Hali bado ni tete kati ya wachimba migodi Afrika ya Kusini!
Askofu Kevin Dowling wa Jimbo Katoliki la Rustenburg, Afrika ya Kusini anasema kwa
sasa hali ni tete sana Afrika ya Kusini kutokana na wachimba migodi wapatao elfu kumi
na mbili kufukuzwa kazi na baadhi ya wachimba migodi hao kuamua kuendelea na kazi,
kutokana na mgomo usio halali uliofanyika kunako tarehe 12 Septemba, 2012.
Wafanyakazi
wote ambao hawakujitokeza kwenye kikao cha nidhamu, kilichoitishwa na Kampuni ya Amplats,
moja ya makampuni makubwa duniani yanayojihusisha na uchimbaji wa madini ya Platinum,
wamefukuzwa kazi kuanzia tarehe 5 Oktoba 2012. Wafanyakazi wanadai ongezeko kubwa
la mishahara kama waliyopewa wenzao kwenye machimbo ya Marikana.
Askofu Kevin
Dowling anasema kwamba, Jimbo lake limelazimika kusitisha baadhi ya huduma kutokana
na kinzani na machafuko yanayoendelea kujitokeza katika maeneo mbali mbali Jimboni
humo. Baadhi ya watu wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na mapambano na vikosi
vya ulinzi na usalama katika eneo hilo.