Zaidi ya watu millioni 870 wanakabiliwa na utapiamlo duniani
Taarifa ya Umoja wa Mataifa inaonesha kwamba, kwa sasa kuna zaidi ya watu millioni
mia nane na sabini, wanaokabiliwa na tatizo la utapiamlo kutoka sehemu mbali mbali
za dunia, lakini, bado kuna uwezekano wa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia.
Hayo yamo kwenye taarifa za Mashirika ya Chakula, Usalama wa Chakula Duniani na Mpango
wa Chakula Duniani.
Waathirika wakuu wa baa la njaa ni wale wanaoishi katika
Nchi changa zaidi duniani, wanaokadiriwa kufkia zaidi ya watu millioni mia nane na
hamsini na mbili. Hawa ni jumla ya asilimia kumi na tano ya idadi ya watu wote wanaokabiliwa
na baa la njaa duniani. Watu wengine millioni kumi na sita, wanaishi katika nchi zilizoendelea
zaidi ulimwenguni.
Inasikitisha kuona kwamba, hata katika ulimwengu unaotaliwa
na kwa kiasi kikubwa kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia bado kuna watoto zaidi
ya millioni mia moja wenye umri chini ya miaka mitano, wanasumbuliwa na utapiamlo
wa kutisha. Hali hii kwa kiasi kikubwa anasema Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi
mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kwamba, inachangia kudumaza
maendeleo ya watoto hawa: kijamii, kiuchumi na kiutu! Utapiamlo bado unaendelea kusababisha
vifo kwa zaidi ya watoto millioni mbili nukta tano kila mwaka.
Haya yote ni
matokeo ya myumbo wa uchumi kimataifa, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia
juhudi za kukwamua uchumi katika Nchi zinazoendelea duniani, kwa kuzijengea uwezo
wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa ajili ya watu wake.
Licha ya changamoto
zote hizi, Umoja wa Mataifa una imani kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia Malengo
ya Millenia, ifikapo mwaka 2015 kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu wanaoteseka
kutokana na baa la njaa duniani. Kuna idadi kubwa ya watu wanaoishi Barani Asia wanateseka
kwa baa la njaa, lakini hali hii inazidi kuongezeka kwa kasi Barani Afrika. Umefika
wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo, sanjari na
kuwawezesha wakulima kuboresha kilimo ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.
Licha
ya baa la njaa kuendelea kutesa watu wengi zaidi duniani, lakini pia kuna watu zaidi
ya billioni moja nukta nne wanasumbuka kutokana na kuwa na uzito wa kupindukia, kiasi
cha kuhatarisha maisha yao. Juhudi za makusudi hazina budi kufanywa na Jumuiya ya
Kimataifa ili kuokoa maisha ya watoto wanaosumbuliwa na utapimlo wa kutisha, kwa kuwekeza
katika kilimo na elimu sanjari na kukuza uwezo wa uzalishaji kiuchumi, ili kupunguza
baa la njaa na hatimaye kufuta kabisa tatizo la utapiamlo.