2012-09-22 14:15:14

Zihafamu nia za Mwaka wa Imani : Padre Flavian Kasalla


maadhimisho ya mwaka wa imani unaotarajiwa kuanza hapa mwezi oktoba mwaka huu. Sina shaka moja ya matarajio makubwa ni kuelewa sababu za kuuita mwaka huu mwaka wa imani. Maadhimisho ya mwaka wa imani ni sehemu ya safari ya Kanisa katika historia nzima ya ukombozi. Kwa utamaduni wake Kanisa nimekuwa likiweka malengo mbalimbali yanayolisaidia kama jamii ya Mungu kuingia katika ukweli wa mafumbo linayoyaadhimisha kila siku. Vipindi hivi vya tafakari huchukua sura mbalimbali kulingani na matukio na ndani ya Kanisa au historia ya Kanisa.

Natumaini tunakumbuka jinsi Kanisa lilivyoadhimisha mwaka wa mapadre na jinsi lilivyotumia nafasi hiyo kuichambua Sakramenti ya upadre, kukosoa mapungufu yanayoikabili huduma ya kipadre, kuwatia moyo mapadre na hatmaye kuweka mikakati mipya ya kuilinda na kuidumisha Sakramenti hiyo kama ilivyotakiwa na Kristo mwenywe. Pia Kanisa katika miaka ya karibuni limekwisha adhimisha mwaka wa Ekaristi Takatifu, mwaka wa rozari Takatifu, nk. Kwa namna ya kipekee kabisa na kwa upendo mkubwa baba Mtakatifu benedikto XVI amelitangazia Kanisa kipindi maalumu cha tafakari kitakachojulikana kama mwaka wa imani.

Katika kuendelea na kuiishi historia yake, Kanisa kwa namna ya pekee linakumbuka matukio makubwa mawili ambayo yamehusianishwa na mwaka wa imani. Kwanza ni kuadhimisha miaka hamsini ya kufunguliwa kwa Mtaguso wa Pili wa Vatikani (11 oktoba 1962). Pili Kanisa linaadhimisha miaka ishirini tangu kuzinduliwa kwa katekismu ya Kanisa katoliki (11 oktoba 1992). Matukio haya mawili yamechukuliwa na Kanisa kama nafasi ya neema inayoliwezesha kutafakari hali ya imani ndani ya Kanisa.


Katika adhimisho la kwanza linaloliingiza Kanisa katika mwaka wa imani, Kanisa ninatafakari Mtaguso wa Pili wa Vatikani ambao ulitambulishwa na Baba Mtakatifu Yohani XXXIII kama “kipindi cha kusambaza mafundisho sahihi na kamilifu, bila mkanganyiko wa tafsiri, ili kuyafikisha kwa uaminifu mafundisho ya imani yasiyobadilika kwa mahitaji nyakati zetu.” Mtaguso unafundisha katika hati yake ya Mwanga wa Mataifa (Lumen Gentium, 1) kwamba “Kristo ni mwanga wa mataifa. Kwa hali hiyo, Mtaguso uliokutanishwa na Roho Mtakatifu unahitaji kupeleka mwanga wa Kristo kwa watu wote, mwanga unaoonekana wazi katika Kanisa lake.” Katika kupeleka Mwanga huo wa Kristo Mtaguso ulichambua mazingira manne na kuyatolea hati maalumu kama mwongozo wa kuifikisha imani katika yakati zetu. Hati ya Kwanza ni ile inayoonesha kwamba mwanga wa Kristo unaonekana katika kila adhimisho la Liturjia Takatifu (hati ya Liturjia, Sacrosanctum Concilium). Hati ya pili inahusika na Neno la Mungu kama pia njia ambamo mwanadamu wa nyakati mbalimbali anakutana na mwanga wa Mungu yaani Kristo mwenyewe, (Hati ya Maandiko Matakatifu, Dei Verbum). Mtaguso unachambua pia kwa kina asili ya Ki-Mungu ya Kanisa katika hati yake juu ya Kanisa, (Hati juu ya Kanisa, Lumen Gentium). Na hati nyingine ni ile inayoonesha uhusiano kati ya Kanisa na ulimwengu kwa nyakati husika (Hati ya Kichungaji, Gaudium et spes). Ni katika hati hazi nne kwa kweli ambamo mafundisho mbalimbali ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani yamejengeka.


Katika tafakari ya mwaka wa imani inayotarajiwa kuanza hapo tarehe 11 oktoba 2012, kinachofanyika kwa kweli ni kusherehekea zawadi ya imani ambayo ni Mungu pekee anaweza kumkirimia mwanadamu. Kipindi hicho cha shukurani na tafakari ya kina juu ya imani, kinasindikizwa na programu mbalimbali ambazo zitahitimishwa hapo tarehe 24 novemba 2013 kwa adhimisho la sikukuu ya Yesu Kristo mfalme wa ulimwengu. Ni kipindi kinachotarajiwa kumwingiza muamini katika undani wa kuitabua imani yake iliyojengeka juu ya mkutano wake na Kristo Mfufuka.
Mwaka wa imani ni mwendelezo wa kuyaweka katika matendo mafundisho yote ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani. Ni kipindi cha tathmini juu ya mafanikio yaliyokwisha patikana kutokana na zawadi iliyotolewa na Mtaguso wa Pili wa Vatikani. Maadhimisho haya ya mwaka wa imani hayatakuwa ya kwanza ya kutambua nafasi ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani katika historia ya Kanisa. Mara tu baada ya Mtaguso wenyewe, mapapa wamekuwa wakiitisha sinodi mbalimbali ili kuangalia na kuongoza utekelezaji wa vipengele mbalimbali vya Mtaguso huo. Na hata katika adhimisho la mwaka huu wa imani bado baba Mtakatifu benedikto XVI ameitisha sinodi nyingine ya maaskofu wa dunia nzima ili kujadili juu ya uinjilishaji mpya sanjari na maadhimisho ya mwaka wa imani.


Mwaka wa imani ni kipindi pia cha shukrani kwa zawadi ya katekismu ya Kanisa katoliki. Katekismu hii ambayo inatimiza miaka 20 imekuwa ni msaada mkubwa wa kuikuza imani kulingana na mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikani. Baba Mtakatifu benedikto XVI anaiita katekismu hii kuwa ni tunda halali za Mtaguso wa Pili wa Vatikani na chombo sahihi cha kupokelea Mtaguso huo. Katikesmu ya Kanisa katoliki ni mkusanyiko wa mambo ya kale na mapya ambayo yote yako kwa ajili ya huduma ya imani ambayo haibadiliki huku ikimsaidia mwanadamu kupata mwanga mpya maishani.


Katika katekismu ya Kanisa katoliki, imani inachambuliwa katika mazingira matatu. Kwanza ni imani kama inavyoungamwa na kila muumini katika kanuni ya imani. Pili imani inaangaliwa katika maadhimisho ya kiliturjia Takatifu, na hasa maisha ndani ya Sakramenti mbalimbali. Tatu imani inajionesha katika maisha ya kikristo kama yanavyoongozwa na amri za Mungu. Na mwisho, ni imani katika maisha ya sala ya kikristo. Mafundisho haya ya kikatekesi ingawa yamekuwa yakifundishwa kwa karne nyingi tu, katekismu ya Kanisa katoliki inayachambua katika mtazamo wa mazingira na hali mpya ya wakati wetu. Hali hii ndiyo inayoifanya katekismu ya Kanisa katoliki kuwa chombo sahihi cha muungano wa kikanisa na njia sahihi ya kufundishia imani.


Kwa hali hiyo, mwaka wa imani unategemewa kuelekeza katika wongofu mpya na katika uvumbuzi mpya wa imani kwa Kristo ili kuwawezesha waamini wote kuwa mashahidi aminifu na wenye furaha wa Kristo mfufuka katika dunia yetu ya Leo. Ni shuhuda unaohusisha pia juhudi za kuwaongoza wengine wote kuelekea mlango wa imani ambaye ni Kristo mwenyewe. Katika kufikia imani ndani ya Kristo, kila mwanadamu anagundua kiini cha maisha, furaha na upendo wa kweli. Kipindi hiki cha neema kinacholielekeza Kanisa katika uinjilishaji mpya ndicho kinachojulikana kama mwaka wa imani. Ni kipindi cha kuvumbua kwa mara nyingine furaha ya kuamini na cha msukumo wa kuwashirikisha wengine imani.








All the contents on this site are copyrighted ©.