2012-09-28 16:10:13

Tafakari ya Neno la Mungu:Jumapili ya 26 ya Mwaka B


Masomo: Hesabu 11:25-29; Yakobo 5:1-6; Marko 9:38-42,45,47-48
Mungu asiyebagua, anayewapa wote wanaomwamini Roho wake. Kiini cha ujumbe wa masomo ya Jumapili hii ni kwamba watu wote waliobatizwa wamepewa kipaji cha Roho wa Mungu, na sio tu watu wa kikundi chetu au viongozi. Hivyo ishara ya mfuasi wa kweli wa Kristo ni kule kuonyesha huruma na kupokea vipaji vya wengine bila kubagua.

Kwenye somo la kwanza, tunaongozwa kugudua kwamba tunao kishawishi cha kujiona kama tu wazuri kuliko wengine. Mungu alikuwa amemwambia Musa achague wazee 70 watakaomsaidia kwenye kazi ya kuwaongoza watu wa taifa teule, kwasababu kazi hiyo ilikuwa imezidi sana. Basi Musa akawalete wale wazee pamoja ili awawekee mikono. Lakini wawili wao, Eldado na Medado walibaki kwenye hema wakati huo na wao pia wakatabiri ijapokuwa hawakuombewa. Wakati Joshua alisikia kwamba hao wazee wawili walitabiri kwenye hema, alikasirika kwa sababu wazee wawili wamepata kipaji cha unabii, hata ingawa hawakuwa pamoja na wengine sabini. Joshua alijaribu kuweka mipaka kwenye matendo na vipaji vya Mungu.

Jibu la Musa latukumbusha kwamba kazi la kueneza Habari Njema ya Mungu duaniani sio tu kazi la watu wachache teule Kanisani, bali ni ya wote. Basi “ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa nabii, na kama Bwana angewatia roho yake”.

Kwenye Injili ya Jumapili hii, mitume wamepata kipaji cha kuwafukuza pepo wachafu kwa jina la Yesu. Huko njiani walimwona mtu mmoja asiye wa kikundi chao akiwafukuza pepo wachafu pia kwa jina la Yesu, na wakamkataza kufanya hivyo. Yesu anawashauri mitume wake wasimkataze yeyote kwa sababu wao sio wa kikundi chao. Tukiangalia maneno ya somo la kwanza na mafundisha ya Yesu kwenye Injili, tutagudua kwamba hata sisi tuna wivu kama Yoshua na Mitume wa Yesu. Tunachukua Ukristo wetu kama chama au kilabu cha pekee ambapo wengine hawana haki kuingia.

Huenda wakati mwingine tukajisikia kama ni sisi tu tunao uridhi wa kiroho wa Yesu. Tunakubushwa kwamba Mungu hana ubaguzi. Roho wake haupewi tu wale wa kikundi chetu au viongozi peke yao. Kulingana na Mtaguzo wa Pili wa Vatikano, kazi ya uenezaji Injili ni wajibu wa wote, Mapadre na Walei pia. Hivyo kila moja wetu amepewa kipaji cha Roho Mtakatifu kwa ajili ya kazi hii kadiri ya cheo chake, ili Neno la Mungu lienee kote duniani.
Kuna ujumbe gani tungepeleka nyumbani Jumapili hii? 1) Ishara ya mfuasi wa kweli wa Kristo ni kule kuonyesha huruma na kupokea vipaji vya wengine bila kubagua. 2) Roho wake haupewi tu wale wa kikundi chetu au viongozi peke yao. Roho wa Mungu hakai tu katika Kanisa letu au katika dhehebu hili au ile. 3) Tunahimizwa tujaribu kushirikiana katika juhudi za uenezaji Habari Njema, kila mmoja kulingana na kadiri ya cheo au kipaji alichopewa na Mungu.
Imeandaliwa na Mons. John Mtiso Mbinda







All the contents on this site are copyrighted ©.