2012-10-09 10:43:22

Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa Uganda na changamoto zake!


Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala Uganda, ameiomba Serikali ya Uganda wakati huu inapoadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Waingereza, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa bila masharti.

Askofu mkuu Lwanga ameyasema hayo, Jumapili iliyopita wakati wa mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Rubaga. Anasema, tukio hili linaweza kuonesha kwa namna ya pekee mchakato unaopania kujenga na kuimarisha amani ya kweli, upatanisho wa kitaifa sanjari na haki.

Kuna baadhi ya wafungwa wa kisiasa ambao wanaendelea kutumikia vifungo vyao kinyume cha haki msingi za binadamu. Kwa sasa Serikali ya Uganda inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na matumizi mabaya ya madaraka walioyokabidhiwa na umma; uvunjifu wa haki msingi za binadamu, kuporomoka kwa sekta ya elimu hali inayopelekea ongezeko kubwa la idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika; rushwa na ufisadi.

Askofu mkuu Lwanga anaichangamotisha Serikali ya Uganda kuhakikisha kwamba, inaipatia ufumbuzi wa kudumu migogoro yote ya ardhi inayoendelea kufuka moshi nchini humo kwa sasa. Kanisa Katoliki pia limejikuta likijitwalia maeneo makubwa ya ardhi, wakati ambapo kuna umati mkubwa wa Wananchi wa Uganda wanaoendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na maradhi.

Anasema, mustakabali wa wananchi wa Uganda bado uko mikononi mwa Waganda wenyewe, changamoto na mwaliko wa kusahau ya kale na kuanza kuganga yaliyopo na yale yajayo mbele yao, kwa imani na matumaini makubwa zaidi. Kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa Uganda ni tarehe 9 Oktoba 2012.

Sherehe hizi zimehudhuriwa na viongozi wa Serikali kutoka nchi mbali mbali Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.