Wanandoa wenye ugumba, kubalini kuupokea mpango wa Mungu katika maisha yenu!
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, napenda kukualika tuendelee tena na tafakari yetu
ya juma lililopita kuhusu matatizo yatokanayo na ugumba, ila leo tukazie zaidi ushauri
tunaoweza kuwapatia wanandoa wagumba. Kanisa linaposikitika
na wale wanandoa wagumba, linawasihi wapokee mipango ya Mungu kwa matumaini kama katika
hali ya kawaida haiwezi kutibika bila kuvuruga muungano wa tendo la ndoa na uzazi.
Hili liwasaidie wazazi kukumbuka daima kuwa mtoto ni zawadi toka kwa Mungu. Wao ni
washiriki katika mpango huu lakini hawana madaraka ya mwisho kuhusu mtoto. Ni katika
misingi hii Kanisa halitabadilisha uamuzi wake kuhusu kuhusu uharamu watoto wa kutengeneza
ndani ya maabara. Kanisa linawaalika wanandoa wagumba wajifunze kuasili (adopt)
watoto hasa wale wasio na wazazi rasmi wa kuwalea kama wanaoishi katika mazingira
hatarishi. Wapo watoto wengi waliopo kwenye mazingira magumu ya kiuchumi, kijamii
na kiroho wakati huo huo, wapo wazazi wagumba wenye hali nzuri za kiuchumi na kijamii
ambao wangeweza kuwaasili. Hata hivyo kuasili watoto kunapaswa kuendana na taratibu
za kisheria zilizokubaliwa na jamii ili kuondoa ukatili unaweza kujitokeza kwa watoto
hawa na kujenga mahusiano mazuri kati ya waliokuwa wazazi wao na wale wazazi wao wapya. Wana-ndoa
wagumba wanaalikwa pale inapowezekana wajiingize zaidi katika huduma za upendo kwa
kuanzisha: vyama vya kitume kwa ajili ya malezi kwa watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi; vikundi au asasi za kuwahudumia wenye shida mbalimbali hasa watoto, wagonjwa,
wazee na wenye shida mbalimbali. Hii itawafanya wasijisikie wapekwe sana pia wawekeze
nguvu zao za malezi kwenye makundi mengine kama wanavyofanya baadhi ya makasisi na
watawa wanaojitoa kwa njia mbalimbali kuhudumia wahitaji zaidi ndani ya Jamii. Daima,
tukumbe kuwa japo uzazi ni moja ya malengo muhimu ya ndoa lakini pia wanandoa wanaalikwa
kutimiza malengo mengine kama umoja na uaminifu katika maisha ya ndoa. Hivyo ugumba
usiwe sababu ya kuvuruga umoja na uaminifu huu unaowanufaisha wanandoa. Usiwe sababu
za talaka, na mahusiano mengi mabaya kati ya wanandoa kama jamii nyingi duniani zimefanya. Kutoka
Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi
ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano- Roma.