wa Kusini mwa Afrika, inaweza kwao kuwa vigumu kutambulisha kati ya Uinjilishaji mpya na uinjilishajiwa zamani. Hata hivyo bado inafaa kuzungumzia Uinjilishaji mpya kwa Afrika, kwa kuanza na changamoto zilizotajwa na Papa Paulo V1 mwaka 1969, aliyewataka Waafrika kujiinjilisha wenyewe .Pamoja na kupita kwa miaka bado , hata leo wito huo kwa Kanisa Afrika, unahitaji kuitikikiwa kwa kishindo. Ni wito kwa Makanisa Afrika kujenga ukomavu katika kazi hii ya kuinjilisha.

Ili kutoa jibu kwa changamoto hii, Kanisa Afrika liliona umuhimu wa kuwa na mfumo wa mmoja wa kichungaji ngazi za kitaifa na kimkoa, kwa ajili ya uhamasishaji mpya kwa kazi hii ya uinjilishaji . Na hivyo Kanisa lilianzisha SECAM, mwaka 1969, kwa lengo la kukuza na kudumisha umoja, katika ushirikiano na utendaji wa pamoja kwa Mabaraza yote ya Afrika na visiwa vinavyozunguka Afrika. Udumishaji wa juhudi hizo zenye kuhamasisha kazi za kichungaji leo hii, imekuwa ni wajibu wa waaamini wote wa waafrika, Maaskofu, Mapadre, Watawa wanawake kwa wanaume, na makatekista na walei..
Na kati ya kazi za kuonekana katika juhudi hizi za uinjilishaji mpya ni uanzishwaji wa jumuiya dogodogo za Kikristu ambazo zimekuwa vituo hai vya uinjilishaji wa kina katika maisha ya kila siku ya kanisa barani Afrika.
Kardinali Polycarp Pengo, pia aliangalisha katika changamoto zinazokwamisha uinjilishaji na uzamishaji wa imani barani Afrika . Kati ya changamoto hizo ni mmomonyoko wa maadili ya utamaduni wa mwafrika, kunakotokana na kasi yamwingiliano wa tamaduni kutoka nje katika mfumowa utandawazi. Na hivyo inakuwa vigumu kwa Wakristu barani Afrika kupambanua kati ya mambo ya kipagani ya nchi za nje na hasa Ulaya na Ukristu . Na kumekuwa na mwelekeo wa Ukristo kuchukuliwa pia kama utamaduni wa kigeni.
Aidha thamani ya utamaduni mahalia kuheshimu maisha unapambanishwa na utendaji wa nchi za magharibi usio thamini maisha. Pamoja na changamoto nyingi toka nje zinazodharirisha maadili ya mwafirika, inakuwa vigumu kwa watu mahalia kupata utambuzi wa ukweli wa maisha.
Kardinali Pengo aliendelea kutaja maovu yanayodharirisha kazi za Uinjilishaji , ikiwemo udhaifu wa kurubuni haraka na kuingia katika mizozo na machafuko ya kikikabila yenye kujirudiarudia, maradhi, usafirikshaji haramu wa watu, mauaji ya kinyama na madhulumu kwa watoto na makundi madogomadogo manyonge kama wanawake .
Pia ameitaja changamoto nyingine inayokabili uinjilishaji barani Afrika ni utendaji wa Waislamu wasiovumilia wengine. Katika hili, uinjilishaji umekuwa ni mgumu hasa uwepo wa majadiliano wazi , katika maeneo yenye kuwa na Waislamu wengi. Sehemu hizo makundi madogomadogo kiimani, hutenda kwa unyamavu mwingi na huishi na hofu za kushambuliwa iwapo watajaribu kueneza imani yao. Na waislamu hao wasiovumilia wengine, hawako tayari kusikiliza wengine na kuukubali ukweli .
Hivyo, Uinjilishaji mpya barani Afrika , unahitaji wainjilishaji waliokomaa katika imani, kutimiza zaidi ya wito wa Paulo V1, kwamba waafirika ni lazima kujiinjilisha wenyewe, kama inavyoonekana sasa kwamba , kuna Waafrika wamisionari katika mataifa ya magharibi, Marekani na Ulaya.
Pia kujali kwamba, katika juhudi hizo za kwenda kuinjilisha nje ya Afrika, zisiwe na sababu za kujitafutia faida binafsi kwa mgongo wa Kanisa na uinjilishaji wa kweli.
Kwa kuzingatia yote haya , Sinodi kwa ajili ya Uinjilishaji mpya, ni tukio linalopokelewa kwa mikono miwili hata barani Afrika. Ni kama ulivyo wito wa Papa Benedikto XV1, kwa Afrika , kusimama imara na kuuchukua mkeka na kutembea (Afrika Munus No. 148)
Na kwa kufanywa upya katika imani, kupitia sinodi hii, Kardinali Polycarp Pengo ameonyesha imani yake kwamba , Afrika itaweza kupambana na changamoto zake kwa ushupavu zaidi leo hii.
Kwa kuangaziwa na nyaraka mbili za matokeo ya Sinodi maalum kwa Afrika, ”Kanisa barani Afrika ya mwaka 1995” na waraka wa ”Dhamana ya Afrika , 2011” na pia Kateksimo ya Kanisa Katoliki, na hati yenye ufupisho wa mafundisho sadikifu ya Kanisa , Kanisa la Afrika linatazamia mambo mengi mazuri kutoka sinodi hii ya Unjilishaji mpya-








All the contents on this site are copyrighted ©.