2012-09-25 10:29:36

Mwaka wa Masomo wazinduliwa Chuo Kikuu cha Mwenge Tanzania


Mahusiano na Mungu na watu wengine ni ya maana licha ya vyeti vyo vyote. Hayo yamesemwa na Askofu Isaac Amani wa jimbo Katoliki la Moshi. Askofu Amani ameyasema hayo alipokuwa akifungua rasmi mwaka mpya wa masomo katika chuo kikuu cha elimu cha Mwenge kilichoko mjini Moshi. Ufunguzi huo umefanyika siku ya Jumatatu tarehe 24 mwezi wa Septemba 2012.
Akiongea kwenye Misa Takatifu ya kufungua mwaka mpya wa masomo, Askofu Amani aliwahimiza wanafunzi wa chuo hicho Kikuu cha Mwenge kuyazingatia mafundisho ya Yesu Mwalimu ambaye ni Mungu anayeongea nasi katika lugha ya kibinadamu. Elimu hii ya Yesu ni kama taa inayotusaidia kutembea duniani tukiwa na mwanga wa ufahamu wa Kimungu.
Alisema Askofu Isaac Amani kuwa Neno la Mungu, Yesu, alitwaa mwili na kukaa kati yetu ili aweze kutufundisha sisi na kwamba sehemu kubwa ya muda wake hapa duniani aliitumia kwa kufundisha watu juu ya kuhusiana na Mungu na watu wengine. Askofu huo wa Moshi alisema kwamba Mungu ni uhusiano na kwamba binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu anazo pia hadhi na heshima na utukufu wa kiMungu; na kwamba mafundisho ya Yesu humpa mtu mbinu na upeo wa kumjua Mungu mwenye kuiongoza dunia kwa amri zake.
Askofu Amani aliongeza kusema kuwa wajibu wa Kanisa ni kumfunza mwanadamu apate kujijua yeye mwenyewe na kuijua pia thamani ya elimu ambayo ni chombo cha ukombozi na uhuru wote. Hivyo basi elimu ya kwanza ni ile ya kumjua Mungu, kuzishika amri zake, na kuusimamia ukweli. Elimu ingine ni ile ya malezi katika tabia njema na maadili. Ni vyema basi mwanadamu kunoa akili yake kwa elimu, usikivu, utafiti na ubunifu ili kuweza kuboresha mazingira yake.
Askofu Isaac Amani amewapa changamoto wanafunzi wote wa Mwenge kujifunza kisawasawa ili kwamba kama Kristo alivyo taa ya dunia, nao pia waweze kuwa Mwanga wa dunia kufuatana na wito wa Chuo hicho ambao ni Lux Mundi, au Mwanga wa Dunia.
Chuo Kikuu cha elimu cha Mwenge (Mwenge University College of Education) kilianzishwa mnamo mwaka 2005 na kiko chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki wa Tanzania. Chuo hico kinatoa shahada katika fani mbalimbali yakiwemo masomo ya sayanso na elimu. Wanafunzi wa Mwenge hutoka kote nchini Tanzania na nchi nyingine barani Afrika.

Mwandishi Sr. Bridgitta Samba.







All the contents on this site are copyrighted ©.