Jitokezeni kutoa maoni yenu kuhusu mchakato wa Katiba Mpya ya Tanzania
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, linaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote
wenye mapenzi mema kujitokeza kwa wingi ili kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya ya
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Wito huo umetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Yuda
Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza.
Kati ya mambo
yanayopaswa kuzingatiwa ni kuangalia pia ukubwa wa Serikali, kwa kuangalia zaidi:
tija, ufanisi na gharama za uendeshaji wa Serikali ikizingatiwa pia masuala ya uchumi.
Ni jukumu la Katiba kuanisha mambo haya.
Kuna haja pia ya kuangalia nafasi
za ubunge wa kuteuliwa na viti maalum na kwamba, wananchi wawe na dhamana kikatiba
ya kuwawajibisha wabunge wao. Madaraka ya Rais kuhusu uteuzi wa viongozi wa juu yana
wigo mpana mno unaoingilia mihimili mingine ya dola. Madaraka haya yanaweza kutumiwa
vibaya na uwajibikaji wa viongozi hao walioteuliwa ukawa hafifu. Kuna haja kwa Katiba
Mpya ya Tanzania kupunguza madaraka haya au kuweka udhibiti wake kisheria. Vigezo
viwe wazi na uwamuzi ufikiwe kwa njia shirikishi.
Kuna haja ya kuwa na Tume
huru ya uchaguzi na tume nyingine ili kuepusha hali ya wananchi kukosa imani na tume
hizi na hivyo kuendelea kuibua malalamiko kwa Serikali. Uundwaji wa Tume ufanyike
kwa uwazi na kwa kutumia njia shirikishi.
Serikali haina dini ndiyo nguzo ya
umoja na amani ya nchi ya Tanzania. Uhuru wa kuabudu unapaswa kuheshimiwa na kulindwa.
Kuna haja ya kuwa makini katika suala hili kwani mahali ambapo umetumika vibaya, umekuwa
ni chanzo cha mtikisiko wa katika familia; chanzo cha kukashifu dini nyingine, uharibifu
wa mali za watu pamoja na kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi.
Msukumo
wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi ndani ya Mfumo wa mahakama za nchi siyo haki kwa hiyo
isiwemo katika Katiba kwa kuwa ni mambo ya kidini na huenda ikawa ni njia ya kuipeleka
Tanzania katika ukiukwaji wa dhana ya kuwa Serikali haina dini.
Kuhusu maoni
ya Muungano: wananchi watoe maoni yao kwa kuangalia sababu zilizopelekea Waasisi wa
Muungano kuuanzisha. Watu waangalie pia faida na hasara za Muungano. Wazo la Muungano
wenye Serikali tatu ni hoja inayoweza kutolewa maoni, ukiangalia Katiba ya sasa ya
Zanzibar.