2012-10-08 10:11:22

Simameni kidete! Msiyumbishwe na shinikizo la utamaduni wa kifo kwa kukumbatia dhana ya utoaji mimba!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland, Jumapili iliyopita, tarehe 7 Oktoba 2012 limeadhimisha siku ya zawadi ya maisha sanjari na maadhimisho ya mwezi wa kuombea maisha. Maaskofu katika barua yao ya kichungaji wanabainisha kwamba, Jamii inawajibika kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa tumboni mwa mama yake.

Hizi ni juhudi za Kanisa nchini Ireland wakati huu Serikali ya nchi hiyo inapojiandaa kutoa jibu muafaka kuhusu hukumu ya haki za binadamu iliyotolewa na Mahakama ya Haki za binadamu Jumuiya ya Ulaya, kwa kutaka kushinikiza uwepo wa sheria ya utoaji mimba, pale inapobainika kwamba, maisha ya mama mjamzito yako hatarini. Itakumbukwa kwamba, Ireland na Malta ndizo nchi pekee Barani Ulaya ambako utoaji mimba ni kosa la jinai.

Maaskofu wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuthamini, kulinda na kutetea zawadi ya maisha ya binadamu, kwa kujikita zaidi katika upendo unaowajali wengine, kama nyenzo ya kutajirishana. Binadamu anapaswa kutambua kwamba, uwepo wake ni kwa ajili ya mapenzi ya Mungu na wala si jitihada zake binafsi. Jamii inatambua kwamba, maisha ni jambo takatifu, changamoto ya kuheshimu tunu hii, katika kila hatua ya ukuaji wa mwanadamu, hadi pale mauti ya kawaida inapomfika mtu kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Maaskofu Katoliki wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchagua zawadi ya maisha. Wanapenda kuchukua fursa hii kuwaomba wanasiasa na viongozi wa Serikali kusimama kidete dhidi ya shinikizo la kutaka kuhalalisha sheria ya utoaji mimba, kwa kuboresha huduma kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi.

Kuruhusu uwepo wa sheria ya utoaji mimba kwa mara ya kwanza nchini Ireland litakuwa ni pigo kubwa kwa nchi kwa sasa na kwa siku za usoni. Viongozi watambue kwamba, maisha ya binadamu ni kito cha thamani ya hali ya juu kabisa, kumbe wanapaswa kuchagua maisha badala ya kuyabeza kwa kukumbatia utamaduni wa kifo!







All the contents on this site are copyrighted ©.