2012-10-09 09:52:44

Benki ya Mkombozi inapania kumkomboa na kumwinua mtanzania katika maisha yake!


Askofu Beatus Kinyaiya, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Mkombozi, inayomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainishwa kwamba, Benki ya Mkombozi inaendelea kupata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya ya watu wanaojiunga na Benkii pamoja na ongezeko la watu wanaowekeza mitaji yao. RealAudioMP3

Lengo la Baraza la Maaskofu kuanzisha Benki ya Mkombozi ni kumwinua mtanzania mwenye kipato cha chini kwa kumwezesha kwa njia ya mikopo inayopania kumjengea uwezo kiuchumi. Lengo hili litaweza kufikiwa ikiwa kama kasi ya kupanuka kwa Benki ya Mkombozi itandelea kama inavyojionesha kwa sasa.

Ni Benki inayojali na kuzingatia maadili ya kazi, uwajibikaji, nidhamu na uaminifu, daima wafanyakazi wake wakihamasishwa kuchapa kazi kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Tanzania katika ujumla wake.

Taarifa za Benki ya Mkombozi zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2011 imejipatia faida ya kiasi cha shilingi millioni 37. Benki inaendelea kuwahamasisha watanzania kuwekeza katika Benki hii ili iweze kukuza mtaji wake hadi kufikia kiasi cha shilingi Bilioni 15. Mafanikio ya Benki ya Mkombozi ni kutokana na uadilifu, ufanisi na moyo wa kujituma.

Benki ya Mkombozi inakabiliana na changamoto mbali mbali katika masuala ya kiteknolojia pamoja na kuendelea kujipanua sehemu mbali mbali za Tanzania. Wakopaji wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanarudisha mikopo yao kadiri ya utaratibu ulioweka ili Benki ya Mkombozi iendelee kutoa huduma kwa Watanzania wengi zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.