Utukufu wa fumbo la Msalaba katika maisha na utume wa Kanisa
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Msalaba ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha
na matumaini. Ni kwa sababu hii, Mama Kanisa anaona fahari juu ya Msalaba wa Bwana
Yesu Kristo. Kuna baadhi ya watu hawajaelewa vema nini maana na ukuu wa msalaba katika
maisha yao. Ni vizuri kutafakari walau kwa ufupi juu ya msalaba. Utakumbuka pia
mwaka jana wakati wa maadhimisho ya ishirini na sita ya siku ya vijana kimataifa,
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, pamoja na zawadi zingine, aliwagawia vijana
wote Msalaba. Msalaba una maana gani kwako! Keti kwa utulivu nikupe siri ya Msalaba
na ishara ya msalaba. Msalaba ni ishara ya wokovu wa mwanadamu na wokovu wa ulimwengu
mzima. Baada ya dhambi ya wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva, mwanadamu na ulimwengu
mzima ulitekwa katika utawala wa utumwa wa mzushi, shetani. Kristo kwa sadaka yake
Msalabani anamuokoa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi, kutoka katika utumwa
wa kuasi, kutoka utumwa wa kiburi. Wokovu huo unamrudishia mwanadamu na ulimwengu
hadhi yake ya awali, nawe unaalikwa kuuenzi na kuuishi msalaba huo ili kushiriki katika
kuikamirisha kazi ya ukombozi. Kama unavyouona msalaba una pembe nne. Hii ni ishara
kuwa msalaba umerekebisha mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu, viumbe vyote na ulimwengu
kwa ujumla. Msalaba unarudisha ule utaratibu wa awali na makusudio aliyokuwa nayo
Mungu wakati akiuumba ulimwengu. Msalaba unaurudishia ulimwengu uzuri wake asilia.
Lakini ukamirifu wa uzuri na utaratibu huo unategemea kushiriki kwako katika kuuishi
msalaba huo wa Kristo. Kumbe unaalikwa wewe pia kujitoa sadaka kila siku kwa ajilia
ya wengine, kwa ajili ya wahitaji, kwa ajili ya kupambana na nguvu za giza, kupambana
na mzushi shetani. Jitoe sadaka kama harufu nzuri ya ubani ili kufukuza mbali kila
uovu unaoinyemelea dunia. Ishi ukristo wako bila aibu, bila woga. Kabla ya chakula
au kabla ya shughuli yoyote anza kwa njia ya msalaba na sala ya kweli na ya rohoni,
ili kuiendeleza sadaka ya Kristo na kuutukuza ukuu wa msalaba. Msalaba na ishara ya
msalaba viwe ni kinga na ngao yako kupambana na mabaya. Msalaba ni muhtasari wa
historia ya mwanadamu, muhtasari wa historia ya wokovu. Ndio sababu baada ya kuja
kwa Kristo wana dunia wamegeuza namna ya kuhesabu nyakati: kabla ya Kristo na baada
ya Kristo. hii ni sababu Kristo ndiye kiini cha historia, ndiye mwenye historia na
ndiye mwenye kuigawa historia. Kristo anaikamirisha historia ndani yake, katika msalaba
wake. “Tazama ya kale yanafanywa kuwa ni mapya”. Kristo anayaweka kwa pamoja na katika
mahusiano na utaratibu bora, mambo ya kale, ya sasa na yajayo. Ni katika msalaba wa
Kristo tu, ndipo matukio yote duniani yanapata umaana wake. Msalaba ni ishara ya
upendo aliyonao Mungu kumtoa mwanaye wa pekee kukukomboa wewe. Ni ishara ya upendo
aliyonao Kristo kukubali kuteseka msalabani kwa unyenyekevu na utii ili kukukomboa
wewe. Unapoutazama msalaba, unapopiga ishara ya msalaba, kumbuka kuwa mnyenyekevu
na mtii kwa mapenzi ya Mungu. Msalaba ni kiungo cha wanadamu wote ndani ya Utatu
Mtakatifu. Kristo asema “ntakapoinuliwa juu, ntawavuta watu wote waje kwangu”. Mbele
ya msalaba wa Kristo umoja kati ya watu unapatikana, umoja kati ya madhehebu na dini
mbalimbali unapata mhimili na nguzo thabiti. Msalaba wa kristo unakuvuta wewe na jirani
zako wote kuwa pamoja na kuwa na umoja ndani ya Kristo. Msalaba ni kiti cha enzi
cha ufalme cha Kristo aliye Bwana. Ni kiti chake cha enzi maana ni katika msalaba
huo ndipo anapomshinda shetani na nguvu zote za giza. Ni katika msalaba hapo ndipo
linapozaliwa Kanisa kwa damu na maji. Kupitia nguvu ya msalaba Kristo anautawala ulimwengu.
Mbele ya msalaba unapata hukumu yako mwenyewe, ya kuwa ni kwa dhambi zako yeye ametundikwa
msalabani hapo, na ni kutoka katika kiti hicho cha msalaba wewe utapata hukumu yako
ya mwisho, kwa kuzingatia jinsi ulivyoishi kufuatana na fumbo la msalaba. Uenzi
na kuutukuza ukuu wa Msalaba huo, chanzo, kiini na kilele cha historia ya mwanadamu
na wokovu. Mpaka juma lijalo, ni sauti ya kinabii, Celestin Nyanda.