2012-10-08 14:57:15

Mpango wa uzazi kwa njia ya asili unahitaji busara na usafi wa moyo!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Karibu tena tuendelee na tafakari yetu ya juma lililopita kuhusu mpango wa uzazi kwa njia ya asili kama njia mbadala ya kuondokana na vizuia mimba. Ni ukweli kuwa kukutana kimwili kwa wanandoa ambayo ni sehemu muhimu katika mahusiano yao hubeba jukumu la uzazi na malezi. Hata hivyo, busara yao katika kupanga uzazi inapaswa isiache nje matendo ya upendo. Kwa mfano si sahihi kukabiliana na hali mbaya ya umaskini kwa kukumbatia utamaduni wa kifo na ukiukwaji wa maadili na utu wema
Afya ya kimwili, kisaikolojia, kiuchumi na fursa ya ajira kwa ajili ya familia inapodai kutafakari mapenzi ya Mungu katika uzazi ni sahihi kabisa. Tunaweza kusema Mungu mwenyezi aliliona hili na kuliweka kwenye maumbile ya mwanamke. Na leo, hili limekuwa rahisi zaidi katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo duara la asili linaweza kufahamika zaidi kuliko miaka ya nyuma.
Mpango wa uzazi kwa njia asili unadai fadhila ya usafi wa moyo toka kwa wana-ndoa wote. Fadhila hii, itawasaidia kukutana wakati mwafaka na kujikatalia kukutana wakati usio mwafaka kwa faida ya familia yao. Pale wanapotamani kupumzika uzazi basi watakutana wakati wa kiangazi ambapo hakuna rutuba ya uzao. Katika mazingira haya hatuwezi kusema wamekataa kuwa wazazi bali wamekubali kuwa wazazi katika mpango uliowekwa na Mungu mwenyewe.
Mpango wa uzazi kwa njia ya asili na vizuia mimba vyote vina nia moja yaani kuzuia uzazi lakini hutofautiana katika njia. Vithibiti mimba haviheshimu maumbile. Wahusika hutaka kutimiza tu haja na vionjo vyao hata kama hakuna kujitoa moja kwa moja kwa upendo. Katika mpango wa asili kuna jengeka fadhila nyingine ya masikilizano.
Mpango wa uzazi kwa njia ya asili hudai ukomavu, majadiliano ya kina na masikilizano. Hudai kusikilizana kwa uvumilivu na hivyo, kuwa tayari kujikatalia na kusubiri wakati mwafaka. Ndio maana waswahili husema nyumba hujengwa kwa matofali bali familia hujengwa kwa masikilizano.
Nilipoanza kusikia kuhusu fadhila ya usafi wa moyo nilijua inawahusu makasisi na watawa tu kumbe ni kila mmoja katika nafasi yake. Tena fadhila ya usafi wa moyo hupata chimbuko lake katika upendo ndio sababu sasa naanza kuwaelewa wale akina mama waliokuwa wananiambia haiwezekani Padre kupanga uzazi kwa njia ya asili kwani mwenzangu hayuko tayari kuambiwa leo tujikatalie pale anapojisikia kukutana nami kimwili.
Hapa tunaweza mapungufu yao ni upendo kama upendo ungetawala na masikilizano yangekuwa rahisi. Ni muhimu wanandoa wajenge fadhila za upendo na masikilizano mithili ya Kristo kwa Kanisa lake alilolipenda upeo hata akawa tayari kutoa maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa dunia.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.









All the contents on this site are copyrighted ©.