Papa safarini Lebanon- Salaam kwa wakuu wa Nchi , na ajibu maswali ya wanahabari
Ijumaa Baba Mtakatifu Benedikto XV1, akipita katika anga za mataifa mbalimbali , alipeleka
salaam zake za matashi mema kwa wakuu wa nchi alimopita. Kwa Rais wa Italia, , Mheshimiwa
Giorgio Napolitano alisema, ”Mheshimiwa Rais, ninapita katika taifa lako, nikielekea
Lebanon kama mhujaji wa amani na umoja. Ambako pia nitawasilisha waraka wangu wa Kitume
, juu ya maoni yaliyolewa wakati wa Sinodi ya Maaskofu niliyoiitisha maalum kwa ajili
ya kutazama kwa makini , hali ya maisha ya Wakristu katika mkoa wa Mashariki ya Kati
na msaada unaohitajika kujenga amani, umoja na matumaini katika mkoa huo. Papa
aliendelea kusema, ataendelea kutolea sala zake, kwa watu wa Italia ili waweze,
katika hali ya utulivu na amani, kupambana na changamoto zinazo wakabili nyakati
hizi. Vivyo hivyo, Papa alitoa salaam kama hizo, alipopita katika anga la Ugriki
, kwa Rais Enerico na kwa Rais Demetris Christofias wa Cyprus. Mkutano
na wanahabari Baba Mtakatifu pia akiwa bado safarini alijibu maswali
ya wanahabari, mengi yakilenga katika hali za ubabe wa kidini na ghasia zinazo onekana
nyakati hizi, Mashariki ya Kati. Wanahabri hao, walitaka kujua kama alikuwa na nia
ya kufuta ziara yake baada ya kusikia habari za ghasia hizi mara kwa mara. Papa
alijibu kwamba, hakuna hata mmoja aliye mshauri kufuta ziara yake na wala hakuwa
na wazo hilo, katika fikira zake , sababu alijua kwamba, kwa kadri hali inavyozidi
kuwa ngumu , ndivyo kunavyokuwa na umuhimu wa kutiana moyo, kujenga umoja na mshikamano
wa kidugu na wale walio katika hali za mahangaiko na mashaka. Na ndiyo maana aliitikia
mwaliko wa ziara hii, kwenda kujadiliana na kuzungumzia amani, kukataa ghasia na
fujo, na kutafuta jawabu la pamoja katika kukabiliana na matatizo yanayojitokeza.
Papa pia alijibu swali juu ya ongezeko la watu wenye imani kali isiyo vumilia
wengine, akisema kwamba utendaji huo ni kuihaini dini, kwa kuwa dini ni mwaliko wa
watu kushirikishana kupendana na kuishi kwa amani duniani kote. Alifafanua , kila
binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo ni lazima wote, mmoja kumheshimu
mwingine . Na ujumbe mkuu wa dini ni lazima ukemee aina zote za ghasia, hasa zinazo
fanyika kwa jina la dini. Kila dini inapaswa kuwa elimisha waumini, kuangaziwa na
kutakatifusha dhamiri , kwa ajili ya ukuzaji wa majadiliano, mapatano na amani. Na
alipoulizwa maoni yake juu ya kile kinachoitwa mapambazuko ya nyakati , katika nchi
za Kiarabu na udumishaji wa Ukristu katika mkoa huo ambako idadi ya Wakristu ni dogo,
alisema, ”katika mtazamo wenyewe, hamu ya demokrasia, uhuru na utambulisho mpya wa
Mwarabu, ni mambo mema katika juhudi hizo. Lakini haya yasiwafanye kusahau kipengere
cha kuvumiliana mmoja kwa mwingine”. Papa amesisitiza ule ukweli kwamba, uhuru wa
binadamu daima ni kushirikishana , na tu, huweza kufanikishwa, kupitia kutembea pamoja
katika njia thabiti ya umoja, kushirikishana , kugawa, na kuishi pamoja. Na hivyo
watu wote wanapaswa kufanya kila linalowezekana kuikubali dhana ya uhuru na hamu ya
uhuru huenda sanjari na uhuru wa kweli bila ya kupuuza uvumilivu na mapatano, vipengere
viwili muhimu katika kuwa na uhuru kamili. Na kwa upande wa Wakristu kuikimbia
Mashariki ya Kati, na hasa Syria na Iraki, Papa amesema, ni lazima kufanya kila
linalowezekana kusaidia Wakristu hawa kubaki katika nchi yao ya kuzaliwa. Na cha msingi
zaidi ni kusaidia kusitisha ghasia zinazoendelea, ambazo katika ukweli, si kwamba
ni madhulumu kwa Wakristu tu lakini pia kwa Waislamu na watu wengine wenye mapenzi
mema katika mkoa huo. Na hivyo inakuwa muhimu, kueneza ujumbe wa amani na maelewano
kati ya watu wa tamaduni mbalimbali kwa kuwa wote ni wana wa Mungu. Papa pia alitoa
wito wa kusitishwa kwa upelekaji wa silaha katika maeneo yenye machafuko. Aliuita
upelekaji wa silaha huo, kuwa ni dhambi kubwa. Ni lazima kukubali kuishi na wengine
licha ya tofauti za kitamaduni na kidini. Papa alifunga mkutano huo na wanahabari
kwa kutoa wito kwa wanasiasa kupata ufumbuzi wa kusitisha ghasia Mashariki ya Kati
. Na pia alitoa ombi kwa mashirika ya misaada ya ubinadamu, yaendelee kusaidia kwa
ukarimu, wote wanaoteswa na hali hizi za ghasia na madhulumu. Pia alikumbusha
umuhimu wa watu kuzama katika sala kwa uaminifu na uchaji , maana sala ya umma inaweza
kuwa na kishindo katika utoaji wa maoni ya umma. Sala inayotolewa kwa Mungu kwa uaminifu,
inaweza kutenda maajabu mengi.