2012-10-08 14:45:54

Epukeni kishawishi cha kutaka kuzalisha watoto kwa njia za maabara!


Ndugu msikiliza wa Radio Vatican katika juma lililopita tuliona jinsi ugumba ulivyo kikwazo kwa matamanio ya wanandoa. Katika kupambana na kikwazo hiki wanandoa huweza kufikia kwenye hatua ya kuwa na kishawishi cha kutengeneza mtoto kwa njia ya maabara.
Ikumbukwe kuwa, Kanisa halipingani na jitihada za daktari za kuwasaidia wazazi kupata mtoto endapo jitihada hizo hazipingani na muungano wa kindoa, unaodhihirika katika tendo la ndoa kati ya mume na mke. Ila endapo jitihada zao zitatenganisha uzazi na muungano wa kindoa basi, Kanisa linapingana na uamuzi huo. Msimamo wa kanisa una lengo la kulinda thamani ya utu na heshima ya mtu ambao ni zawadi ya Mungu mwenyewe na hivyo, maabara hayana uamuzi wa mwisho kuhusu uhai pia kwa faida ya umoja wa familia yao.
Maendeleo ya kisayansi yamefikia mahali pa kuhamisha mbegu za kiume au yai la kike kutoka mmoja mwa wanandoa na kuziingiza kwa mwingine, ili kumtegeneza mtoto/watoto endapo mmoja kati ya wanandoa au wote wanaonekana kuwa na mapungufu katika mahusiano ya kindoa. Hali kadhalika mbegu hizi au yai, huweza kuchukuliwa nje ya mmoja kati ya wanandoa, au hata wakati mwingine nje kabisa mwa wanandoa wote wawili.
Mimba pia huweza kubebwa na mwanamke anayeajiriwa kufanya kazi hii tu na kisha kuzaa hukabidhi mtoto kwa wale waliomwajiri. Yapo pia majaribio ya kutengeneza mtoto kwenye chupa. Yaani kuchanganya viini mimba za kike na kiume katika chupa ndani ya maabara na hivyo kufanya mtu. Na mengine mengi ambayo yanaendelea kugunduliwa kila siku jinsi sayansi inavyoendelea kukua na kupanuka, hata wakati mwingine kupoteza dira na mwelekeo wa kimaadili na utu wema.
Kanisa kwa nyakati zote limefundisha kuwa njia yoyote ya uzazi inayotenganisha tendo la ndoa na uzazi sio halali. Mtoto sio kitu cha kutengeneza ila mtu mwenye asili yake na sura yake toka kwa Mungu mwenyewe. Mtoto sio kitu cha kutengenezwa ila mzaliwa anayetokana na upendo wa mke na mume katika tendo la upendo linalodai kujitoa kimwili mmoja kwa mwingine. Mtoto anapaswa kusema nipo kwa sababu wazazi wangu walipendana nami nimetokana na upendo wao ulibarikiwa na Mungu mwenyewe, sio kwamba, nipo kwa sababu mzazi/wazazi wangu wakishirikiana na daktari wametaka niwepo.
Kanisa pia limeendelea kupinga uzazi kwa njia ya maabara kwani, licha ya kutoheshimu muungano wa tendo la kindoa madhara mengine ya kutoheshimu uhai yameonekana katika kuchezea hivi viini mimba ndani ya maabara. Viini mimba visivyo hitajika huuawa au kutumika kama rasilimali za mazoezi ndani ya maabara ambayo si halali kutumika kwa mazoezi. Na pia udanganyifu waweza kuwa bayana ndani ya maabara.
Ndugu msikilizaji leo tuishie hapa, ili juma lijalo tutoe ushauri kwa wanandoa wagumba ambao sayansi ya kawaida haiwezi kuwasidia kuondokana na ugumba wao.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.