2012-10-04 12:41:51

Maelfu ya mahujaji yaanza kuelekea Jimbo Katoliki la Bukoba katika sherehe za kuhamisha masalia ya Kardinali Laurian Rugambwa!


Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, anaongoza umati wa waamini na watu wenye mapenzi mema, kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, kuelekea Jimboni Bukoba katika sherehe za kuhamisha Masalia ya Mwadhamana Kardinali Laurian Rugambwa kutoka kwenye maziko ya muda Parokia ya Kashozi, kutabaruku kwa Kanisa kuu la Jimbo la Bukoba sanjari na maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja tangu Kardinali Rugambwa alipozaliwa.

Maadhimisho yote haya kadiri ya mujibu wa ratiba yataanza hapo tarehe 6 Oktoba, m ajira ya jioni na kuendelea hadi tarehe 7 Oktoba 2012, asubuhi kwa Ibada ya Misa Takatifu.

Askofu Msaidizi Nzigilwa akihojiwa na Radio Vatican anabainisha kwamba, ushiriki mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa kuwajalia kiongozi aliyejitoa bila ya kujibakiza katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza wa Mungu nchini Tanzania. Ushiriki wao unapania pia kuendelea kumwombea ili aweze kupata tuzo huko mbinguni na Kanisa Katoliki Tanzania liendelee kushamiri kadiri ya mpango wa Mungu.

Askofu Msaidizi Nzigilwa anasema kwamba, msafara huu unawajumuisha: Mapadre, watawa na waamini walei kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, waliojiandaa kwa umakini mkubwa kushiriki katika tukio hili la kihistoria, kwa kuwahamasisha waamini kiroho na kimwili.

Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Laurian Rugambwa alizaliwa kunako tarehe 12 Julai 1912. Mara baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, alipewa daraja takatifu la Upadre hapo tarehe 12 Desemba 1943. Kunako tarehe 10 Februari 1952 aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo la Kagera Chini, utume alioufanya kati ya mwaka 1952 hadi mwaka 1953. Baada ya hapo aliteuliwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Rutabo kati ya mwaka 1953 hadi mwaka 1960.

Aliteuliwa kuwa Kardinali hapo tarehe 28 Marchi 1960. Akawa pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba kati ya mwaka 1960 hadi mwaka 1968. Alihamishiwa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuendeleza utume wake kuanzia mwaka 1969 hadi mwaka 1992. Alifariki dunia kunako tarehe 8 Desemba 1997.







All the contents on this site are copyrighted ©.